Jumatano, 19 Aprili 2017

SIRI TATU ZINAZOWEZA KULETA USHINDI MKUBWA.
--------------------------------------------------------------------------
Na, Steven Mshiu.
Shalom mtu mwema sana wa Mungu. Naamini umekuwa na wakati mwema wa mapumziko mazuri ya kuikumbuka pasaka ambayo Yesu alitolewa au alijitoa kwa ushindi mkubwa ili kuleta ukombombozi wa mwanadamu.
Tunapoadhimisha siku hii tukumbuke kuwa Yesu yu karibu kurudi kulichukua kanisa au wale watakaokuwa na alama ya damu ya Yesu ktk mioyo yao. Damu iliyotuletea wokovu mkuu sana.
Jana niliweza kupata fursa na kibali cha kufundisha Neno la Mungu katika kanisani, hapa moshi-Mdawi, na niliweza kushirikiana ujumbe huu ambao ulikuwa baraka sana kwangu binafsi na hata kwa washirika wote.
Hivyo nimeona ni vyema nikakushirikisha nawe japo kwa kidogo tu.
Unafahamu kuwa hakuna ushindi unaopatikana kimiujiza ujiza. Hakuna ushindi unaotokea from nowhere. Ushindi unapatikana kwa kuvuja jasho, tena baada ya maumivu makubwa sana.
Matokeo ya ushindi ni kutuzwa. ILi mshindani aweze kutuzwa ni lazima ahakikishe anapambana hadi mwisho wa mchezo. Huwezi kuishia katikati ya mchezo halafu ukategemea kupewa zawadi. Hiyo itakuwa ni ndoto.
Yapo mambo mengi yanayoweza kuwa sababu ya kukuletea ushindi mkubwa sana, lakini kwa leo nataka nikuletee mambo haya matatu ambayo yamekuwa ni siri kubwa na yenye mafaniko kwa washindani.
#SiriYaKwanza.
UJASIRI. Unapoingia katika mashindano yoyote yale jambo la kwanza unalotakiwa kufanya ni kujivika ujasiri. Ujasiri ni kile kitendo cha kufanya jambo pasipo kuwa na woga, pasipo kuwa na hofu. Huku ukitarajia kuwa kuna matokeo mazuri yatakayotokea juu ya kile unachokifanya. Ujasiri unakupa uwezo wa kujiamini.
Ujasiri unakufanya umuone mshindani wako kuwa hana uwezo kama wako. Kwa wale mashabiki wa mpira wanaweza kukubaliana nami, maana timu zinapoingia uwanjani huingia kwa ujasiri mkubwa sana huku kila timu ikiamini kuwa ni lazima ishinde.
Kifo cha msalaba kilihitaji mtu jasiri. Mtu atakaekubali kudharauliwa na kuaibishwa kwa ajili ya makosa ya wanadamu. UJASIRI ndio kitu pekee kilichoweza kumfanya YESU aiistahimili hukumu ya kifo cha msalaba. Kitu kinachohafifisha Ujasiri ni maneno ya watu. Dharau kutoka kwa wanaokuzunguka. Unaweza ukapanga kufanya jambo fulani either biashara, lakini watu wanapoanza kukubeza na kukudharau ile hali ya kuthubutu inapotea na hatimaye unaingia katika hatari ya kulipoteza lengo na kusudi la wewe kuishi hapa duniani.
#SiriYaPili. KUSUDI KAMILI.
Hakuna mwanadamu aliezaliwa kwa bahati mbaya. Kila mwanadamu yupo hapa duniani kwa kusudi maalum. Katika dunia hii ya sasa yenye ushindani mkubwa kila nyanja inahitaji watu wenye kulitumika kusudi lao la kuwepo hai hadi wakati huu. Unapolitambua kusudi kamili ni lazima mabadiliko yatokee. Yesu alilitambua kusudi lake la kuja hapa duniani baada ya kuacha kila kitu huko mbinguni. Kusudi kuu lilikuwa ni kumwokoa na kumkomboa mwanadamu. Na hakukubali kuondoka hapa duniani kabla ya kulitimiza kusudi hilo.
Nawe pia unalo kusudi. Je utaondoka hapa duniani kabla hujalitimiza? Kumbuka kusudi kubwa la kuokolewa kwetu ni ili tumtumikie Mungu kama Yesu anavyotuagiza ktk Mathayo 28:18-20.
Baada ya utumishi huo thawabu yake inapatikana ktk Yohana 14 na 15. Mpendwa litumike kusudi hili. Tupo kwenye mashindano. Mpambano wetu ni juu ya shetani anaeibeza kazi ya msalaba. Ni lazima tupambane na tuhakikishe tunamshinda. Na tutapambana nae kwa kuitangaza habari Ya Msalaba. Habari za mshindi Yesu. Kwa kuwa Yesu alishinda Nasi tutashinda tu. KUSUDI KAMILI.
#SiriYaTatu. IMANI
Imani ni jambo kubwa sana na ni kitu cha muhimu kwa mwanadamu yeyote. Kila jambo linalofanyika na kuleta matokeo makubwa huanza kwa imani. Mkulima analima shamba, hakuna dalili yeyote ile ya mvua. Anaotesha mbegu ardhini tena kwenye vumbi. Imani yake kubwa ni kwamba mvua itanyesha na zile mbegu zitaoza na kuota na hatimae kuleta mavuno mengi. Mtu anaanza biashara kwa mtaji wa 50,000/= lakini anaamini kuwa kuna siku mtaji wake utakuwa mkubwa naatamiliki biashara kubwa. Tunawasiliana Na Mungu kupitia maombi ya imani. Imani anatufanya tuamini kuwa Mungu yupo. Tunaokolewa kwa imani tu, Imani yetu inatufanya tukubaliane na yale yote aliyotuagiza Yesu. Tunaamini kuwa kuna Makao ambayo yameandaliwa huko mbinguni kwa wale watakaoshinda. Imani Imani Imani.
Yonathani mtoto wa Mfalme Sauli alitumia siri hizi katika kitabu cha 1 Samwel 14:1-16. Aliweza kuwaletea Israeli ushindi mkubwa sana.
Jambo la msingi ni kuamini kuwa Mungu yupo pamoja nawe kwa kila unalolifanya kwa ajili ya kulitimiza kusudi. Na yuko tayari kukupatia ushindi mkubwa sana utakaokuwa historia kwa wale wanaokubeza.
Mungu akubariki sana.
(kesho nitakuletea sababu zinaokwamisha au kuchelewesha ushindi na namna ya kuzishinda)
@Steven Mshiu.
0655-882074
smshiu42@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...