
Na Steven Mshiu
Natamani nimtie moyo mtu mmoja ambaye anaona amekwama na kila akiangalia mbele haoni mpenyo. Kila kona amezungukwa na maadui, watu wanakunenea mambo ya ajabu.
Unaishi kwa wasiwasi kutokana na vitisho vya adui zako. Umekata tamaa kabisa kwa kuwa huoni msaada wowote.
NISIKILIZE.
Mfalme Senakerbu aliyekuwa akiitawala Ashuru ambayo kwa sasa ni Siria, aliinuka na kuanza kuipiga baadhi ya miji ya Yuda kisha akaitwaa. Mfalme huyu wa Ashuru au Siria hakuwa anamfahamu Mungu kabisa.
Aliabudu miungu, na inasemekana kwamba miji hii aliyofanikiwa kuiteka nayo pia walikuwa ni waabudu miungu ambayo ni kazi za mikono ya wanadamu.
Baada ya kufanikiwa kuiteka miji hii akadhamiria kuiteka Yerusalemu ya Israel iliyokuwa ikitawaliwa na Mfalme Hezekia.
Historia ya Hezekia kwa kifupi ni kwamba alikuwa ni miongoni mwa wafalme waliokuwa wakimfahamu MUNGU wa kweli. Kila alichokifanya alitegemea msaada wa MUNGU, Hakufanya chochote kile bila kumuuliza Mungu. Kwa ufupi alimtetea na kumdhihirisha Mungu wake, kuwa ni MUNGU WA MSAADA.
Huyu Senakerbu akatuma waraka kwa taifa la Israel ili kuwavunja moyo, kuwa Hezekia anawadanganya kuwa huyo Mungu wake hawezi kuwatetea, hivyo mje kwangu ili muwe watu wangu, maana yake taifa la Israel liwe watumwa kwa Ashuru chini ya mfalme Senakerbu.
Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa Hezekia kutokana na Senakerbu kuwa na nguvu kubwa sana ya kijeshi. Hezekia hakuona popote pale ambapo angeweza kupata msaada. Baada ya kupata ule Biblia inaniambia kuwa Hezekia alirarua mavazi yake ya kifalme akavaa magunia na kuanza kumtafuta Mungu wake.
Alitambua kuwa hakuna mtetezi mwingine zaidi yake. Mfalme akaingia magotini kumwomba MUNGU. Ona maombi yake katika Isaya 37:15-20, moja kwa moja tunaona ni namna gani mfalme huyu alivyokuwa akimtetea Mungu wake.
Mungu anapenda kutetewa, anampenda mtu aliye tayari kujitoa kwa ajili yake. Niweke sawa jambo moja, Ninaposema kuwa Mungu anapenda kutetewa simaanishi kwamba yeye ameshindwa kujitetea mwenyewe. La Hasha. Anatamani aone mwanadamu anaweza kusimama upande wake kwa kiasi gani.
Mungu alimuumba mwanadamu kwa ajili ya utukufu wake. Hivyo mwanadamu anapofurahia kazi ya muumbaji wake na kuwa na wivu naye Mungu hujisikia vizuri sana, Kule kumtetea Mungu humfanya ashindwe kutulia katika kiti chake cha Enzi hivyo hushuka na kututetea sisi pale tunapokuwa tumeshindwa.
Kutokana na ujasiri huu wa Hezekia kumtetea Mungu wake, Katika sura ya 37: kuanzia mstari wa 21, Mungu anajibu au anajitokeza ili kumtetea Hezekia. Kwa kifupi ni kwamba hapa Hezekia aliuza kesi yake kwa Mungu. Hivi unafikiri Mungu atamfanya nini huyu Senakerbu? Kwanza alitukana Mungu, Akamtisha Mtu anaemtegemea Mungu. Akamuona Mungu kama ni vile vimiungu alivyoviharibu ambavyo vilitengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
Kuanzia mstari wa 29, Mungu anaanza kusema vile atakavyomtenda huyu Senakerbu, kwanza atamfunga pua na huo mdomo unaomtukana Mungu, Ukizibwa pua na mdomo sidhani kama unaweza kuishi kwa zaidi ya dakika kumi. Lakini pia hataweza kutimiza azma yake ya kuiteka Yerusalemu kwani Mungu anasema atamrudisha kwa njia ile ile aliyoijia.
Mungu akamtoa Hezekia wasiwasi na kumhakikishia kuwa ATAMTETEA na ataulinda ule mji na kuuokoa. vs 35
Kilichomkuta Senakerbu sio kizuri, Isaya 37:36, watu wanaamka asubuhi zaidi ya watu laki na themanini wamekufa haijulikani waliuawa na nani , Senakerbu naye akiwa anaabudu miungu yake(Niskori) wanawe walimtokea na kumuua kwa upanga.
Hali ikawa shwari kwa Hezekia.
Inawezekana hata kwako maadui zako wameinuka kwa ajili yako hebu mwombe MUNGU akutete.
Yale ambayo unayaona ni mazito kwako kila ukiwaza unaona hakuna njia kabisa Biblia inasema katika Zaburi 37:1-7 MKABIDHI BWANA NJIA ZAKO na MAWAZO YAKO YATATHIBITIKA
pia anasema ni jambo gani ambalo yeye hawezi. Hapana. Anaweza kila jambo,
Mathayo 11:28-29, Anasema kuwa Mizigo yetu tumtwike yeye(YESU) kwani nira yake ni laini na mzigo wake ni mwepesi. Yeye peke yake ndiye mtetezi anayeza kuleta furaha na raha ya nafsi. Huyu ndiye aliyemletea Hezekia furaha ya nafsi yake. Hata wewe anaweza kukuletea raha ya nafsi yako.
Lile unaloliona ni gumu lisukumize kwa Mungu, Hakika yeye ndiye mtetezi wa haki. Wanadamu wanaweza kukutetea lakini watakudai uwalipe, Lakini Mungu ndiye MTETEZI pekee asiyetaka malipo zaidi ya kumsifu na kurudisha sifa na utukufu kwake.
Ubarikiwe sana mtu wa Mungu. Inuka. Sio wakati wa kukaa tena chini. Sio wakati wa kusononeka tena. Tafuta kutetewa na Mungu..
Tafuta kuipata RAHA ya nafsi yako.
Nikutie moyo kuwa "BWANA ATAKUPIGANIA NAWE UTANYAMAZA KIMYA"
Steven Mshiu
0655-882074
Nov 13, 2017.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni