CHUKUA HATUA KUFIKIA KILE
UNACHOKIWAZA. KITALETA MAFANIKIO.
Na Steven Mshiu
Habari za wakati huu mpenzi msomaji wa makala zetu kupitia blog hii. Ni matumaini yangu kuwa u bukheri wa afya, hata mimi pia namshukuru Mungu kwa uzima alionipa..
Karibu tuendelee kujifunza na kutiana moyo kutokana na changamoto ambazo tunazipitia kila iitwapo leo katika maisha yetu. Nakutia moyo kuwa kila hali unayoipitia tambua ni kusudi la Mungu, na uamini kuwa ataifanya kuwa njema. Soma Mwanzo 50:20.
Leo katika mtiririko wa makala zetu natamani tukaangalie kuhusu KUCHUKUA HATUA KWA KILE UNACHOKIWAZA KWANI KITALETA MATOKEO MAZURI. Unajua watu waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali hususani biashara n.k, walikuwa na wazo na walipoamua kuchukua hatua za kulitimiza wazo lao lilileta mafanikio makubwa.
Hakuna mwanadamu aliezaliwa kwa bahati mbaya. Wote tuko kwa kusudi maalum, hivyo ni lazima tuchukue hatua za kulitimiza kusudi hilo. Watu wengi wana mawazo mazuri tena yenye kuleta mafanikio lakini kutokana na ile hali ya kuogopa na kukata tamaa, inafanya lile kusudi kutotimia. Na pia ni lazima uanze kuishi maisha ya kile unachokisudia.
Kama una ndoto za kuwa daktari, ishi maisha ya udaktari, una ndoto za kuja kuwa
mtu mkubwa katika nyanja mbalimbali, ishi maisha hayo. Itakuwa ni kituko
kikubwa au ajabu la nane la dunia kama unataka kuja kuwa rais halafu tukukute
kwenye vijiwe unacheza bao. Ni lazima uishi maisha ya kuja kuwa rais,. Chukua
hatua.
Ukisoma katika Biblia kitabu cha 2 Wafalme 7:3-10, utakutana na habari ya wakoma wanne, ambao walikuwa wametengwa, wamenyanyapaliwa, hawathaminiwi, walipoamua kuchukua hatua na kuingia mjini, nchi ilineemeka kupitia wao.
Lakini kama wangekaa na lile wazo lao tu bila kuchukua hatua, matokeo yake wangekufa wote kwa njaa. Kumbuka kitu hiki, Mungu anasubiria wewe uanze kuchukua hatua, halafu yeye aitimilize,. hawa wakoma hawakuwa na mikono, vidole na baadhi ya viungo vingine, lakini walipochukua hatua, Mungu akafanya kule kutembea kwao kuwa mshindo mkubwa kama wa jeshi kubwa. ila walikuwa wanne tu.
Rafiki yetu mpendwa, nikuhamasishe tu, bado hujachelewa, wakati bado upo. Hebu anza sasa kuchukua hatua kufikia kile unachokitaka. Kitaleta mafanikio. Una wazo la biashara, kufanya chochote, au hata kuandika makala kama mimi, hebu anza kuchukua hatua. Kumbuka hata mimi nilichukua hatua ya kuanza kuandika nilipopata wazo hili. Na ninaamini kuwa umejifunza mengi.
Woga wako ndio umaskini wako. Changamka chukua hatua. Dont die with your dream, make it to happen.
Ubarikiwe sana kwa kusoma makala hii. Na kama utakuwa na swali au kutaka ushauri usisite kuwasiliana nasi.
Mwandishi: Steven I. Mshiu
0655882074
Barua pepe:smshiu42@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni