Jumatano, 28 Juni 2017

KUNA HAJA YA KANISA KUOMBA KWA AJILI YA VIJANA



KUNA HAJA YA KANISA KUOMBA KWA AJILI YA VIJANA
Na Steven Mshiu.
Siku mbili zilizopita nikiwa katika tafakari yangu binafsi juu ya mustakabali wa maisha yangu kama kijana, nilijihoji maswali mengi sana.
Katika maswali niliyojihoji ni kuwa mimi ni nani? Ni kitu gani natakiwa kufanya nikiwa kama Kijana? Je jamii inautambua mchango wangu? Ni Kwa kusudi lipi nipo hai hadi leo? Kanisa linatambua nafasi yangu kama kijana? Je naitendea haki nafasi yangu?
Biblia inamzungumziaje kijana? Kwa nini nyakati hizi vijana wengi hawana muda na Muumba wao?
Kwanini vijana wengi tunajikuta tumeshaangukia katika kutenda dhambi? Tatizo liko wapi? Je ni hatua gani za kuchukua ili kuweza kutatua tatizo hili?
Baada ya kujiuliza maswali haya na mengine mengi tu, nikajumlisha na utafiti wangu mdogo nilioufanya kwa muda mchache sana ambao nilibaini mambo kadha wa kadha kuhusiana vijana.
Mambo niliyoyabaini ni kwamba, Kwa nyakati hizi vijana wengi hasa waliopo kwenye makanisa ya kiroho wapo kwenye mahusiano yasiyo rasmi kabisa. Mvulana na msichana wanaishi kama tayari walikwisha oana siku nyingi tu, Binti yupo tayari kwenda kwa kijana tena mwenyewe na wanaweza kukaa hata kwa muda mrefu wakiwa wenyewe tu. Hata the way, wanavyotembea, maongezi, na michezo yao inaakisi mahusiano yasiyo rasmi kabisa.
Pia nilibaini asilimia kubwa ya vijana hawaendi kanisani. Hawana muda wa ibada. Nilitembelea kanisa moja ili kuzungumza na vijana ila nilikuta vijana 12 tu, wa kiume wanne(4) na mabinti 8, Nilipowauliza kuna vijana wangapi kanisani hapo niliambiwa wapo 37, maana yake ambao hawajaenda kanisani siku hiyo ni mara mbili ya walioenda kanisani siku hiyo.
Kati ya hao vijana 12., niliowakuta, vijana 7 hawakuwa na Biblia, vijana watatu walikuwa na Biblia kubwa, wawili walikuwa na zile za Agano jipya tu.
Kati ya hao vijana 7 ambao hawakuwa na Biblia, vijana wanne walikuwa na simu za Smartphone zenye memory card, na nyimbo nyingi sana za Bongo Fleva. Vijana watatu wao walikuwa na simu nyingine nzuri tu, zenye thamani ya zaidi ya elfu 40.
Hivyo nikagundua kuwa vijana wengi hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu.
Kingine Nilichogundua ni kuwa vijana wengi hawajui kuomba. Nilimsimamisha kijana mmoja ili aombe, aliomba kwa sekunde 57, tena kwa kunong'ona. Binafsi sikumsikia kabisa.
Yapo mambo mengi niliyoyagundua ikiwa ni pamoja na vijana wengi kutokupenda maonyo au kukemewa pale wanapokosea. Kutokuhusika na huduma yoyote wawapo kanisani. Utakuta binti amejipara akapendeza kuliko hata nyanya, lakini hawezi hata kuimba pambio la sifa, haimbi kwaya, hafundishi hata watoto. anakuja kanisani kwa kuchelewa. Anakuta kiti kimefutwa. Anakaa tuu. HAlafu mchungaji akimaliza mahubiri anaita vijana mbele "Haya wale ambao Wanahitaji Mungu awatendee muujiza wa kupata mume au mke watoke mbele niwaombee" Bila aibu unainuka unaenda kuombewa. My friend. Unasubiri U-download huyo mchumba kutoka google au?
Kingine nilichobaini ni kuwa vijana wengi tunachelewa kuingia kanisani. Kijana hana mtoto, hana kuku, hana mbuzi yani hana shughuli yoyote ile lakini anachelewa kanisani.
Sasa basi nikawaza nini kifanyike ili kuweza kumrudisha kijana katika mstari.
Katika Zaburi 119:9 Biblia inasema, "Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Ni kwa kutii na kulifuata Neno lako(MUNGU)
Kumbe njia za vijana zimechafuka. Zimechafuliwa kwa uzinzi, Zimechafuliwa na anasa za dunia hii. Sasa dawa ni kutii na kulifuata Neno la Mungu.
Zaburi 119:11, "Moyoni mwako nimeliweka Neno lako ili nisije nikakutenda dhambi. Dawa ya kuepuka dhambi ni kuliweka Neno la Mungu moyoni. Huwezi kuliweka Neno moyoni kama husomi Biblia. Huwezi kusoma Biblia kama huna. Nunua Biblia na anza kuisoma.
Katika Mhubiri 12:1-14, Sulemani aliyekuwa mfalme mwenye hekima hata Biblia inathibitisha hivyo, ameandika mambo mengi sana kuhusu maisha ya ujana. Anasema kipindi cha ujana ndicho kipindi cha kumkumbuka Muumba maana kuna siku zinakuja ambazo utatamani kufanya mambo lakini itashindikana
Hutaweza kuonda raha tena. Maana meno yatakuwa yameshaanza kung'ooka mdomoni. Hizo nywele ambazo unatumia zaidi ya masaa sita sijui kusuka na saloon, kichwa chote kitajawa mvi, Leo unaona kufunga kilemba ni ushamba nyakati hizo wala hutaambiwa ufunge kilemba. Actually ni nyakati mbaya sana. MKUMBUKE MUUMBA WAKO.
Tambua kuwa wewe ni wakili wa Kristo. Katika 2 Korinto 5:20, Biblia inasema kuwa, " BAsi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo. Kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu, twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Vijana tumepewa jukumu la kuupatanisha ulimwengu na Mungu. Na kazi kubwa hapa ni kuwepo kwenye huduma.
Katika makala zangu za nyuma niliwahi kuandika "MAMBO SITA ANAYOTAKIWA KUWA NAYO KIJANA ILI AWEZE KUKUBALIKA KATIKA JAMII" Ukisoma katika 2 Timotheo 4:11-12, Hapa ziko sifa kadhaa anazotakiwa kuwa nazo kijana yeyote yule. Unapokuwa na sifa hizi hakika jamii itakutambua, kanisa litakutambua, pia utaheshimika.
Katika 1Yohana 2:13b, anasema "Nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule mwovu"
14b anasema tena "Nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu mna nguvu, na Neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu"
Neno kumshinda mwovu limerudiwa mara mbili katika sura hii moja. Nguvu ya kumshinda mwovu inapatikana kwa kusoma Neno la Mungu na maombi. Tambua kuwa Mungu amekupa nguvu ili umtumikie yeye,
Mafanikio ya huduma ya Timotheo ni kwa sababu alikuwa ni mtu wa kumtumikia Mungu. Muda mwingi alikuwa akitumika na Paulo. Alikubali maonyo, licha ya kuwa alikuwa ni kijana. Pia Timotheo huyu aliyaishi malezi ya wazazi wake kama Paulo anavyosema katika 2Timotheo 1:1-6,
Nafasi ya watumishi wa Mungu kwa vijana.
Wachungaji na watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya kuweza kuwarejeza vijana kwenye mstari. Ni kwa njia ya maombi tu.
Hezekia baada ya kuota kiburi na kumsahau Mungu, Mungu alimtuma Isaya amwambie kuwa atakufa. Hivyo atengeneze Mambo ya nyumbani kwake. Hezekia akatubu na kuomba rehema. Mungu alimponya lakini kupitia utendaji wa mtu mwingine ambaye ni Daudi. Soma Isaya 38:5. Ikiwa na maana kuwa tayari kuna maombi ambayo Daudi aliyaomba akiwa kama Mtumishi wa Mungu, hivyo yakafanyika kama chanzo cha uponyaji wa Hezekia.
Isaya 37:35, Mungu anasema ataulinda mji huu na kuuokoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya DAUDI MTUMISHI WAKE.
Ina maana katika nji huo kuna juhudi za maombi ya Daudi
Hivyo watumishi wa Mungu watakapoweka juhudi kubwa za maombi ya kuwakomboa vijana juu ya baa hili la kuangukia mikononi mwa shetani, Hakika Kwa maombi yao Mungu atawaponya vijana.
Jambo la mwisho kwetu sisi vijana wenyewe. Tukumbuke kuwa tunahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu katika Maisha yetu, Hatuwezi kumshinda mwovu kama hatuna roho mtakatifu, hatuwezi kuushinda ulimwengu kama hatuna Roho Mtakatifu. Licha ya kumhitaji Roho Mtakatifu katika maisha yetu, Huyo Roho Mtakatifu ndiye atakaehusika katika unyakuo.
Nina mengi ya kuandika ila naamini kwa haya machache umejifunza mengi. Mimi pia kama kijana nimejifunza na kuyatendekea kazi.
Natamani umshirikishe mwenzako unaemfahamu kuwa ni kijana, iwe ni kwenye groups au popote ili kila kijana apate ujumbe huu, ili abadilike.
Ahsante na Ubarikiwe sana.
Makala hii imendikwa na;
Steven Mshiu,
Mwandishi, na mwalimu wa Neno la Mungu,
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...