Alhamisi, 10 Agosti 2017

KUTOAMINI NI DHAMBI INAYOUA

KUTOAMINI-DHAMBI INAYOUA
Na Steven Mshiu.
Habari za wakati huu mpendwa rafiki. Naamini umekuwa na siku njema ya leo. Hakika Mungu ni mwema kwetu maana anatuwezesha hata pale ambapo akili zetu zinafikia ukomo.

Ahsante kwa wewe ambaye unafuatilia makala zangu, naamini kuna kitu au vitu huwa unajifunza, kutiwa moyo na kuinuliwa tena. Sisi sote tu viungo katika mwili wa Kristo hivyo ni lazima tujengane kila iitwapo leo.
Tangu jumatatu sikuweza kuandika makala yoyote, lakini nilikuwa nikitafakari kila siku kuwa ni kitu gani Mungu anataka kuwakumbusha watu wake kwa wakati huu.

Juzi niliweka headline hii inayosema "KUTOAMINI NI DHAMBI INAYOUA. Hivyo tangu jumatatu nimekuwa nikijiuliza maswali mengi sana kuhusu IMANI,

Kipindi Yesu akiwa hapa duniani, akifanya huduma huku na kule akihubiri na kuponya wagonjwa alikuwa anakutana na changamoto nyingi sana.

Moja ya changamoto alizokuwa akikutana nazo ni juu ya suala la imani. Wako ambao imani zao za kupokea muujiza zilikuwa ni ndogo sana, Si kwamba Yesu alishindwa kuwaponya. La hasha. Kabla Yesu hajawaponya alianza kuziponya imani zao kwanza. Kama wewe ni msomi wa Biblia utaona mara nyingi Yesu alikuwa akiwaambia wale wagonjwa. Inuka. Jitwike godoro lako uende. Imani yako imekuponya,

Mara njingi sana Yesu alikuwa akiwaambia "Imani yako imekuponya". Namkumbuka yule mtumwa wa yule akida. Akida alipokwenda kwa Yesu akihitaji uponyaji wa mtumwa wake, Alipojenga imani yake kwa Yesu na kumwambia kuwa hakuna haja ya Yesu kwenda hadi nyumbani kwake akisema neno tu yule mtumwa atakuwa mzima. Yesu aliishangaa sana imani ya akida huyu. Kulingana na imani yake yule mtumwa akawa mzima.

Namkumbuka yule mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu kwa zaidi ya miaka 12. Akaamini kuwa atakapolishika pindo la vazi la Yesu tu, hakika atakuwa mzima. Ikatokea kama alivyoamini. Akawa mzima kulingana na imani yake.

Wako watu wanne waliokuwa na mgonjwa wao. Walizunguka kila mahali kutafuta uzima wa mgonjwa wao lakini juhudi zao zikagonga mwamba. Waliposikia habari za Yesu na matendo yake ya uponyaji, imani yao ikajengeka na kuwa kubwa sana. Wakiamini kuwa Yesu atamponya mgonjwa wao. Lakini wakakutana na tatizo la kusongwa na watu. Wakakosa nafasi ya kumfikia Yesu.

Nikukumbushe jambo moja la muhimu sana, imani huwa haiangalii gharama.
Wakaamua kukwea juu ya nyumba na kuanza kubomoa nyumba, yaani paa la nyumba ili tu wamfikishe mgonjwa wao kwa Yesu, Walipomaliza Biblia inaniambia Yesu alipoangalia imani ya wale watu akamponya yule mgonjwa.

Kiasi kile unachoamini ndicho kiasi sahihi cha mafanikio au matokeo uliyo nayo, Yule mwanamke wa Sarepta aliyeambiwa na Nabii atafute vyombo vya kuweka mafuta. Aliamini vile vyombo alivyotafuta vingemtosha, Na kweli alipokea mafuta kulingana na idadi ya vyombo aliyokuwa navyo, Najaribu kuwaza kama angetafuta vingi zaidi ndivyo ambavyo angepokea mafuta mengi zaidi.

Hadi hapa nikawa nimeziona faida nyingi sana za kuamini. Nikarudi kwa Naamani aliyekuwa mwanajeshi mwenye ukoma, Alipoambiwa akaoge mto Yordan mara saba, akataka kukataa, lakini aliposhauriwa imani yake ikakua alipoenda kuoga tu, ile imefika mara ya saba akawa mzima kabisa.

Mpendwa rafiki imani yako haiwezi kukua kama hakuna au huna kitu chochote kitakachoifanya imani yako kukua. Imani huanzia kwenye mambo madogo tu, au yale ambayo hayaonekani.
Katika Ebrania 11:1, Inatueleza kuwa imani ni kuamini au kuwa na uhakika kwenye vitu vinavyoonekana au visivyoonekana, Wengine wanasema ni kuwa na hakika. Naam nami naafiki.

Lakini sikuishia hapo kwa kupata tu faida za kuwa na IMANI. Nikajaribu kuwaza kuwa ikiwa mtu hataamini ninini kitatokea? Nikapata majibu kuwa ni lazima mauti imkute mtu huyo. Yohana 3:16-18, Biblia inasema kwenye mstari huu wa 18 kuwa "Aaminiye hahukumiwi, asiyeamini amekwisha kuhukumiwa kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

Kuhukumiwa inayozunguzwa hapa ni kule kuangukia jehanum moja kwa moja. Hukumu hii haina rufaa. Ukiangukia jehanam, Huo ndio umauti wa milele. Hivyo nikaamini kuwa kutokuamini ni dhambi inayoua.
Nilipoendelea kuyatafuta maandiko zaidi ndipo nikakutana kisa hiki cha ajabu sana cha akida mmoja katika kipindi cha Elisha.

Ilitokea kipindi fulani Elisha aliomba mvua isinyeshe kwa muda wa miaka mitatu na nusu katika taifa la Israel. Ikafikia hatua watu wanakula mavi ya njiwa na vichwa vya punda, Bidhaa hizi zilikuwa zikiuzwa ghali sana. Ilikuwa ni hali mbaya sana ya njaa kwa taifa la Israel,

Baada ya miaka mitatu na nusu kuisha Elisha anatoa unabii kuwa baada ya muda hali itakuwa shwari, Watu watakula na kustarehe, Lakini anatokea mlinzi mmoja wa mfalme, anatofautiana na Elisha, 2 Wafame 7:2, Akasema hivi Tazanma kama Bwana angefanya madirisha ya mbinguni je jambo hili lingewezekana????
Elisha anamjibu kuwa yeye ataangalia tu kwa macho wengine wakipata chakula, wale walioamini.

Mungu akaamua kuwatumia wakoma kuleta ushindi mkubwa juu ya taifa la Israel kwa kuwatisha washami wakakimbia wakaacha kila kitu kambini. Israel wakapata chakula kama neno la Elisha lilivyosema,
Cha kusikitisha yule akida ambaye hakuamini yeye aliwekwa getini kusimamia watu wakipata chakula. Msongamano ukawa mkubwa sana. Watu wakamkanyaga yule akida hadi akafa.
Kutoamini kwake kukamsababisha yule akida aone kwa macho tu lakini hakupata chochote zaidi ya kukumbwa na kifo. 2 Wafalme 7:17-19

Mpendwa rafiki,
Nataka nikukumbushe mambo machache.
Mungu hampendi mtu asiyeamini. Mtu asiyeamini hana muda wa kusoma Neno la Mungu. Imani huja kwa kusikia. Na kusikia Hutokana na Neno la Mungu. Kupitia Neno la Mungu huwa tunamsikia Mungu akisema na maisha yetu,

Imani husababisha mambo yatokee. Vitu vyote vinavyoonekana juu ya uso ni matokeo ya imani. Kumbuka imani ni matokeo ya Neno. Mungu aliumba kwa Neno(Imani) Tunaokolewa kwa kujenga imani yetu kwa Yesu. (Amwaminiye Mwana Yu na uzima tele).

Kutoamini kutakufanya ushuhudie wengine wakitendewa miujiza tu mwisho wake wewe utakufa bila kutendewa. Jifunze kwa huyu akida kwenye 2 Wafalme 7:18.

Kutokuamini kutakufanya wewe uwe daraja la wale wanaoamini katika kuelekea kupata kile wanachokiamini. Epuka dhambi ya kutokuamini sasa,

Nimalizie kwa kukutia moyo kuwa Yesu akamwambia Martha kuwa ukiamini utauona ukuu wa Mungu. Martha alipoamini na kuliondoa jiwe hakika Lazaro alifufuka.

Kuna mambo umeyaua mwenyewe kwa kutokuamini kwako. Lakini leo nakukumbusha kuwa ukiamini tu, yataenda kufufuka tena, jambo la kuzingatia ni kuliondoa jiwe la kutoamini tu ndani ya moyo wako.

Ahsante sana, Mungu akubariki na kukuinua tena wewe ambaye nimezungumza nawe.
Unaweza ku-share ujumbe na rafiki yako ukimkumbusha kuwa kutoamini ni dhambi inayoua, ili imani yetu ikue hatimaye kuiathiri dunia.

Rafiki yako,
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...