
Na Steven Mshiu
Moshi, Tanzania.
Habari mpendwa rafiki. Naamini umeamka vyema na tayari umeshayaanza majukumu yako ya kila siku. Na kama bado hebu fanya haraka, maana muda haukusubiri hata kidogo.
Leo nataka tukumbushane mambo kadhaa. Hivi unaahamu kama fikra na mawazo yetu ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo? Kile unachokiwaza au ulichokuwa ukikiwaza kwenye akili yako ndio matokeo unayoyaona leo.
Kuna vitu ambavyo tulikuwa tukivifikiri pindi tulipokuwa wadogo, lakini kadri siku zinavyokwenda haviwi kama tulivyokuwa tukifikiri. Vinabadilika na kutufanya nasi tubadili namna ya kufikiri.
Kipindi nikiwa na umri wa miaka minne, Hapo nimeshaanza kupata akili kidogo. Siku moja nilisafiri nikiwa nimeambatana na bibi yangu ambaye kwa sasa ni marehemu. Ilikuwa ni safari ndefu kidogo. Hivyo ilitulazimu kutumia usafiri wa gari la abiria aina coaster.
Kwa kuwa ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kupanda gari nilifurahi sana. Nilitamani kujifunza mambo mengi sana kupitia safari ile. Bibi yangu alitumia muda mwingi kunitajia majina ya maeneo na vituo kadhaa wakati tukiwa ndani ya gari lile. Kwakweli nilikuwa makini sana kumsikiliza ili na mimi nivielewe vituo vile.
Wakati safari ikiendelea mimi nikiwa ndani ya gari nilishangaa jambo moja tuu, Binafsi lilinisumbua sana akili maana halikuwa jambo la kawaida kabisa kwangu.
Nilishangaa kuona miti, nguzo za umeme, na baadhi ya mabango vikirudi nyuma tena kwa kasi.
Kwa kuwa sikupenda kuuliza kwanini inakuwa hivi mimi nikajiaminisha kuwa kumbe ukiwa ndani ya gari miti nayo hutembea. Nikaamini hivyo, na hata kama ningekutana na mtu akaniuliza basi ningemjibu hivyo.
Hatimaye tukafika kule tulipokuwa tukielekea lakini mimi tayari namna yangu ya kufikiri ni kwamba miti nayo hutembea. Lakini jambo lililoendelea kunichanganya akili ni wakati tunarudi kutoka kule safarini, nilishangaa kuiona tena ile miti ikirudi kule tulipotoka kwa kasi ile ile. Hapa ikabidi niulize.
Eti bibi, Mbona wakati ule hii miti ilikuwa inarudi nyuma kwa kasi, na sasa tumekutana nayo tena inarudi kwa kasi?
Ina maana miti nayo husafiri?
Akaniambia mjukuu wangu miti, wala hizo nguzo za umeme hazisafiri wala hazijahama pale zilipo. Kinachofanya uone kama miti nayo hutembea ni hii gari uliyopanda ndiyo inayotembea. Hapo ndipo namna ya kufikiri kwangu, na kuona kumbe nilikuwa nafikiri tofauti na namna inavyotakiwa kuwa. Hivyo bibi yangu akawa amebadilisha namna ya kufikiri kwangu. Tangu siku hiyo sijawahi kufikiri tena kuwa miti nayo hutembea.
Nataka nikukumbushe mambo haya ya msingi, huenda yakawa msaada kwako. Sote tuna namna ya kufikiri, Na kila mtu kuna jambo ambalo kwake analiona ni sahihi au yuko sahihi kifikra. Sawa sijakataa. Ila ni vyema ukainyambua akili yakili yako ikupe majibu je hicho unachokiwaza kipo sahihi? na kama hakipo sahihi ni hatua gani uchukue kuhakikisha kuwa kinakuwa sahihi?
Kama mimi nisingemuuliza bibi yangu yawezekana hadi leo ningekuwa naamini kuwa miti nayo hutembea. Unapoziamini fikra zako tu bila kutaka kujifunza ni kutafuta kupotea. Biblia inasema tutafute maarifa. Maarifa hayapatikani bure bure tu. Hupatikana kwa kujifunza.
Dunia inabadilika, na mambo nayo yanabadilika. Kama utabaki na fikra ulizokuwa nazo miaka mitano iliyopita, utaiona dunia kama sio mahali sahihi kwako kuishi. Kipindi kile tunauziwa sukari kilo moja kwa shilingi 800 lakini leo tunanunua kilo moja kwa shilingi 2500 hadi 3000, Ni lazima tubadili fikra zetu kutoka 800 hadi 3000.
Kama ulikuwa unafikiria kutengeneza kipato cha elfu kumi miaka hiyo, Hivi sasa ni lazima ubadili zile mbinu ulizokuwa ukizitumia kutengeneza elfu kumi, ufikiri mara mbili yake.
Kufikiri kwako ndiko kutakufanya ufanikiwe ama usifanikiwe. Uinuliwe ama usiinuliwe. Mtu mmoja akawa ananiambia eti wale ambao wako bize wanasema wanamtumikia Mungu ni kwamba wamekosa kazi ya kufanya. Nikamjibu unatakiwa kubadili namna ya kufikiri. Nikamuuliza mbona wewe huna mafanikio yoyote. Akaniambia eti hali ya maisha ni ngumu. Magufuli amebana. Nikamwambia pole sana. Fikra zako na mawazo yako ndio yamekufanya uwe jinsi ulivyo.
Yesu alipotaka kumponya mtu jambo la kwanza alianza kumbadilisha yule mgonjwa fikra zake. Alipokutana na mtu aliyekuwa pale birikani kwa miaka 38, akamuuliza unataka kupona? Yule mgonjwa fikra zake zilikuwa kwa malaika tu, kwamba pale maji yanapotibuliwa na malaika, basi mtu mwingine huwahi kule birikani na kupona ugonjwa wake.
Lakini Yesu hakuwa anahitaji maelezo yote hayo. Yeye alitaka jibu moja tu kutoka kwa mgonjwa yule kuwa "NDIO NATAKA KUPONA". Pale alipobadili namna ya kufikiri kuwa hakuna njia moja moja tu ya kupata uponyaji na akamuamini Yesu, Yesu akamwambia beba godoro lako na uende. Mara yule mtu akawa mzima.
Ningeweza kukuletea habari nyingi za watu ambao Yesu aliwatendea miujiza lakini ni baada ya kubadili namna zao za kufikiri.
Naamani alikuwa akifiri kuwa ukoma wake utapona baada ya kuwekewa mikono na nabii Eliya, Lakini anaambiwa akaoge Mto Yordan mara saba, alipobadili namna ya kufikiri kutoka kuwekewa mikono na kwenda kuoga Yoradan mara saba akapokea uponyaji.
Mitume wa Yesu walinogewa na mikate kipindi walipokuwa pamoja na Yesu, Hawakuelewa kuwa kuna wakati Yesu atawaacha, Yesu alipowaacha tu, ndipo akili zao zilipobadili namna ya kufikiri na kutambua majukumu yao. Wakaanza kuihubiri injili.
Mpendwa rafiki,
Nakukumbusha kuwa kuna siku hutakuwa hapo ulipo. Kile unachokitegemea hakitakuwepo. Leo upo kazini lakini kesho unaweza usiwepo kazini. Leo unasoma kesho utamaliza shule, lakini utakosa ajira. Badili namna ya kufikiri. Anza kufikiri endapo hutakuwa na kazi maisha yatakuwaje? Na kama unasoma ukakosa ajira itakuwaje. Leo una nguvu kesho zitapungua. Uwezo wa kufikiri nao utapungua.
Ni vyema ukatumia muda huu kufanya mambo yenye tija, ambayo pia yatasababisha fikra za wengine kubadilika.
Mungu akubariki kwa kuisoma makala hii, naamini kuwa utabadili namna ya kufikiri. Kama ulikuwa ukifikiri kwa kiwango cha chini sasa utaanza kufikiri kwa kiwango cha juu kabisa.
Fikra zako zitasababisha uweze kufika pale unapotaka.
Huna sababu ya kuishia njiani
Bali una kila sababu ya kuhakikisha unafikia Ushindi mkubwa.
Ahsante sana
Ni mimi rafiki yako.
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni