
Na Steven Mshiu.
Habari za leo mpendwa rafiki. Naamini una uzima wa kutosha kabisa. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana kwa uzima huu tulio nao.
Leo tumeuanza mwezi wa nane ni matumaini yangu kuwa utakuwa ni mwezi wa ushindi mkubwa sana kwangu na hata kwako pia. Nakutia moyo endelea kuweka juhudi juu ya kile unachokifanya ili uweze kufanikiwa sana.
Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza kwanini huwa tunakwama au kushindwa jambo fulani? Ni wapi ambapo huwa tunakosea ili tujirekebishe? Lakini sikupata majibu. Baada ya kufikiri na kuwaza kwa muda mrefu ndipo nikagundua kuwa kuna kitu kinaitwa USHUHUDA.
Wakati nilipoamua kumkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, na kujiunga na kanisa linalomwabudu Mungu katika Roho na Kweli, Kipindi hicho nilikuwa darasa la saba. Nilikuwa bado ni mtoto sana. Umri kama miaka 12 hivi.
Nilipofika kanisani hapo, na ratiba za ibaada zikiwa zinaendelea kama kawaida ilifika kipindi cha watu kushuhudia matendo makuu ambayo Mungu amewatendea kwa wiki nzima, au mambo Mungu aliyotenda kwenye maisha ya waumini.
Niliona watu kama sita hivi wamesimama na kuanza kushuhudia. Kila mmoja alishuhudia jambo ambalo Mungu amemtendea. Kwakuwa nilikuwa bado ni mgeni sana sikuweza kuelewa ni kwanini watu wanashuhudia na kusema mambo waliyokutana nayo?
Baada ya kutoka ibadani, niliamua kumuuliza swali hilo mama yangu mzazi ambaye ndiye aliyenionyesha njia ya wokovu, na kwa bahati mbaya ni marehemu kwa sasa. Akaniambia, Mtu anaposhuhudia jambo ambalo Mungu amemtendea husababisha kuleta ushindi mkubwa sana. Kwa hiyo kushuhudia ni chanzo cha ushindi.
Niliridhika na majibu yale kuwa kushuhudia ni chanzo cha ushindi. Nakumbuka jambo lingine alilonisisitiza sana kuwa nisiache kusoma Biblia. Sasa siku moja wakati nasoma Biblia nikakutana na andiko kutoka Ufunuo wa Yohana 12:11, "Nao wakamshinda kwa damu ya mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda wao ambao hawakupenda maisha yao hata kufa"
Nilipoendelea kusoma maneno haya nilifarijika sana. Ukisoma mistari ya nyuma kwenye sura hii tunaona kuna vita inatokea huko mbinguni kati ya malaika Mikael na shetani, Ilikuwa sio vita ya kawaida. Lakini ushindi mkubwa unatokea baada ya yule joka kutupwa chini kabisa. Lakini chanzo cha ushindi huu ni lile Neno la Ushuhuda kama inavyojieleza kwenye mstari huo tuliouona hapo juu.
Tangu wakati huo nilikipenda sana kile kipindi cha watu kushuhudia katika ibaada.
Unajua unaposhuhudia huenda yuko mtu ambaye amekutana na changamoto kama yako, na amekata tamaa kabisa, akiamini kuwa Mungu hawezi kusaidia, Lakini anaposikia mtu akishuhudia kwamba Mungu amemtendea jambo, Imani ya mtu yule huinuka tena. Imani yake hujengeka tena.
Ngoja nikupe mfano mmoja,
Kipindi fulani alitokea mtu mmoja aliyeitwa Goliath, Mtu huyu alikuwa ni mbobevu wa vita kwa nyakati zile. Alikuwa ni mfilisti. Kwa muda mrefu taifa la Israel lilipigwa sana na mtu huyu Goliath, Katika makala zangu zilizopita nilishawahi kuzitaja sifa za huyu Goliath. Alikuwa ni mtu mkubwa sana kwa umbo(giant) au unaweza kusema alikuwa ni jitu.
Mtu huyu alisababisha adha kubwa sana kwa taifa la Israel. Majeshi yote ya Israel yalijificha mbele ya mtu huyu. Wanaume wote wa Israel waliingia mapangoni. Mfalme Sauli naye hakuweza kupambana na Goliath, japo naye alikuwa ni mtu wa vita.
Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Yese. Baba huyu alikuwa na watoto kadhaa na miongoni mwa watoto hawa walikuwa kwenye jeshi la Israel linalopambana na Goliath, Lakini nao walishindwa.
Yese alikuwa na kijana wake mdogo jina lake akiitwa DAUDI. Kwa kuwa Daudi alikuwa ni mdogo yeye hakuruhusiwa kwenda vitani badala yake alikuwa akichunga kondoo wa baba yake.
Wakati akichunga kondoo hao walijitokeza wanyama wakali kama simba na dubu wanaotaka kuwakamata kondoo wa baba yake hivyo Daudi alikuwa akipambana nao hadi kuwaua na kuwaokoa kondoo wale.
Siku moja Daudi alienda kuwaangalia ndugu kule vitani. Akakuta wamejificha. Goliath naye analitukana jina la Mungu, wala hakuna aliyejitokeza kupigana na Goliath..
Daudi akaamua kujitoa kupambana na Goliath. Kumbuka Daudi hana uzoefu wowote ule wa kivita kwa hiyo ilikuwa ni ngumu sana kuaminika. Kwanza ni kijana mdodo sana. Kaka zake wameshindwa. Yeye ataweza? Lakini Daudi alifahamu NGUVU YA USHUHUDA.
Alipopelekwa kwa mfalme Sauli, yawezekana Sauli aliona kama kijana anafanya utani. Hakumwmini kabisa. Daudi akaanza kushuhudia mambo aliyoyafanya. Akasema alipambana na simba hadi akamuua. Alipambana na dubu hadi akamuua, Hivyo Goliath ni kiumbe mdogo sana. Soma zaidi 1 Samweli 17:32-37
Sauli alimfahamu simba na dubu. Hawa ni wanyama hatari sana. Hivyo akamruhusu Daudi. Watu wote walihisi labda huo ndio mwisho wa kijana Daudi. Wakasahau kuwa tayari Daudi alishajitengenezea ushindi wake tangu zamani kwa njia ya ushuhuda. Sipendi niendelee sana ila sote tunafahamu kilichokuta Goliath. Alianguka kifudifudi mbele ya Daudi.
Mpendwa rafiki.
Nataka nikukumbushe mambo machache.
Mungu anapokutendea jambo usiache kushuhudia. Yaseme matendo makuu ya Mungu. Ushuhuda ni chanzo cha ushindi
Ushuhuda hujenga ujasiri. Na ujasiri unaojengeka kupitia ushuhuda humdhoofisha adui.
Mungu amekubariki chochote usiache kushuhudia. Kushuhudia ni njia moja mojawapo ya kuonyesha kushukuru. Mungu anampenda mtu anaeshukuru.
Pia kushuhudia ni njia mojawapo ya kumtangaza Mungu na kuutangaza ukuu wake. Unapomtangaza Mungu kwa njia ya ushuhuda humfanya Mungu kupata sifa. Mungu anaposifiwa yeye hushuka na uwepo wake.
Nikuhakikishie kuwa Mungu atakaposhuka na uwepo wake hutabaki vile ulivyo. Mungu aliposhuka kwa Daudi, Daudi hakuendelea kuchunga kondoo. Aliinuliwa hadi kuwa Mfalme. Kina Shadraki na wenzake walipoamua kumshuhudia Mungu hawakubaki kuwa watumwa. Yusufu alipoamua kushuhudia Mungu, hakubaki kuwa mtumwa. Aliinuliwa hadi kuwa waziri mkuu.
Ushuhuda wako ndio utakaokuweka pale ambapo wewe unataka. Utabarikiwa kulingana na ushuhuda wako. Utakula mema ya nchi kutokana na ushuhuda wako.
Changamoto tuliyo nayo ni kwamba je tunatengenezaje mambo ambayo yatakuwa na nguvu ambayo itakuwa ni ushuhuda mbele za watu na kwa Mungu wetu. Daudi yeye aliua simba na dubu. Haya yalikuwa ni majaribu makubwa sana kwake.
Ili utengeneze ushuhuda mzuri na wenye nguvu ni lazima kuyashinda majaribu makubwa unayokutana nayo. Kama utakuwa ni mtu wa kuanguaka anguka kwenye majaribu madogo madogo sahau kupata ushindi unaotokana na NGUVU YA USHUHUDA.
MUngu akubariki sana. Anza leo kufanya mambo yatakayotengeneza Ushuhuda wako.
Ushuhuda wako ni ushindi wako
Ni mimi rafiki yako,
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni