Jumatatu, 23 Oktoba 2017

HAKIKISHA UNAMALIZIA VIZURI

UKIANZA VIZURI HAKIKISHA UNAMALIZIA VIZURI.
Na Steven Mshiu,
Shalom mtu wa Mungu. Ninamtukuza yeye kwa kunijaalia pumzi ambayo siilipii hata senti moja. Hii ni neema ya kipekee ambayo nimepewa na Mungu. Naamini hata kwako umepewa neema hii.

Nikupe hongera na pole kwa mikiki mikiki ya kupambana na maisha haya ambayo kila kunapokucha yanakabiliwa na changamoto mbalimbali. Lakini kwa sababu tupo hapa duniani kwa kusudi maalumu ni dhahiri kuwa tutafikia mwisho mwema.

Nirudi kwenye kile ambacho nilitaka tukumbushane siku ya leo. Kama nilivyoanza kwa kichwa chenye maneno haya kuwa “UKIANZA VIZURI HAKIKISHA UNAMALIZIA VIZURI”, ina maana unaweza ukaanza vizuri na ukamalizia vibaya au ukaanza vibaya na ukamalizia vizuri au ukaanza vibaya na ukamalizia vibaya.

Jambo moja la msingi na la muhimu ni kujiuliza kuwa umeridhika na huo mwisho wako? Mwisho wako umekuletea matokeo chanya?. Kama umekuletea umekuletea matokeo chanya basi hongera, na kama umekuletea matokeo hasi ni wakati wa kukaa chini na kujitafakari ni wapi ambapo ulifanya vibaya ili uweze kuchukua NAFASI NYINGINE ya kufanya vizuri zaidi.

Leo kuna watu wanaanza mahusiano yao katika hali ya utakatifu. Ukiuangalia mwanzo wao unajisemea moyoni hawa watu ni lazima watafika mbali tu, lakini kadri siku zinavyokwenda ule utakatifu wa mwanzo unaanza kupungua kidogo kidogo. Ile nidhamu binafsi inapungua kidogo kidogo. Walikuwa na lengo la kufunga ndoa takatifu, mwezi mmoja kabla ya ndoa wanaanguka katika dhambi ya uzinzi.

Mwingine alianza safari yake ya wokovu, safari yenye uhakika wa kufika mbinguni, alihudhuria vipindi vyote kanisani, hakukosa ibaada hata siku moja, alikuwa mwaminifu kwa Mungu, lakini kadri muda unavyokwenda dunia na anasa zake zikaanza kumzuzua. Fasheni za dunia zikamponza, marafiki wakamponza, ile hali ya kumpenda Mungu ikaanza kuporomoka, mwishowe akamwacha Mungu kabisa. Mara nyingi pale tunaporidhika na mwanzo wetu na kujihakikishia kuwa hauhitaji kuboreshwa zaidi ndipo tunapoanza kuharibu na kutengeneza mwisho mbaya.

Yesu akasema kuwa ile saa tusiyodhani ndiyo saa ambayo mwana wa ADAM atakaporudi. Wengi tutakuwa hatujauandaa mwisho wetu maana tulishabweteka na mwanzo wetu.

Mpendwa hakikisha mwisho wako unakuwa ni mwema.
Isije ikawa tumeumia kuutengeneza mwanzo wetu halafu tukausahau mwisho wetu. Hivi ni vitu viwili vya muhimu vya kuangalia na kuzingatia.

Tunaposoma Biblia, leo nimekutana na kisa hiki cha mfalme Yosia, mwana wa Amoni, mwana wa Manase. Yosia alianza kutawala Yerusalemu akiwa na miaka nane. Kabla ya hapo alitanguliwa na baba yake alieitwa Amoni ambaye alifanya machukizo mengi mbele za Mungu kama alivyofanya baba yake Manase.

Wafalme hawa waliiacha njia ya Mungu wakaiandama miungu na ibaada za sanamu. Alipoingia ktk ufalme kinda huyu wa Amoni, baada ya babaye Amoni kuuawa, YOSIA hakutaka kuifuata njia ya wazazi wake. Akaamua kumuelekea Mungu, akadhamiria kumtafuta Mungu. Akaanza kuisafisha nyumba ya MUNGU ambayo ilitelekezwa kwa muda mrefu, akazivunja ashera zote na madhabahu zote za miungu ya wazazi wake.

Kwa ufupi alifanya matengenezo makubwa kati ya Mungu na wana wa Israel. Tunaweza kusema kuwa alifanya huduma ya utakaso. Ule upako na uwepo wa Mungu ukarudi tena juu ya Israel maana MUNGU alishakasirishwa na uovu wa MANASE na AMON. Yosia akawa amefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika ufalme wake.

Na kwa kuwa mfalme huyu alienza kutawala akiwa na umri mdogo sana, alianza vizuri na Mungu wake, Mungu alimstarehesha sana, hakuna sehemu inayosema kuwa kuna maadui walioinuka ili wapigane na ufalme wake. Biblia inasema katika 2 Wafalme 23:25, Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake aliemwelekea BWANA Kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote na kwa nguvu zake zote sawasawa na sheria zote za Musa wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.

Ni kweli kabisa anahitaji kupongezwa.
Sasa je mwisho wake unakuwaje?
Baada ya Mungu kumneemesha mfalme huyu, kumstarehesha kila pande, akaamua kujitia kiherehere cha kuingilia vita isiyomhusu. Ukisoma katika 2 Wafalme 23:29, Farao-neko mfalme wa Misri anainuka kupigana na mfalme wa Ashuru, haya ni mataifa mawili tofauti kabisa na israel/Yerusalemu,. Lakini Yosia akaenda ili apigane. Huyu mfalme wa Misri akamuua Yosia.
Huo ukawa mwisho wa kizembe kabisa wa mfalme Yosia ambae alianza vizuri hadi kusifiwa na Mungu.

Mpendwa mtu wa Mungu kuna mambo mengi sana kujifunza hapa:
1. Ni mambo mangapi tulianza vizuri lakini kadri siku zinavyokwenda tunatengeneza mwisho mbaya?
2. Je pale tunapogundua kuwa mwisho wetu unakuwa mbaya ni hatua gani za kuchukua?
3. Je tunabweteka na mwanzo wetu, na kujihalalishia kuwa sisi tumeshakamilika hivyo tuna uwezo wa kujiongoza wenyewe?
4. Je tuko tayari kuyaacha yale yote yanayosababisha mwisho wetu kuwa mbaya?
5. Je tunatambua kuwa Mungu anafahamu mwanzo wetu na mwisho wetu, ila ametupa "option" ya kuchagua tuanzeje na tumalizieje?
Mungu akubariki sana.
Nakutakia tafakari njema
#USIISHIE_NJIANI
Imeandikwa na
Steven Mshiu,
0655-882074
au baruapepe smshiu42@gmail.com
Oct 20, 2017

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...