#USIISHIE_NJIANI
USIJIDHARAU.
Na Steven Mshiu.
Nina kila sababu ya kumtukuza na kumuinua Mungu wa mbinguni
kwa kunipa nguvu na afya tele. Mungu ametupa wiki nzuri ambayo ni ya ushindi
mkubwa kwako wewe uliyedhamiria kuupata. Jambo la msingi ni kuweka juhudi kubwa
juu ya kile unachokifanya ambacho kina matokeo chanya. Mara nyingi huwa napenda
kusema kitu chenye matokeo chanya maana unaweza jikuta unafanya vitu ambavyo
havifai na havina utukufu.
Siku moja nilikuwa katika kusanyiko Fulani. Kwa bahati nzuri
tulikuwa ni vijana. Mimi nikiwa kama msemaji mkuu wa kusanyiko hilo
nilim-appoint mmoja miongoni mwa vijana wale kutuongoza katika pambio la
kuabudu. Kimuonekano niliamini anaweza kufanya hivyo, maana kama ni sauti anayo
tena nzuri tu,
Lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida huku vijana wote
tukiwa tumesimama na kufumba macho, ukimya wa zaidi ya sekunde 45 ulitawala
bila kumsikia Yule kijana niliemteua atupatie pambio ya kuabudu akianzisha
wimbo. Basi nikaamua kuimba mimi mwenyewe kuliko kuendelea kupoteza muda.
Baada ya mambo yote nikamuita Yule kijana na kumhoji mambo
kadhaa. Nikamuuliza kwanini hakuimba pambio? Nini kimemsibu? Je alikuwa ni
mgonjwa?
Kati ya maswali yote niliyomuuliza majibu yake yalikuwa ni
“HAKUNA”. Akaniambia kuwa yeye hawezi kabisa kuimba. Nikamuuliza unaweza
kufanya nini sasa. Je kuomba? Looh!! Akawa mkali kabisa akasema hapo ndio
hawezi kabisaaa..
Anyway. Nikawa nimejifunza mambo mengi sana. Kupitia kijana
huyu. Unajua kuwa Mungu amewaumba wanadamu wote sawa. Hakuna aliyempendelea
hata mmoja. Wala hakuna aliyeumbiwa kushindwa jambo lolote. Ila mwanadamu huyu
kwa kushindwa kulitambua kusudi lake au kujitambua mwenyewe akaamua
kujitengenezea mazingira ya kushindwa yeye peke yake.
Nilikuwa nasikiliza Audio moja ya kijana mmoja amabaye ni
mwandishi na mhamasishaji kwenye group la WhatsApp akawa anafafanua kuwa akili
ya mtu inapokea yale maneno anayoyazungunza na kuanza kuyafanyia kazi kwa
haraka sana. Yaani kwa mfano ukisema huwezi instant akili yako inachukua lile
neno siwezi na kuanza kulifanyia kazi, na huwa inaleta matokeo sahihi ambayo ni
SIWEZI.
Tuko hapa tulipo kutokana na mazingira ambayo tumejijengea.
Upo hapo ulipo au jinsi ulivyo kulingana na kile ulichoamua akili yako
ikifanyie kazi.
Kipindi Fulani Mungu alimtaka Gideoni akapambane na
Wamidian, Taifa lililowatesa Israel kwa kipindi kirefu sana. Gideoni akaanza
kuwaza how comes yeye ataenda kupambana na hao wamidiani. Akairuhusu akili yake
iwaone Wamidiani kuwa ni tatizo na hana namna ya kuweza kupambana nao. Akili
yake ikamletea majibu mazuri tu. KUmbuka akili yako ni kama kiwanda. Akili ya
Gideoni ikazalisha “bidhaa” ya woga. Ikamuelekeza akajifiche mapangoni.
Kumbuka kusudi la Mungu kwa Gideoni ni kuwa Mungu anamuona
yeye kuwa ni shujaa. Mungu anaamua kumfuata Gideon kule kule mapangoni na
kumtia moyo kuwa yeye ni shujaa na atawaokoa Israel dhidi ya Wamidian.
Kwa sababu akili ya Gideon ilishaathirika Mungu anaamua
kufanya kazi ya ziada kumtia moyo Gideon, Mungu anamwambia aende kwa ule uwezo
wake naye Mungu atajidhihirisha kwake. Lakini Gideon hakuridhika na majibu ya
Mungu akawa anataka uthibitisho wa kutosha kutoka kwake, naye Mungu hakusita
kufanya hivyo.
Baada ya moyo na akili ya Gideon kupona, ile sumu ya kujiona
hawezi imeshaondoka, Gideon anaandaa jeshi la watu elfu 32, ili kwenda
kupambana na jeshi la Wamidian lenye wanajeshi zaidi ya laki na thelathini. Kwa
akili za kawaida ni ngumu kuamini, yaani mwanajeshi mmoja wa kikosi cha Gideon
akapambane na wanajeshi wane wa Wamidian.
Kwa sababu Gideon ameshajivika hali ya ushujaa na kujiona
Kuwa ni mshindi Mungu anamwambia hao wanajeshi ni wengi, hivyo awapunguze,
Hatimaye wakapungua hadi kufikia idadi ya wanajeshi mia tatu tu (kumbuka hawa
wanajeshi mia tatu wanaenda kupambana na wanajeshi laki na thelathini)
Nataka nikuonyeshe kitu kimoja hapa, Ukibaki ukiwa
unajiangalia hali yako, unaangalia mazingira yako, unalinganisha na ukubwa wa
tatizo lako, akili yako itakuletea kushindwa tu. Gideon akaamua kwenda na kundi
lile la wanajeshi mia tatu lililogawanyika kwenye vikundi vitatu vya wanajeshi
mia moja kila kikundi. Kwa hesabu ya haraka ni sawa na mwanajeshi mmoja wa
Gideon anapambana na wanajeshi 440 wa Wamidian.
Nataka nikuambie kuwa huwezi kuamini Gideoni aliwapiga
Wamidian kama vile panzi. Gideon wakapata ushindi mkubwa sana. Mungu
akajithibitisha kwa viwango vya ajabu. Unajua ni kwanini? Gideon na jeshi lake
waliweka kando ile dhana ya kushindwa na kukikiri kile Mungu alichowaambia
Kwamba wao ni MASHUJAA (Ukipata muda soma Waamuzi sura ya sita nay a saba)
Watu Fulani kwenye Biblia wakaenda kuipeleleza nchi ya
Kanaani wakarudi na majibu ya kukatisha tama kabisa. Wakasema kuwa nchi ile ni
nzuri sana na ina kila kitu lakini watu wanaokaa katika nchi hiyo ni majitu,
yaani wanawala watu wakaao katika nchi hiyo. Wakajiona wao ni kama panzi tuu.
Lakini anatokea Joshua na Kalebu wanawatia watu moyo kuwa wanaweza kuimiliki
nchi ile.
Nataka nikukumbushe kuwa Mungu hayuko radhi na mtu
anaejidharau. Kitendo cha mwanadamu kujidhararau ni kumdharau Mungu. Tumeumbwa
kwa mfano na sura ya Mungu. Pumzi yetu tumepewa na Mungu hii inamaanisha kuwa
Mungu anaishi ndani yetu. Hivyo ukijidharau tu aisee jiandae kupigwa na Mungu
Mara nyingi tumekuwa tukisoma maamndiko kuwa hakuna jambo
ambalo linamshinda Mungu,. Usifikiri Mungu atashuka mwenyewe aje afanye jambo.
Kama akishuka yeye hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kuhimili. Badala yake
Mungu anamtumia mtu kufanya jambo. Alimtumia Gideon kuwapiga Wamidian.
Alimtumia Daudi kumuua Goliath. Usifikiri zilikuwa ni nguvu za Samson peke yake
kuweza kuwapiga watu laki na themanini kwa taya la punda. Hapana. Ni Mungu
alikuwa anafanya kazi kupitia Samson.
NAtamani uondoke kwenye hiyo hali ya SIWEZI. Nataka ujione
ukiwa shujaa kama Gideon. Unapojidharau ukajiona huwezi kumbuka kuwa hata watu
wengine wanaathirika sana. Taifa la Israel lilifadhaika sana kutokana na majibu
waliyoletewa na wale wazee 12 waliokwenda kuipeleleza nchi ya Kanaani
INUKA
Anza safari mpya leo. Anza kufanya kile ulichosema huwezi
kukifanya. Anza kufanya kile ulichoshindwa. Niliwahi kusema kuwa kile
unachoogopa kukifanya ndicho kilichobeba mafanikio yako. Kikwazo chako ndio
mafanikio yako. Huna haja ya kuishia njiani, Nikthibitishie utakapoanza mwanzo
mpya hakika utafikia ushindi mkubwa sana
Kama utabarikiwa na ujumbe huu ni ruksa kushea popote ili
unisaidie kumkumbusha mtu mmoja kuwa asijidharau, ana nafasi ya kufikia ushindi
mkubwa hivyo asiishie njiani.
Ahsante na ubarikiwe sana.
Ni mimi rafiki yako
Steven Mshiu
+255 768 882074
+255 655 882074
Smshiu42@gmail.com
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni