Alhamisi, 24 Agosti 2017

AMELIPA GHARAMA

AMENILIPIA GHARAMA.
Na Steven Mshiu.
Mara nyingi nimekuwa nikikutana na matukio mengi ambayo yananifanya niendelee kujifunza mambo mengi sana. Kumbuka kila unachokutana nacho una jambo la kujifunza.
Nakumbuka ilikuwa ni jumanne ya wiki iliyopita majira ya asubuhi sana na mapema. Kila mtu yuko busy tena kwa mwendo wa haraka kuhakikisha anawahi katika eneo lake la kujitafutia riziki.
Nikiwa ndani ya daladala, tulifika kituo fulani, tukakuta wanafunzi wengi ambao nao wanahitaji usafiri wa daladala ili waweze kufika shuleni.
Miongoni mwa wanafunzi alikuwepo mmoja ambaye nauli yake haikutosha. Akajaribu kumsihi kondakta amsaidie, lakini kondakta alikataa kata kata, Kondakta akagonga bodi ishara ya kumruhusu dereva aondoke.
Kwa kuwa nilikuwa nimekaa seat ya mbele kabisa, Nilimuona yule mwanafunzi akiwa katika hali ya majonzi makubwa sana, Akiwa kama amekosa msaada kwa wakati ule. Akiwaangalia wenzake waliokuwa na nauli ya kutosha wao wameruhusiwa kuingia ndani ya gari.
Wakati daladala ile imeanza safari nilijisikia kukosa amani kabisa. Nikasikia sauti ikiniambia unajisikiaje kumwona mwanafunzi yule ameachwa pale. Hivi akichelewa shule si ataenda kukumbana na adhabu?
Tukiwa mwendo wa kama mita kumi na tano hivi, nilimwambia dereva asimamishe gari halafu amwambie kondakta amruhusu yule mwanafunzi aingie ndani ya gari, MIMI NITAMLIPIA NAULI,
Ghafla dereva akasimamisha gari na kumwagiza kondakta tena kwa haraka amwite mwanafunzi yule. Ikabidi nitoe uso wangu kwa nje huku nikimuashiria yule mwanafunzi aje. Alikuja kwa furaha kubwa sana, hatimaye akaingia ndani ya gari. Yule kondakta ambaye alimzuia kuingia ndani ya gari ni kondakta huyo huyo aliyemwambia njoo, tena kaa hapa. Maana kuna mtu amekulipia nauli.
Yule mwnafunzi alifurahi sana, maana hata ile nauli yake hakuitoa, kwa sababu tayari nilishamlipia.
Alipofika sehemu anayotelemkia alinishukuru sana sana. "Kaka ahsante sana sana".
Mara nyingi nimekuwa nikikutana naye kwenye daladala au nje ya daladala na kila anaponiona hunisalimia kwa furaha sana, halafu anawageukia rafiki zake na kuwaambia "kuna siku sikuwa na nauli huyu kaka akanilipia aisee"
TUNAJIFUNZA NINI???
Wanadamu tulimkosea Mungu kwa kutenda dhambi. Dhambi ikatutenga na uso wa Mungu. Dhambi hii ikavunja mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu. Hivyo lilihitajika daraja litakalomuunganisha Mungu na mwanadamu. Gharama ya daraja hili ni lazima lijengwe au liunganishwe kwa damu
Au kwa kifupi ili mwanadamu awe karibu na Mungu ilitakiwa amwage damu yake maana yake ajiokoe kwa damu yake. Hii ilikuwa ni adhabu kubwa sana kwa wanadamu. Wapo waliojaribu kuchinja kondoo, mbuzi, njiwa, lakini damu zao zilionekana hazina thamani mbele za Mungu.
Mungu akaitisha kikao kikubwa sana mbinguni akiuliza ni nani atakaekuwa tayari kuja kuwaokoa wanadamu? Hakuna malaika yeyote, wala Kerubi wala Serafi aliyeweza kuinua sauti yake kuwa atakwenda kuwaokoa wanadamu.
Inawezekana walijiuliza maswali mengi sana, Hivi wataachaje enzi ya mbinguni ili waje kuwaokoa wanadamu?
Viumbe hawa walifahamu fika sifa za kiumbe anayetakiwa kuwaokoa wanadamu. Sifa ya kwanza ya mtu huyo ni lazima awe mwenye haki, pia awe mwenye upendo na sifa ya tatu ni lazima akubali kufa. Utasoma kitabu cha Ufunuo 5 kuzipata sifa hizi. Lilipofikia suala hili la kufa pakatokea ukimya mkuu sana kama anavyosema katika Ufunuo 5
Ndipo iliposikika sauti ya mtu mmoja aitwae YESU. Yeye alijitokeza kwa ujasiri mkubwa akiiacha enzi na utukufu wake wote uliopo mbinguni akasema "mimi nitakenda nimkomboe mwanadamu"
Kwa lugha nyepesi alikuwa tayari kulipa gharama ya makosa ya mwanadamu.
Akaja duniani akaishi kama mwanadamu kwa asilimia mia na kama Mungu kwa asilimia mia, Wanadamu hawa hawa wadhambi wakamsulubisha ili tu litimie neno.
Kwa kusulubiwa kwake akawa ameyakomboa maisha yetu kwa damu yake. Nikamkumbuka mwanafunzi huyu aliyepungukiwa nauli alivyokuwa katika sintofhamu kubwa nikafikiria maisha ya mwanadamu yangekuwa kwenye hatari gani endapo Yesu asingelipa gharama. Nikawaza huyu mwanafunzi endapo angechelewa shule angekutana na adhabu kali sana.
Vipi kwa huyu mwanadamu kama Yesu asingejitolea kulipa gharama wanadamu tungekutana na adhabu gani.?
Sisi sote ni abiria. Safari yetu inaelekea mbinguni. Nauli ni damu ya Yesu. Wale ambao hawajalipiwa nauli hii hawana furaha kabisa. Wapo kwenye wakati mgumu sana. Wanawaza kuchelewa kufika. Wanawaza adhabu itakayotokana na kuchelewa. Wanawaza mbona wenzao wana nauli ya kutosha?
Lakini wale ambao tuna nauli yaani tumeshaokolewa kwa damu ya Yesu kwetu ni furaha ya ajabu. Hatuna hofu ya kupata adhabu. Tuna uhakika wa safari.
Nikimkumbuka yule mwanafunzi niliyemlipia nauli kila akiniona jinsi anavyonichangamkia na kunisemea kwa rafiki zake huwa najisikia vizuri sana. Lakini huwa naenda mbele zaidi na mimi namkumbuka yule aliyelipa Gharama ya dhambi zangu. Yeye amenipa agizo moja tu katika Mathayo 28:18-19, Ameniagiza kuzitangaza habari zake kwa ulimwengu wooote, na kuwaambia wanadamu kuwa yeye ndiye aliyelipa gharama ya dhambi zangu.
Mpendwa rafiki,
Naomba nikuache na maswali machache ya kutafakari,
Ukiwa unasafiri halafu umepungukiwa nauli mara nyingi hukosa furaha kabisa. Hivi umeshajiuliza juu ya safari ya mbinguni? Una nauli ya kutosha?
Je kama ungetakiwa ujilipie peke yako gharama ya dhambi zako ungeweza? Ikiwa malaika mbinguni walikaa kimya wewe ungeweza?
Unairtumia vizuri nafasi uliyopewa kwa ajili ya kumtangaza huyo aliyekulipia gharama? Anasema atakayenionea haya mbele za wanadamu(Yesu) naye atamuonea haya Mbele za baba yake(MUNGU).
Mpendwa, hakuna gharama nyingine tunayotakiwa zaidi ya kufuata Yesu tu.
Kuna wimbo mmoja katika Tenzi huwa naupenda sana
Anasema "Nimekombolewa na Yesu, Aliyenirehemia, Kwa bei ya mauti yake nimekuwa mtoto wake"
Huna haja ya kuwa na hofu. Umeshalipiwa gharama. Tatizo hujijui kama umeshalipiwa gharama.
Ni kazi yako kutafuta kujua kama umelipiwa gharama.
Na Steven Mshi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...