
Na Steven Mshiu
Nimefika ofisini mapema leo hii asubuhi. nikaukumbuka wimbo wa Ambwene unaosema "TANGULIA MBELE". Nimetumia zaidi ya nusu saa kuusikiliza huku nikitafakari mambo mengi sana.
Kwenye wimbo huu amemzungumzia ndege aina ya TAI.
Tai ni miongoni mwa ndege wakubwa sana tena wa ajabu. Mazingira ambayo Tai wanaishi ni tofauti kabisa na mazingira wanayoishi ndege wengine.
Tai hujenga kiota chake mahali ambapo hakuna chochote kile kinachoweza kumdhuru kufika. Hujenga kwenye maporomoko makali sana. Ni vigumu sana kwa nyoka na hatari nyingine kufikia kiota hicho.
Tai ni ndege anaeweza kuruka juu sana kuliko ndege wengine. Ni ndege aliyebarikiwa hekima na busara nyingi sana.
Lengo la Tai kufanya hivyo ni kuhakikisha usalama wa uzao wake.
Wakati anapojenga kiota chake, hutanguliza miiba mikali halafu kwa juu huifunika ile miiba kwa manyoya yake, Hivyo yale makinda yake yanapokaa pale kwenye kiota hufurahia sana joto la yale manyoya na hayafahamu kama kuna miiba kwa chini,
Mama yao hufanya juhudi kubwa sana kuyatafutia chakula, na pale anapokosa hujitoa manyoya upande wa chini wa tumbo lake hivyo anapokuja kukaa karibu na makinda yake huanza kula nyama kutoka kwenye mwili wa TAI huyo,
Kadri siku zinavyokwenda yale makinda hupata nguvu. Hufikia wakati yakajitafutie chakula. Mama huanza mafunzo rasmi. Kwanza huyanyima chakula ili yatoke pale kwenye kiota. Yanapokataa kutoka mama yao huyapuliza yale manyoya hivyo ile miiba huanza kuyachoma yale makinda.
Huanza kutoka bila kupenda. Mama yao huyachukua hadi juu sana halafu huyaachia. Yale makinda yanaporuka huruka bila muelekeo. Huweza kuhisi kama mama yao anawachukia. Yanapofikia hatua ya kuishiwa nguvu, Mama yao hutokeza kwa mbele na kuyanyaka.
Hapo ndipo hugundua hekima na upendo wa mama yao
TUNAJIFUNZA NINI KUHUSU TAI??
Mungu kwetu yeye ni kama TAI, sisi ni makinda yake. Aliandaa mazingira mazuri sana kwa ajili yetu sisi kuishi. Lakini alifahamu kuwa humu duniani kuna majaribu ya kila aina. Na mpango wake sio tuangamie kenye majaribu hayo.
Anasema hakuna jaribu linalompata mtu linalozidi uwezo wake.
Lengo la majaribu hayo ni kutupa mafunzo ya kuweza kuimarika katika imani ili tuendelee kumtegemea yeye.
Mara nyingi tunaweza kuishi bila kutambua kuwa kuna changamoto au majaribu, Hii ni kwa sababu ya neema ya kipekee ya Mungu. Unaweza kuishi bila kujua njaa ni nini. Unaweza kuishi bila kujua shida ni nini?
Hivyo Mungu huondoa ile neema ili utambue kuwa yeye ni nani na ufahamu upendo wake kwetu ukoje. Kama vile Tai anapoyanyima makinda yake chakula ndivyo ilivyo Mungu wetu aanapotupitisha kwenye jaribu. Pale unapoleta kiburi huondoa kile kitu ambacho kinakupa kiburi hivyo hukulazimu kutoka tuu.
TAI huyapuliza yale mmanyoya hivyo yale makinda hutoka pale kiotani tu.
Mungu anataka tutoke, tukalitimize kusudi lake. Lakini sisi tumeng'ang'ania kwenye kiota tu. Tulipookoka tu tulilibeba kusudi la Mungu la kuufikia Ulimwengu. Pale tunapofika kanisani tunajiona kama tumefika. Hapana tunatakiwa kutoka.
Akili zetu haziwezi kukua kama tutaendelea kubaki kwenye kiota. Tutaendelea kulishwa tu. Ifike mahali nasi tutosheke kulishwa nasi tukalishe.
Hivyo mpango wa Mungu kutupitisha kwenye majaribu, mwanzoni tunaweza kuona kama Mungu anatuonea lakini pale tunapoanza kupita katika jaribu hilo na tukaonyesha kumhitaji yeye, yeye hutupa nguvu za kustahimili jaribu jaribu hilo
Na hatimaye hutuinua na kutuweka katika viwango vingine.
Nikukumbushe jambo moja la muhimu. CHANGAMOTO sio zakukuumiza bali ni za KUKUIMARISHA.
Steven Mshiu
Nov 10, 2017
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni