Jumanne, 26 Septemba 2017

UJUMBE MAHUSUSI KWA VIJANA WA LEO.

KWA VIJANA WENZANGU AMBAO BADO HATUJAFANIKIWA KUWA NA WATOTO.
Image may contain: one or more peopleNa Steven Mshiu.
Moshi,
Nataka nikushirikishe umuhimu na faida za kuwaombea watoto wako ingawa hujafahamu hata watatokea wapi.

Kwanza kabisa fahamu watoto ni urithi kutoka kwa Mungu. Zaburi 127:3, "Tazama, wana ndio urithi wa BWANA. Uzao wa tumbo ni thawabu.

Hakuna kitu cha thamani kama urithi. Urithi huwa unatunzwa kwa gharama yoyote ile. Huku kwetu uchagani tunaambiwa shamba la urithi huwa haliuzwi kabisa.
Mwana mpotevu alijikuta akila chakula walichokuwa wakila nguruwe kwa sababu alichezea urithi wake.

Maombi kwa watoto wetu ni kinga imara kwao.
Pili, Kila mtoto huzaliwa kwa kusudi kamili, Kusudi la Musa lilikuwa ni kuwatoa wana wa Israel kutoka utumwani Misri

Kusudi la Daudi lilikuwa kuja kuwa mfalme wa taifa la Israel, na kupitia kwake angezaliwa Yesu Kristo.

Kusudi la Yesu lilikuwa ni kuuokoa ulimwengu.
Siku zote shetani hupambana sana kuhakikisha analiua lile kusudi lililopo ndani ya watoto wetu.

Wakati Musa alipozaliwa ilitoka amri kuwa watoto wote wa kiume umri wa mwezi mmoja hadi miaka mitano wauwawe, vivyo hivyo kwa Yesu pia ilitoka amri hiyo.

Lengo lilikuwa ni moja tu, kuua lile kusudi lililopo ndani ya watoto wale.
Huwezi kufahamu mwanao atakuja kuwa nani. Huenda ni rais wa Tanzania miaka 50 ijayo. Shetani ataanza kumharibu kwa roho ya ulevi ili tu lile kusudi lisitimie. Una nafasi ya kuwaombea.

Tatu, Tunapowaombea tunawakabidhi kwa Bwana. Wewe kama wewe huwezi kuwalea watoto wako. Ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kuwalea watoto wetu. Katika Isaya 54:13, Biblia inasema "Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA. Amani ya watoto wako itakuwa nyingi"

Siku za leo kwa wazazi wengi imekuwa ni kilio kikubwa sana. Ukifuatilia utakuta tatizo ni watoto tu. Utamkuta mama ana kilio juu ya watoto wake, vivyo hivyo na wanaume pia. Na mara nyingi mtoto anapoharibika lawama nyingi huwa zinamuendea mama, Wanaume ni mara chache sana kujali juu ya hilo.

Kwenye Kitabu cha Mithali kuna sehemu anasema kuwa mwana mpumbavu huwa mzigo kwa mama yake, Lakini yule mwana mwerevu humfurahisha baba yake.
Mwana mpumbavu atatengenezwa na wazazi vivyo hivyo na mwana mwenye hekima atatengenezwa na wazazi. Wewe binti au kijana huna muda wa kuwaombea watoto wako halafu unataka kupata watoto werevu usifikiri ni kirahisi hivyo. Wahenga walisema kuwa ukiona vyaelea vimeundwa.

Wewe huna muda wa kuunda watoto wako, Unategemea mchungaji aje kukuombea siku ile unafunga ndoa pale kanisani, Kuwa Mungu abariki uzao wako, aisee utakuwa umechelewa sana.
Elewa kwamba hatima ya watoto wako ipo mikononi mwako. Wakati Mungu anatafuta ni nani atakaeweza kumzaa mtu mnadhiri wa Mungu Samsoni usifikiri aliwachagua Manoa na mke wake bila sababu. Watu hawa walikuwa wakimcha Mungu. Waliishi maisha ya maombi na imani kwa Mungu. Kuna mambo ambayo hutakiwi kufanya ili kutunza kusudi la wanao. Soma Waamuzi 13:4,

Mke wa Manoa anapewa maelekezo namna ya kutunza mimba ya mtoto atakaezaliwa, Kwanza anaambiwa asinywe kileo wala mvinyo wala divai, pia asile vitu visivyo najisi. Kwanini? Mtoto atakaezaliwa ni mnadhiri wa Mungu.

Kumbuka maelekezo yote haya anayopewa hajapata hata ujauzito, Lakini maandalizi yameanza mapema sana. Hakupata ujauzito halafu ndio apewe maelekezo. Ndipo sasa Manoa na mkewe wanaungana kuyashika na kuyatunza yale maelekezo ya Mungu juu ya mtoto atakaezaliwa ili kuitunza hatma ya maisha yake.

Malaika anamtokea Mariam na kumpa maelekezo kuwa atazaa mtoto kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, anapewa maelekezo kuwa huyo mtoto atakuwaje, lengo la kupewa maelekezo kabla ni ili ahakikishe analilinda lile kusudi lililopo ndani ya mtoto huyo.

Kwa hiyo basi mimi naamini kabla Mungu hajaruhusu mtoto kuzaliwa huanza kutoa maelekezo kuwa mtoto atakaezaliwa atakuwaje na kusudi lake ni lipi. maelekezo haya huyatoa kwa wazazi husika wa mtoto huyo. Maelekezo haya huyatoa kupitia maombi, Kama huna muda wa kumuomba Mungu na kumsikiliza itakuwa ngumu kupata maelekezo na utajikuta ukienda kwa akili zako na kujikuta uko nje ya mpango wa Mungu.

Kijana muombee mke wako. Yusuph alidhamiria kumuacha Mariam kwa siri kwa sababu alihisi ameshamsaliti. Lakini hakufahamu nini kusudi la Mungu. Watu hawa walikuwa ni wataua kama Biblia inavyotuambia. Kwa sababu bwana huyu alimfahamu Mungu, alipomuomba ndipo Mungu anamwambia kuwa asimwache maana kilicho ndani yake ni kitakatifu.

Elikana hakuacha kumuombea Hana, alimuombea na alimpenda sana. Ingawa Hana hakufanikiwa kuwa na mtoto, lakini alimuombea. Hatimaye Mungu akawapatia Samweli. Utaona baada ya Samweli kuzaliwa Elikana anafanya karamu kubwa sana. Tunakuja kkuona kazi kubwa sana aliyoifanya Samweli kwenye kitabu cha 1 samweli sura za mwanzo mwanzo.

Watabirie mema wanao. Sema wanao hawatavuta bangi, wanao hawakuwa machangudoa, wanao hawatakuwa watu wa kawaida. Wasemee watoto wako vile unavyotaka wawe. Unataka wawe wabunge watabirie kuwa wabunge, unataka wawe watumishi wa Mungu watabirie hivyo. Endapo hautawatabiria mema shetani atakuongoza kuwatabiria mabaya. Niliwahi sikia mama mmoja akimwita bintiye "njoo hapa mbwa wewe"

Halafu sidhani kama anafahamu tabia za mbwa. Huyo binti akikua kidogo akianza umalaya unaanza kusema mwanangu ameharibika. Unasahau kama ulimtabiria hivyo wewe mwenyewe.

Mimi huwa nawatabiria na kuwaombea wanangu mambo mema sana katika ulimwengu wa roho. Huwa nawatabiria kuwa watu wakuu wa Mungu. Watu wenye mamlaka. Watu wabarikiwa. huku nikijitahidi kuishi maisha ya utakatifu. Maisha ya kutokujichanganya. Yani nikifika kuomba juu ya jambo hili hapo sinaga utani kabisa.

Sulemani anaambiwa "Mjue sana Mungu wa baba yako(DAUDI) ndipo mambo mengi mema yatakapokujia. Kumbe wazazi kumjua Mungu ni chanzo cha baraka za watoto wetu.

Unaweza kujilaumu mbona wanao hawana mafanikio, kumbe mzazi huna muda na Mungu.
Jifunze kuomba toba na rehema kwa wanao. Ukisoma kitabu cha Ayubu sura ya kwanza, Mara nyingi Ayubu alitoa sadaka na kuwaombea rehema watoto wake, huenda labda wamefanya dhambi au la. Hili ni jambo lingine la Muhimu sana.

Natamani ningeendelea kuandika mengi lakini kwa haya machache naamini yanaweza kukusaidia sana
Jifunze kuwaombea watoto wako.
Inspired by Steven Mshiu
+255 655 882074

Maoni 1 :

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...