Alhamisi, 24 Agosti 2017

WAACHE WAONGEE TU

WARUHUSU WASEME TU
Na Steven Mshiu
Baba mmoja alimaliza elimu yake ya juu miaka kadhaa iliyopita ni m-bobevu kwenye masuala ya uhasibu. Akiwa ametunukiwa cheti chake kutoka bodi ya wakaguzi wa hesabu za taifa inayojulikana kama CPA,
Mwanaume huyu alizunguka na vyeti vyake vyenye ufaulu mzuri akihangaika kutafuta kazi bila matokeo yoyote. Alizunguka kila wizara, aliingia kila shirika, lile la uma hata mashirika binafsi. Lakini hakufanikiwa kazi.
Mwanaume huyu alimtumainia Mungu kwa kiwango cha hali ya juu sana. Licha ya kutumia muda mwingi kutafuta kazi, hakukosa kutenga muda wake mwingi kumtumikia Mungu, mara nyingi alikuwa akikesha kanisani kumwomba Mungu, pamoja na kufanya huduma nyingine.
Ndugu zake na marafiki zake walipomuona akitumia muda mwingi kwa mambo ya kikanisa baada ya kukosa kazi, Walianza kuongea kama ilivyo desteuri ya wanadamu.
Wakadiriki kusema, "Ona sasa mnajiita walokole. Huyo Mungu wako yuko wapi mbona asikupe kazi sasa," "Tuliwaambia walokole wamechanganyikiwa, Sasa utakula huko kanisani"
Wengine wakasema, "Twende tukupeleke kwa mtaalam" akutengenezee dawa ya "kisimati" ili upate kazi" Wengi walikejeli sana na kumdharau sana.
Yule ndugu hakukubali maneno ya wale ndugu zake yauathiri moyo wake. Aliendelea kumtegemea Mungu tu. Siku zikaenda bila matokeo ya kupata kazi, miezi ikakata, miaka nayo ikazidi kusogea,
Siku moja akiwa kanisani alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akielekezwa kufika sehemu fulani kwa ajili ya usaili ili aweze kupata kazi. Anasema alimshukuru sana Mungu. Hatimaye akaenda kwenye usahili huo. Mungu si Athumani alifanikiwa kupata kazi na kuanza kupewa mshahara mzuri tu huku akipewa baadhi ya promosheni nyingi tu.
Ghafla yale maneno ya wale ndugu zake yakaanza kuyeyuka ghafla kama mshumaa. Wakakosa cha kuongea tena. Mbaya zaidi wakawa wakimkwepa. Hawakupata tena ujasiri wa kumwangalia usoni.
Wakati wa Bwana ukifika wale waliokucheka na kukubeza itakuwa ni zamu yao kuaibika. Akiwa kazini yule ndugu alipata nafasi ya kujiendeleza kimasomo kwa ngazi ya Masters, Baada ya kumaliza masomo yake moja kwa moja akapata kazi ofisi ya Waziri mkuu akiwa kama mkaguzi wa hesabu za mashirika yote yaliyo chini ya ofisi ya waziri mkuu.
Mungu akamuinua kwa mfumo huo. Yale maneno ya ndugu zake yakawa ni chanzo cha baraka zake. Akathibitisha uzuri wa wokovu wake. Akamthibitisha Mungu wa Walokole mbele ya wale ndugu zake. Kwa sasa wale ndugu zake wote wanamtegemea baba huyu kwa kila kitu.
Mpendwa rafiki,
Kuna watu watasema mbona umekaa miaka bila kuoa au kuolewa? Huoni kama umri unakwenda? Waruhusu waseme tu. Kuna mambo mazuri Mungu amekuandalia mbele.
Walisema mengi juu ya Hana. Hana aliwaruhusu waseme tu. Hatimaye leo tunasoma habari za Samwel.
Unamkumbuka Yusufu?
Walisema mengi sana juu yake. Ohh Mara yule Bwana ndoto anakuja kule. Wakamkejeli sana na kumdharau sana. Yusufu hakuwazuia kusema. Biblia yangu inaniambia wakati wa Yusufu kuinuliwa na Mungu, kisima hakikuweza kuzuia, mke wa Potifa hakuweza kuzuia, Hata gereza halikuweza kuzuia. Hatimaye akawa WAZIRI MKUU. Wale ndugu zake waliokuwa wakimsema wakashiba kwa mkono wa Yusufu.
Leo huna kazi. Waache waseme tu, Mungu amekuandalia ofisi yako. Utawaajiri hao hao wanaokusema.
Leo unatembea kwa miguu, wanasema mbona umeajiriwa miaka kumi huna hata Vitz? Waache waseme tu. Kuna siku watakuomba lifti au watakuona ukiwa kwenye BMW yako.
Leo si unaishi kwenye nyumba ya kupanga? Wanasema "tulijua hata kujenga hataweza kabisa" Waache waseme tu. Kuna siku hao hao watakuja kupanga katika nyumba zako. Ulifeli darasani wakasema tulijua tu. Wa kusoma uwe wewe?
waache waseme tu, kuna siku watakuona ukitukiwa cheti kutoka chuo kikuu.
Leo chakula kwako ni cha shida. Ukipata dagaa unamshukuru Mungu. Wanasema ona watoto wamevimba tumbo, tena wana kwashakoo. Ukiomba unga kwao watakutangaza mtaa mzima. Kuwa wewe ni omba omba. Nataka nikuambie kuwa wakati wa Mungu kukufanyia kicheko cha shibe u karibu. Utakula na kusaza. Hao hao wanaokuita omba omba watahitaji vyakula kutoka kwako. Utakula na kusaza mpendwa. Waruhusu waseme tuu.
Wale waliomsema Yesu kuwa si mwana wa Mungu eti anatoa pepo kwa Belzebuli, Leo ulimwengu mzima unamtambua Yesu kama MFALME. Mtu pekee aliyekufa na kuzikwa na akafufuka. Zaidi akapaa mbinguni.
Waache waseme tu. Maneno yao ni chanzo cha baraka zako. Maneno ni daraja la mafanikio yako. Muda si mraefu watashuhudia kinyume cha yale waliyokutabiria.
Mungu akupe uvumilivu wa kubakia kimya pindi wanaposema maneno yao juu yako.
Nakutia moyo mtu wa Mungu. Kamwe usiishie njiani.
Kumbuka wahenga walisema kuwa "KELELE ZA CHURA HAZIMZUII TEMBO KUNYWA MAJI" Maneno ya adui ni kelele za chura tu. Kamwe zisikutoe kwenye lengo.
Insipired by
Steven Mshiu
0655 882074

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...