
Na Steven Mshiu
Kwa wale ambao ni mara ya kwanza kufika mahali ambapo hukuwahi kufika hapo awali unaweza ukakubaliana na mimi.
Nakumbuka siku moja nikiwa nasafiri kutoka Moshi kwenda Mbeya, ilinibidi nipite Dar, nipumzike japo kwa siku moja ili niendelee na safari yangu.
Nikiwa Moshi watu waliwahi kuniambia historia ya Dar. Dar sio mahali pa mchezo. Pale watu huwa hawalali. Wizi, Utapeli, Ujambazi vimekithiri ndani ya jiji la DAR, Ni mji ambao umegubikwa na matukio mengi ya kutisha.
Wengine wakaniambia ukienda kama wewe ni mgeni unahitajika kuwa makini sana, Unaweza tapeliwa kila kitu.
Basi bhana, baada ya kufika zangu Ubungo na kwakuwa ilikuwa ni jioni sana, nikayakumbuka maneno ya wale watu, NIkakumbuka kuna rafiki yangu mmoja naye alishaibiwa simu na pesa hapo hapo Ubungo.
Kiukweli niliingiwa na hofu kubwa sana. Muda mwingi niliutumia kulinda mizigo yangu yaani begi langu, fedha nilizokuwa nazo pamoja na simu inayonisadia kupata mawasiliano. Kila niliyekutana naye pale DAR sikuweza kumwamini hata kidogo.
Chumba chenyewe nilichokitumia kama sehemu ya kupumzika sikupata hata lepe la usingizi. Muda wote nilikuwa macho nikiamini kuwa sehemu ile sio sahihi kwangu, maana mimi ni mpitaji pale tu. Hivyo endapo nitafanya ujinga na kutokuwa makini ninaweza kuibiwa jambo ambalo litasababisha safari yangu kuwa ngumu.
Kulipopambazuka tu nilifanya haraka haraka na kuelekea moja kwa moja kwenye basi nililokuwa nimekata tiketi kwa ajili ya safari yangu kuelekea Mbeya. Baada tu ya kuingia ndani ya lile basi la New Force, Aisee nilijihisi comfortable sana, Nikaamini kuwa sasa naweza kufika kule ninakoelekea.
NIlifika salama, na baada ya kufika pale nilipopataka, yaani sikuwa na wasiwasi wala ile hofu tena, Niliamini hakuna tena kitu ambacho kitaweza kuizuia safari yangu. Kwanza nimeshafika. Watu wa mahali pale ninawafahamu. hivyo sikuwa na hofu kabisa.
Hii ilikuwa ni safari yangu ya hapa duniani tu.
SASA NATAKA TUJIFUNZE NINI???
Sisi kama wakristo, hapa duniani ni wageni na wapitaji tu. Kuna mahali ambapo tunaelekea. Yesu mwenyewe alituthibitishia hilo na akatuambia kuwa anaenda kutuandalia makao huko mbinguni, na atarudi tena kutuchukua ili tukaishi kwenye hayo makao.
Jana nilikutana na andiko hili lililonifanya niikumbuke hii safari yangu, ni jinsi gani nilivyokuwa na hofu maana nilikuwa sijafika kule ninakoelekea.
1 Petro 1; 17, kwamba hapa duniani sio petu hivyo tuishi kwa hofu tukifahamu kuwa kuna siku tutaiacha.
Kuishi kwa hofu ni kutunza kile kitu kinachokusaidia kufika pale unapotaka kufika.
Ili mtu afike mbinguni jambo la kwanza ni lazima autunze UTAKATIFU wake. Ukisoma sura hii utaona Mungu anaagiza tuwe WATAKATIFU, maana yeye ni MTAKATIFU.
Hakuishia hapo, Katika Ebrania 12;14, anasema tafuteni kuwa na amani na watu wote, akaongezea jambo lingine pamoja na huo UTAKATIFU ambao pasipo huo hakuna atakaemuona MUNGU.
Kuna watu wanacheza na wokovu, wanona hii neema ya wokovu ni kitu cha mzaha tu, wamejisahau kuwa kama shetani halali anafanya kila njia kukunyang'anya wokovu wako. Ili aupate wokovu wako, anaanza kukutoa kwenye UTAKATIFU. Hapo amemaliza kazi yake.
Watu tuko busy kulinda mali zetu kama mimi nilivyokuwa ninalinda begi langu, simu na pesa ambazo zingenisaidia katika safari yangu ya kuelekea Mbeya, lakini tumejisahau kuulinda Utakatifu wetu utakaotusaidia kwenda mbinguni.
Watu tuko busy kupambana na wezi wanaotuibia mali zetu, wengine hatupati usingizi kama mimi, lakini tumemsahau shetani ambaye yeye halali usiku na mchana akituwinda.
Mimi nilifuata maelekezo ya wale walioniambia historia ya dar ilivyo, nikayaelewa vizuri sana. Kwetu sisi tunaolekea mbinguni maelekezo yetu yanapatikana ndani ya neno la Mungu.
Nilikuwa makini sana kuitunza simu yangu ili mradi tu nipate mawasiliano ya kule ninakoelekea. Ingetokea nikapoteza simu tu. safari yangu ingekuwa ngumu sana.
Mawasiliano yetu ya wale tunaoelekea mbinguni ni maombi. Usikubali shetani akuibie mawasiliano haya.
Biblia inaniambia kuwa vile vyenye maana hatuvipi maana, bali vile visivyo na maana ndivyo tunavyovipa maana.
Kuna mtu anaishi hapa duniani bila hofu ya Mungu. Anaishi kwa kufanya yasiyompendeza Mungu. Yesu anatutahadharisha. Atakuja kama mwivi. Wale ambao watakuwa wameutunza utakatifu wao watamlaki mawinguni,
Wale ambao watakuwa wameishi hapa duniani kama wamefika, wakalala usingizi, wakaruhusu shetani awaibie utakatifu wao, kwao itakuwa ni kilio na kusaga meno.
Ningeweza kukueleza mambo mengi ila jambo moja ninalokukumbusha ni kuwa usiku umeendelea sana, asubuhi inakaribia, Amka lkatika usingizi wako, kaa tayari, Ishi ukijua kuwa uko safarini. Ukilala kidogo tu, jiandae kuibiwa tiketi, na kila kitu.
Mungu akubariki sana
Steven Mshiu
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni