Jumatano, 6 Septemba 2017

MAFANIKIO YASIKUTEKE MOYO

MAFANIKIO YA KIMWILI AU YA KIROHO YASIUTEKE MOYO WAKO.
Na Steven Mshiu.
Habarini za muda huu watu wa Mungu. Naamini sote tumeanza juma hili tukiwa na nguvu na afya tele. Kwa muda wa wiki moja hivi nimekuwa kimya ni kutokana na mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wangu.
Bado tuko pamoja.
Karibu tuendelee kubadilishana mawazo pamoja na kujifunza mambo kadha wa kadha ambayo yanaweza kuwa msaada wa maisha yetu na viroho vyetu.
Kwa nyakati za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa sana la watu wanaohubiri sana habari za mafanikio. Asilimia kubwa wamejikita kwenye mafanikio ya kimwili. Ukipita kwenye mitandao ya kijamii watu wako busy kuchangamkia fursa zinazojitokeza, huko whatapps ndio usiseme. Yapo magroup mengi sana yanayofundisha kwa wingi juu ya habari ya mafanikio ya kimwili.
Hata mimi napenda kuwa na mafanikio. Tena mafanikio makubwa sana. Na ninajitahidi kuyatafuta. Maana Biblia imeagiza baraka zinifuate. Mara nyingi nimekuwa nikisema kuwa mafanikio ya kimwili ni matokeo ya mafanikio ya kiroho. Yaani mtu anapoanza kuziogelea baraka za kimwili, ni kwamba baraka hizo zimeanzia rohoni.
Yohana anapomwandikia waraka mzee Gayo, anaanza kwa kumwambia Naomba ufanikiwe kama vile roho yako ifanikiwavyo. Ikiwa na maana kuwa baraka za Gayo zianzie rohoni kwanza.3 Yohana 1:1-2.
Kama utakuwa busy kukimbizana na kazi au na fursa ambazo unahisi huenda ukafanikiwa ukasahau kukimbizana kutafuta ustawi wa kiroho chako, utakuwa unapotea.
Kama uko busy kwenye kazi hadi unasahau muda wa kumtumikia Mungu imekula kwako. Kama moyo wako umetekwa na habari za pesa tu imekula kwako.
Mahali fulani Biblia ikasema kuwa palipo na hazina ya mtu ndipo ambapo na moyo wake ulipo. Yaani moyo unafuata pale ulipoweka juhudi kubwa. Kama umeweka juhudi kubwa kwenye kilimo, moyo wako utakuwa kwenye kilimo, kama umeweka juhudi kubwa katika kumtumikia Mungu, moyo wako wote utakuwa umejawa mambo ya kiMungu, maana hap ndipo hazina yako ilipo. Lakini anaendelea kusema kuwa jiwekeeni hazina yenu mbinguni, mahali ambapo hakuna kutu wala wezi wala chenye kuweza kuiharibu hazina yako.
Pale unapong'anga'ania kujiwekea hazina yako hapa duniani, Yaani 24/7 unatafuta pesa tu, huku ukitoa sababu kuwa hali ya maisha ni ngumu nikupongeze tu maana umechagua njia ya kupoteza. Usifikiri kuwa hutafanikiwa. La hasha. Utafanikiwa sana. Lakini jiandae kisaikolojia. Unaweza kujikuta kila unapopata pesa nondo wanakula. kutu inaharibu. wezi wanakuibia. Kwanini? Umeuruhusu moyo wako uelekee mafanikio ya kimwili.
Nikupe mfano huu ambao Yesu aliutoa.
Anasema kulikuwa na mtu mmoja alipambana na kilimo sana, Mungu akamsaidia akapata mavuno meeeengi sana, baada ya kuvuna akayaangalia yale mavuno, halafu akaziangalia ghala zake, akaanza kuwaza ndani ya moyo wake,
Kuwa atazivunja ghala za mwanzo, halafu atajenga nyingine kubwa zaidi zitakazotosha kuyahifadhi mazao yale.
Akaendelea kusemea moyoni mwake kuwa baada ya kujenga ghala hizo na kuyahifadhi mazao yake ataiambia nafsi yake kuwa sasa huu ni wakati wako wa kukaa ule, unywe na ufurahi maana nimepata mazao mengi. Wakati natafuta tafakari ya mfano huu nikajifunza kuwa pale mtu anapopata mafanikio kidogo tu wengi humsahau Mungu. Hufikiri wameyapata kwa nguvu zao tu. Hata huduma wengine huacha kabisa. HUbadili hata mfumo wa maisha. Mungu amekuinua kidogo tu hata kwenye huduma kiburi cha uzima huota. Huchukua hata ile nafasi ya utukufu wa Mungu.
Huyu mkulima alisahau mambo kadhaa, alisahau kuwa Mungu ndiye aliyenyesha mvua mimea ikaota, Akasahau kama Mungu ndiye aliyeyalinda mazao hayo na wadudu waharibifu. Inawezekana hata hakukumbuka kumtolea Mungu malimbuko. Yeye aliona ni wakati wake wa kukaa na kuanza kula. Ndivyo ilivyo kwa watu wengi siku za leo, mtu anapopata kidogo tu anajisahau kabisa.
Majibu ya Mungu kwa mtu huyu yalikuwa ni magumu sana. Mungu anamwita mtu huyo kuwa ni mpumbavu. Anamwambia Usiku huu wa leo wanaitaka roho yako. Je hayo yote uliyokuwa ukiyawaza yatakuwa ni ya nani? Unafahamu watakaokula hayo mazao yako? Jifunze kitu kimoja hapa. Mungu anamwambia kuwa WANAITAKA roho yako. Hapa sio Mungu anaitaka. Bali ni wengine wanaitaka. Soma Luka 12:16-20.
Haya ni madhara makubwa sana ya kukubali mafanikio yawe ya kimwili au ya kiroho yachukue nafasi ya ndani ya moyo wa mtu. Lusifa alitolewa kule mbinguni kwa sababu aliruhusu moyo wake uchukue utukufu wa Mungu. Kiburi cha uzima kikaota ndani ya nafsi yake, naye pia alijisemea nafsini mwake kuwa atakiinua kiti chake hadi mbinguni ili afanane na aliye juu. Kumbuka anjisemea moyoni mwake. Mungu akamshusha hadi chini kabisa. lile lengo lake halikuweza kutimia. Soma Isaya 14: 13-20.
Mpendwa rafiki, wakati Mungu anapokufanikisha hebu mtukuze na umkumbuke yeye. Kumbuka kuwa ni yeye amekupa tu kwa kupenda. Pia usisahau kumtumika Mungu. Moyo wako usitekwe na mambo ya ulimwengu huu, Tengeneza mafanikio mazuri ya moyo wako kwanza, Kumbuka maji hufuata mkondo. Baraka za kimwili nazo hufuata mkondo wa baraka za kiroho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...