Na Steven Mshiu.
Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza katika makundi mbalimbali. Waweza kuwa watu wema au wabaya. Hali na vipato vyetu husababisha kutokea mgawanyiko na kutengeneza makundi. Leo nataka nikupe aina mbili za makundi haya.
KUNDI LA KWANZA: KUTOKA NDANI KWENDA NJE:
Hili ni kundi ambalo lipo pamoja na wewe. Nia ya kundi hili sio nzuri hata kidogo. Lipo na wewe pale unapokuwa katika raha tu. Watakula na kunywa vyako. Watatumia kila kilicho chako. Hii ni kwa sababu una kitu. Siku ukiishiwa Kundi hili hutoka upande wako, kwenda nje ya maisha yako.
Halikuthamini tena kwa sababu umefikwa na upungufu. Siku zote hubeba taarifa zako mbaya na kuzipeleka nje. Kama huna akili ya ziada huwezi kulitambua kundi hili hadi pale utakapofikwa na tatizo ndipo utakapofahamu uhalisia wa kundi hili.
KUNDI LA PILI:KUTOKA NJE KUJA NDANI
Hili ni kundi ambalo mara nyingi huwezi kulipa thamani yake. Halipo na wewe pale unapokuwa katika raha au furaha. Pale unapofikwa na matatizo ndipo linapojitokeza.
Kundi hili hutoka nje na kuja kwako.
Wakati lile kundi la kwanza likitoka kwako kwenda nje na hili la pili linalotoka nje kuja kwako lile kundi la kwanza hujaribu kulivunja moyo lile kundi la pili kwamba mambo yameharibika, Hivyo lisijisumbue kuja kwako. Lakini kwa sababu kundi hili la pili limebeba habari za matumaini huwa halivunjiki moyo.
Luka 8:49-56, Hapa tunaona makundi mawili, moja ni la Yesu lakini la pili ni la waombolezaji. Kundi la Yesu linaletewa habari ya msiba wa binti, Yesu anasema kuwa yule binti hajafa kwani amelala tu, Lakini lile kundi lingine linazipinga habari au taarifa za matumaini zilizotolewa na Yesu za urejesho wa uhai wa binti yule.
Kundi hili lipo pamoja na mfiwa likiomboleza na kulia lakini pale linaposikia habari za binti kurejeshewa uhai linaanza kucheka na kulibeza lile kundi lililotoa habari za matumaini.
Ndivyo ilivyo hata katika maisha yetu, Kuna kundi utaliona lipo pamoja na wewe lakini nia yake ni kukuona tu ukiwa katika hali mbaya. Halipendi kukuona ukiwa umefanikiwa. Halipendi kukuona ukipata kitu. Kupoteza kwako kwao ni furaha. Cha ajabu laweza kuwa ni kundi la wapendwa. Liepuke kundi hili.
Usifikiri kila mtu ni mwema kwako. Kuna ambao wanalia pamoja na wewe lakini mioyoni wao wanacheka. Kuna wanaokutia moyo lakini dhamira zao zinawashughudia
Mpendwa rafiki jitahidi ukae upande wa kundi hili la pili. Hili ni kundi lenye habari za mafanikio, Hubeba habari njema. Kundi hili hutokea na kuchukua nafasi inayoachwa na kundi la kwanza.
Mungu akusaidie kuyapambanua makundi ya watu wanaokuzunguka.
Steven Mshiu
0655 882074