Jumatano, 28 Juni 2017

Matokeo Mabovu ya Kutotii Sauti ya Mungu



MATOKEO MABOVU YA KUTOTII SAUTI YA MUNGU.
Na Steven MshiuMara nyingi Mungu huwa anasema na mtu au watu kabla hajafanya jambo fulani. Hii inategemea wewe umejiweka ktk nafasi gani ya kuweza kumsikia wakati akinena. Tumejikuta tukikwama kutokana na kutokuelewa kwetu kuwa Mungu anasema nasi kitu gani.
Wakati Eli alipotoka nje ya kusudi la Mungu, akafanya kama alivyoweza ndani ya hekalu, akaacha kuwalea watoto wake ktk maadili ya kiroho, wakalichezea hekalu la Mungu, wakafanya dhambi na uchafu wa kila namna kama walivyoweza bila kuulizwa chochote na baba yao Eli. Ndipo hasira ya Bwana ilipowaka juu ya Eli na wanawe. Mungu akaacha kuongea na Eli, kwa sababu hakuwa anayafuata maagizo yake tena. Na wakati huu neno la Mungu lilikuwa adimu sana ktk Israel. Kwa sababu bado Mungu alikuwa analipenda taifa la Israel, ndipo alipoanza mpamgo wa kumtafuta na kumwandaa Samwel kuichukua nafasi ya Eli. 1 samwel 2:35, Sikio la kufa siku zote huwa halisikii dawa. licha ya unabii wote huu bado Eli hakuweza kutubu wala kufanya juhudi za kulirejeza hekalu na taifa ktk hali ya utakatifu wa Mungu.
Mungu anaposema na Samwel juu ya dhambi ya Eli, anaanza kumwambia yatakayompata Eli pamoja na familia yake. 1 Samwel 3:11-14. Tayari Mungu alishamkataa moja kwa moja. Hapa anasema mambo makubwa na mabaya yatakayompata Eli na familia yake. Hakuna kitu kibaya kama kukataliwa na Mungu. Mungu anapokukataa kifo ni lazima kiwe nyuma yako. Na hatua ya kwanza unaanza kudhoofika kiroho. Kifo cha kimwili kama kinavyoonekana ktk 1 Sam 4:11,19 ni matokeo ya kifo cha kiroho.
Jambo lingine ni utukufu wa Mungu kuondoka. Mungu anakaa pale ambapo utakatifu wake unaenziwa. mahali ambapo anaposema watu wanaisikia sauti yake. Lakini wakati dhambi inapoingia tu basi utukufu wake huondoka. 1 Sam 5:1-2.
Yapo matokeo meeengi yanayotokana na kutoitii sauti ya Mungu. Kuna wakati hata wewe Mungu alisema nawe kuhusu kufanya jambo fulani, na unaweza ukawa ni shahidi wa kilichotokea kama ulitekeleza au la. Ni vizuri kutii na kufanya kile anachotuagiza Mungu ili aendelee kuwa pamoja nasi. Yeye anampenda mtu mti na mnyenyekevu anaeisikia sauti yake na kufuata maagizo yake.
Naibariki asubuhi yako na Mungu awe pamoja nawe kwa kila unalolifanya linalomletea utukufu.
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

MTAZAMO WA MUNGU NA MTAZAMO WA WANADAMU



MTAZAMO WA MUNGU NA MTAZAMO WA WANADAMU.
------------------------------------------------------------------
Na, Steven Mshiu
Nakusalimu kupitia jina la Kristo Yesu ambaye ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu. Ni matumaini yangu kuwa bado una uzima wa kutosha. Nina kila sababu ya kumtukuza Mungu kwa hilo.
Tumekuwa busy sana kwa mambo
mbalimbali, hadi kukosa muda wa kuweza kuweka
makala katika blog hii, ni kwa sababu tunaandaa mipango mizuri ya kuhakikisha blog hii inakuwa bora zaidi. Tumeshapata walimu kadhaa wa Neno la Mungu, na mapema tu utajifunza mengi, utahamasika kwa mengi kupitia blog hii. Lengo letu ni kuihubiri injili ya Kristo inayoleta wokovu kwa wanadamu. Ndicho kiini cha blog hii.
Leo napenda nikuletee makala hii fupi. Nafikiri
itakuhamasisha na kukupa morali wa kuamini kuwa kile Mungu alichokisema
juu ya maisha yako ni lazima kitimie haijalishi ni kwa muda gani. Unajua wanadamu tuna mtazamo, na Mungu pia ana mtazamo. Wewe waweza kuona hivi, Mungu akaona vile. Hivyo kuna tofauti kubwa sana kati ya mtazamo wa MUNGU na wa wanadamu.
Nikuletee kisa kimoja kwa leo ndani ya Biblia kinachomhusu mmoja wa watoto wa YAKOBO mwana wa ISAKA Ambaye ni uzao wa ahadi ya MUNGU kwa IBRAHIMU. Alikuwa ni mtoto wa 11 katika uzao wa Yakobo na kifungua mimba katika tumbo la Rahel, nduguye Leah. Kumbuka Isaka alikuwa na wake wawili (Lea na Rahel). Jina lake aliitwa YUSUFU.
Yusufu alikuwa ni mwana wa uzee kwa Yakobo, hivyo kwa kiswahili chepesi, baba yake alimdekeza sana, kama yeye(babaye)
alivyodekezwa na mamaye Rebeka.
 Mtazamo wa Yakobo kwa Yusufu alimtazama kama mpelelezi wa
nduguze, maana kipindi fulani alikuwa akienda kuwatazama nduguze makondeni
na kumletea babaye habari. Mwanzo 37:2-3.
Kwa ndugu zake, mtazamo wa ndugu zake Yusufu, walimtazama kama ni kiherehere, mmbea na mnafiki, hivyo wakamchukia Mwanzo 37:4 Haikuishia hapo.
Waishmaili wakamtazama Yusufu kwa mtazamo wa kibiashara. Hivyo wakamnunua Yusufu, Mwanzo 37:27-28 Kwa kuwa wa- Ishmaili walikuwa ni wafanyabiashara, na wameshapata dili jepesi hivyo wakamuuza tena kwa wafanyabiashara wengine wakubwa ambao ni wa-Midian. Na wa-Midian nao wakamuuza tena kwa POTIFA.
N.B: Kumbuka hii ni mitazamo ya wanadamu juu ya YUSUFU, Lakini Mungu alishamtazama kivingine, hivyo kote huku anakopitia mtazamo wa Mungu uko pale pale. Kwa Potifa. Potifa akamtazama YUSUFU kama mlinzi wa nyumba yake maana alikuwa mwaminifu sana. Mwanzo 39:4-5 Lakini bado mitizamo ya wanadamu haiishi. Mke wa POTIFA akamtazama kwa mtaza.mo wa tamaa. Yaani mtazamo wa kimapenzi, kwa kuwa alikuwa ni kijana mzuri, body yake iko safi. Hivyo akamtamani Mwanzo 39:6b-7. Na kwa sababu kijana huyu asieijua dhambi alikuwa akilinda utakatifu wake na mtazamo wa MUNGU kwake, hivyo hakutenda dhambi yoyote.
Katika kukimbia kwake akaangukia gerezani, mle gerezani wakamtazama kama ni mhalifu mkubwa sana. Maana alifungwa katika gereza la mfalme. Mwanzo 39:20, Mkuu wa gereza naye akamtazama Yusufu
kama msimamizi wa wenzake 39:21 Wakati wa MUNGU kudhihirisha jinsi anavyomtazama YUSUFU ulipofika, hakuna hata mmoja alieweza kuubadilisha.
Akiwa gerezani, ndipo mtazamo wa Mungu ulipoanzia safari ya kutimia. Miongoni mwa wafungwa wa mfalme, wawili wanaota ndoto, na Yusufu anawatafsiria. Kutokana na tafsiri ya Yusufu, yakawa ya kweli. Farao akaota ndoto ambayo ilimnyima usingizi na hapakupatikana mtu wa kuitafsiri.
Yule mfungwa mmoja akamkumbuka Yusufu alivyomtafsiria ile ndoto yake, akapeleka ombi kwa farao, kuwa kuna mfungwa/mhalifu mmoja wa kiebrania katika gereza la mfalme anaweza
kuitafsiri ndoto yako. Yusufu akaitwa mbele ya Farao na kuitafsiri ndoto. Hakika ikawa ni ya kweli.
Soma Mwanzo sura ya 41. Yusufu akapata kibali mbele ya Farao. Mwanzo 41:37-40. MUNGU
ALIMTAZAMA YUSUFU KAMA MTU WA TATU KTK TAIFA LA MISRI. Kwa lugha nyingine ni kwamba Mungu alimtazama
kama WAZIRI MKUU. (Mwanzo 41:41-42). Wakati wa kuinuliwa kwa Yusufu ukafika. Muda hautoshi kuendelea kuandika mengi, ila nina haya ya kuandika,
Wanadamu wanaweza
wakakutazama kama kahaba/malaya fulani hivi, lakini Mungu akakutazama kama mama/baba bora wa familia. Wanaweza wakakutazama kama
jambazi/mwizi fulani hivi lakini Mungu akakutazama kama mtumishi wake. Wanaweza wakakutazama mtumwa lakini Mungu akakutazama kama mfalme.
Wanaweza wakakutazama kama
asie na mwelekeo lakini Mungu akakutazama kama kiongozi mkubwa. Wanaweza wakakutazama kama masikini lakini Mungu akakutazama kama tajiri. Wanaweza wakakutazama kama
wewe ni wa kufa tu lakini Mungu akakutazama kama mtu wa kuishi. MTAZAMO WA MUNGU NI TOFAUTI KABISA NA MTAZAMO WA WANADAMU.
Walimtazama Daudi kama kijana mdogo, tena mchungaji wa kondoo tu, ambaye hayawani wanaweza kuila nyama yake. lakini Mungu alimtazama kama
shujaa na Mfalme wa Israel. Wanadamu wasikutishe na
mitizamo yao.
Nimalizie kwa kukumbusha mambo
machache.
*Ili mtazamo wa Mungu utimie ktk maisha yako ni lazima uuishi huo mtazamo. Mwanzo 39:9.
*Dhambi ni kikwazo kikubwa cha mtazamo wa Mungu kutimia. Amuzi 16:17-20
*Pale mtazamo wa Mungu unapotimia usilipe kisasi kwa wanadamu waliokuwa na mtazamo tofauti juu yako. Mwanzo 48:8-21
*Mtangaze Mungu wako kuwa yeye ndie mwezeshaji wa kila kitu.
Nikushukuru kwa kusoma ujumbe huu mfupi. Ni maombi yangu Mungu akakuinue na kutimiza kile alichoahidi katika maisha yako.
Ahsante.
Kama utakuwa na maoni au ushauri, unaweza kuwasiliana
na mwandishi wa makala hii,
Imeandikwa na Steven Mshiu,
0655-882074, 0768-882074
baruapepe smshiu42@gmail.com

UMEPAKWA MAFUTA KWA KAZI MAALUMU



UMEPAKWA MAFUTA KWA AJILI YA KAZI MAALUM. HUNA NAMNA YA KUYAKWEPA MAJARIBU. HEBU HAYO MAJARIBU YAWE NI DARASA KWAKO.
...............................................................................................................................
Na, Steven Mshiu.
Habari mpendwa rafiki,
Naamini Mungu anakutunza vyema,
Ninawiwa kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe ambaye kupitia makala ninazoziandika humu mtandaoni na kwenye blog zetu zimekuwa msaada kwako.
Kama unavyofahamu sote tu viungo katika mwili wa Kristo. Hivyo ni vyema kujengana na kutegemezana. Sote tunategemeana ili kuujenga mwili wa Kristo ili tuweze kuufikia ufalme wake.
Unapotenga muda wako kusoma makala hizi naamini kuna kitu Mungu anaenda kukutendea. Nikutaarifu tu kuwa kabla ya kuandika chochote humu huwa namuomba Mungu anijalie hekima Na ujumbe utakaokuwa ni wa muhimu kwa mhitaji.
Leo napenda nikuletee mambo machache tu. Hivi unafahamu kabla hujazaliwa tayari Mungu alishakupangia majukumu au kazi maalum utakayokuja kuifanya hapa duniani?
Katika Yeremia 1:4-7, tunaona ni jinsi gani ilivyomsumbua Yeremia kutambua kuwa yuko kwa ajili ya kazi maalum. Mungu anamwambia kabla hajazaliwa alikwisha kumchagua Kwa kazi maalum Kama inavyojieleza kwenye mistari inayofuata.
Hata wewe una kazi maalum. Hata mimi ninayo pia.
Baada ya Mungu kumkataa Sauli, sio kwamba utendaji wa Mungu ungekomea pale. Bado Mungu alikuwa ana mpango mzuri juu ya taifa la Israel. Kwa wale wasomaji wa Biblia watakumbuka kuwa Mfalme Sauli hakuwa ni chaguo la Mungu kwani alikuwa ni chaguo la wanadamu. Hivyo hakuona umuhimu wa kuyashika maagizo ya Mungu. Ndiyo sababu kubwa ya kukataliwa. Soma 1 Samwel 15:
Kwa kuwa Sauli hakuwa ni chaguo la Mungu, na kwamba tayari chaguo la wanadamu limekwama, Mungu anajipatia chaguo lake katika nyumba ya Yese mtu wa Bethlehem. Kijana mdogo, tena mtoto wa mwisho wa mzee Yese. Mungu anamtaka yeye awe Mfame. Matendo 13:22, Mungu anajisifia kwa kijana Daudi Kuwa yeye anaupendeza moyo wake na atafuata maagizo yote atakayoagizwa na Mungu.
Majukumu ambayo anatakiwa kuyakabili sio madogo. Tayari taifa la Israeli lilikuwa limeshambuliwa na maadui wengi. Wafilisti ndio walikuwa maadui wakubwa sana wa taifa hili teule la Mungu. Hivyo alitakiwa akabiliane nao na alete ushindi mkubwa. Sio Wafilisti tu. Mfalme Sauli naye angekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa Daudi. Kwani ile nafasi yake kama Mfalme ndio inachukuliwa na kijana Daudi badala ya mwanae Yonathan. Bado ndugu zake waliomtangulia wangeweza kuwa ni jaribu kwake. Yaani kwa nini yeye ni mdogo halafu anakiwa awe mfalme??
Kwa kuwa Mungu alikuwa ndiye mpangaji wa mambo yote alifahamu fika kuwa Daudi asingeweza kukabiliana na majaribu hayo yoooote bila kutiwa mafuta. Ndipo Mungu anamugiza Samwel akamtie mafuta kwa ajili ya kazi ambayo ipo mbele yake.
Nataka tujifunze jambo moja au mawili ya muhimu hapa. Chaguo la Mungu ni tofauti na la wanadamu kabisa. Nakukumbuka kipindi cha nyuma niliwahi andika makala moja inayosema "MTAZAMO WA MUNGU NI TOFAUTI NA MTAZAMO WA MWANADAMU". Kuwa mwanadamu yeye anaweza kuangalia Kwa nje tu na kutoa hukumu (judge) lakini Mungu huangalia moyo na ile hali ya ndani ya mtu.
Hivyo basi wakati amefika katika nyumba ya Yese, Yese aliweza kuwaita wanawe wote ili wapite mbele ya Samwel, Akamwacha Daudi ambaye kwa wakati huo alikuwa akichunga mifugo ya baba yake. Wao walimtazama kwa mtazamo wao kama wanadamu kwanza ni mdogo, halafu hana hata uzoefu wa vita. Kumbe ndie aliyekuwa chaguo la Mungu. Na kweli walipopita wote ya Samweli hakuonekana hata mmoja. Soma 1Samwel 16:1-13. Yese anaulizwa je wanao wote wako hapa??? Anasema ndio ILA kuna mmoja tena mdogo wao yuko machungani. Daudi alipokuja kweli akawa ndiye ambaye Mungu alikuwa amemchagua. Naye Samweli AKAMTIA MAFUTA
Mara nyingi Mungu huinua vile vinyonge ili kuviaibisha vyenye nguvu. Daudi huyu ndiye atakaekuja kumuangusha Goliath ambaye Mfalme Sauli na wengine wamemshindwa. Mungu alimwinua Yusuph alieonekana ni mwota ndoto tu, mtumwa na mfanyakazi wa kazi za ndani kuja kuwa WAZIRI MKUU, lakini ni baada ya kupitia majaribu mengi ambayo yalikuwa ni darasa kwake na kuweza kuitimiza ndoto yake.
Kupakwa mafuta ni ishara ya Roho Mtakatifu. Yesu akawaambia wanafunzi wake kuwa wasitoke pale walipokuwa wamekusanyika hadi watakapopokea nguvu. ambayo italetwa na Roho Mtakatifu. Ndipo watakapoweza kuwa mashahidi wake. Matendo 1:8, Huyo Roho ndiye atakaewawezesha maana kwa nguvu zao wasingeweza. Yapo majaribu meengi ambayo yalikuwa mbele zao na pasipo Roho Mtakatifu wasingeweza kuvumilia.
Yesu akiwa amefunga siku arobaini hali akijawa na Roho mwovu alipokuja na kunjaribu hakika aliweza aliweza kumshinda. Kwanini. Kwa sababu ROHO MTAKATIFU tayari alikuwa ndani yake. Mathayo 4:1-12, Stefano akiwa amejawa Roho, anapigwa kwa mawe hadi kufa huku akimshukuru Mungu, na kuwaombea rehema waliokuwa wakimpiga mawe. Asingeweza kuvumilia kama alikuwa hajapakwa mafuta ya Roho Mtakatifu. Yesu asingeweza kuvumilia kifo cha aibu. Kifo cha Msalaba kama Hakuwa na mafuta haya Ya Roho Mtakatifu
Daudi naye asingeweza kupambana na majaribu yaliyokuwa mbele yake dhidi ya Sauli Kama hakuwa na Mafuta haya. Asingeweza kupambana na Goliath aliyekuwa tishio kwa akina Yonadabu na Israel kwa ujumla kama hatakuwa na mafuta Haya yaani Roho Mtakatifu.
Hata sisi leo hatuwezi kukabiliana na majaribu ya dunia hii kama hatuna mafuta haya. Hatuwezi kufanya chochote pasi kuwa na uongozi wa Roho Mtakatifu. Sehemu fulani katika Biblia inasema kuwa "Wanaoongozwa na Roho ndio wana wa Mungu. Akasema tena katika Warumi 8:26, Kuwa sisi hatuwezi kuomba ipasavyo, ila Roho hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkika. Mambo mengi tu hatuwezi peke yetu pasipokuwa na msaada wa Roho Mtakatifu.
Hapo kazini kwako kuna watu wengi tu wanaimezea mate hiyo nafasi yako.
Kuna watu wanaimezea mate familia yako. Wanammezea mate mume wako. Wanammezea mate mke wako
Wanammezea mate huyo mchumba wako.
Wanaimezea mate biashara yako.
Wewe kama wewe huwezi kwa nguvu zako. Unamhitaji Roho Mtakatifu atakaekuwezesha katika yote. Sauli alijitahidi kutumia nguvu zake matokeo yake alishindwa vibaya.
Sote tunamhitaji Roho huyu. Maana tunaishi katika dunia ambayo ina kila aina ya majaribu.
Hayo ni kwa uchache tu. Ningeweza kuandika mengi lakini nataka tu uone umuhimu wa Roho Mtakatifu katika kila unachokifanya.
Binafsi kila siku huwa kila siku ninamuomba Mungu anijaalie na anipe Roho wake aniongoze juu ya kitu.
Na ukiona unapata hasara kwenye kila kitu unachokifanya tambua fika kabisa hujamhusisha Roho Mtakatifu
Mungu akubariki kwa ujumbe huu mfupi.
Kama utakuwa na maoni au chochote, usisite kuwasiliana nami.
Naamini pia yuko Roho Mtakatifu anaeweza kukufundisha mengi zaidi.
Ahsante.
Makala hii imeandikwa na Steven Mshiu,
Mwandishi, mwalimu na mshauri juu ya masuala ya kiroho na kumjua Mungu
0655-882074
smshiu42@gmail.com

UNA NAFASI YA KUSTAWI TENA



USIKATISHWE TAMAA. BADO UNA NAFASI YA KUSITAWI TENA
---------------------------------------------------------------------------------------------------
Na, Steven Mshiu.
Shalom Mtu mwema wa Mungu. Ni faraja yangu kukuona ukisonga mbele bila kuhofia chochote. Nakutia moyo kuwa japo usiku umeendelea Sana asubuhi yako itafika tu.
Nimekuwa nikikutana na baadhi ya watu wakiniambia kuwa wamechoshwa na maisha eti yamekuwa magumu.
Juzi nikamuuliza mtu mmoja kuwa Kama maisha yamekuwa magumu hebu nipe "suggestion" yako tufanyeje?
Kweli hakuwa na jibu la kunipa kabisa. Nikamwambia. Mpendwa, Ukibaki kulalamika tu ni kweli utaona maisha kuwa ni magumu.
Lakini ukitambua kuwa wewe ni mwana wa Mungu Hakika utakula mema ya nchi.
Nikamwambia kuwa maua ya kondeni, Mungu huyavisha na kuyapendezesha. Kiasi kwamba mazungu wanaweza kutumia gharama nyingi tu kuja kuyaangalia.
Nikamkumbusha tena kuhusu ndege wa angani. Wao hakuna sehemu yoyote ile wamelima shamba lakini Mungu huwalisha kila siku.
Sasa kwako wewe mwanadamu uliyeumbwa na Mungu sio zaidi ya hawa ndege au maua??
Tunaishi kwenye dunia ambamo kuna vitu vingi vinavyokatisha tamaa, Hali ya kimaisha kuwa ngumu inaweza kukukatisha tamaa. Unaweza kujikuta umesoma na una vyeti safi lakini una miaka zaidi ya nane bado hujapata kazi. Kukosa kazi kukakufanya ukate tamaa kabisa na kujutia elimu yako.
Unaweza kuwa na wazo la kufanya jambo fulani na umejiandaa vyema lakini kwa kuwa kuna ambaye alishindwa jambo hilo anaamua kukukatisha tamaa, na wewe ukakubali kukatishwa tamaa. Kusitawi kwako itakuwa ni ndoto.
Najua wote tuna kucha na nywele. Siku moja nikiwa saloon(chegani). Nikamwambia kinyozi kuwa nataka anitengeneze vizuuri, yaani aninyoe nywele zote ziwe za "size" moja tena ndogo kabisa, Naye akafanya hivyo. Baada ya kutoka hapo kila mtu akaniambia kuwa nimependeza sana, Nikasema ahsante.
Lakini kadri siku zilivyoendelea kwenda ndivyo zile nywele ziliendelea kukua na baada ya wiki tatu tu. Daaaah! zikawa kubwa. Binafsi sikutambua zimekua lini na sangapi.
Vivyo hivyo kwa kucha tena. Kila nikizikata lakini baada ya muda tu naziona tena zimeshakuwa kubwa. kila nikizikata. Zinaota.
Ndipo nilipojifunza jambo moja kubwa sana. Hata kama tunakatishwa tamaa kwa kiasi gani, Pale ambapo tu unapojitambua kuwa una kila haja ya kuendelea mbele, Hakika utasitawi tena. Na utafanyika baraka kwa wale wanaokukatisha tamaa.
Yule kinyozi alijitahidi kuninyoa vizuri sana, na nikamlipa. Lengo lake ni kuzikatisha tamaa nywele zangu ili zisiwepo. Lakini baada ya mwezi nikarudi tena pale akaninyoa tena na nikamlipa tena.
Mpendwa,
Pale unapokata tamaa kumbuka kuwa kuna watu wanaathirika. Kuna watu wanaikosa Huduma yako. Wewe hapo ulipo ni fursa tosha.
Ukijitambua tu kuwa wewe ni fursa hakika hutakata tamaa. Wala hutakubali kukatishwa tamaa
Marafiki zako kila siku wanaoa na kuolewa lakini wewe bado. Wao wana watoto lakini wewe bado. Unabaki ukisononeka na kuona kama Mungu hakuoni kabisa. Tena kwa wale ambao wako makanisani wanaamua kuacha wokovu kabisa. Kisa tu wenzao wameolewa na kuoa. Kwanini unakata tamaa mapema hivyo??
Kumbuka madhara ya kukata tamaa hujikuta unatenda dhambi. Sara alipoahidiwa mtoto akasubiri kwa muda mrefu bila mafanikio akajikata akitenda dhambi ya kumshawishi mumewe Ibrahimu azae na mfanyakazi wake Hajiri.
Usikatshwe tamaa mpendwa nakutia moyo kuwa bado una nafasi ya kustawi tena.
Bado una nafasi ya kuinuliwa tena
Yesu akasema kuwa liko tumaini kwa mti uliokatwa ukachipua tena.
Naamini hata kwako lipo tumaini la kuchipua tena
Uchumi wako unaenda kuchipua tena,
Hayo mahusiano ambayo huyaelewielewi yanaenda kuchipua na kustawi tena
Familia yako inaenda kuchipua tena
Hata huduma yako inaenda kuchipua tena.
Yote haya yatatokea endapo tu hutakubali kukatishwa tamaa.
Mungu akuinue tena
Usisite kuwasiliana nasi kwa kuhitaji ushauri juu ya masuala mbalimbali ya kiroho na kimwli pia
Ndimi rafiki yako
Steven Mshiu
0655-882074

Tumia Kipawa Mungu alichoweka Ndani Yako



TUMIA KIPAWA AMBACHO MUNGU AMEKIWEKA NDANI YA MOYO WAKO
 
Na Steven Mshiu .
Mungu anapoweka huduma au kipawa ndani ya moyo wako, yeye si mjinga. Anafahamu fika kuwa kuna mtu anaihitaji huduma yako au kile kitu ambacho Mungu ameweka ndani yako.
Nikiwa shuleni mwalimu wa Baiolojia aliwahi kunifundisha kitu kinachoitwa "use and disuse" Kwamba kadri kitu kinavyotumika sana ndivyo kinavyozidi kuwa imara, na endapo hakitatumika basi hupoteza ubora wake au kupotea kabisa.
Wakati nikienda shamba lile jembe ambalo nalitumia mara kwa mara linakuwa jepesi mkononi mwangu. Ni kwa sababu nimeshalizoea.
Mwanadamu anapozaliwa tayari Mungu alishaweka kazi maalum ndani yake. Yeremia anaambiwa kuwa atakuwa nabii na atakwenda kila mahali ambapo Mungu atamtuma. Yeremia anaanza kujitetea kuwa yeye bado ni mdogo.
Mungu anamwambia kuwa alimchagua tangu akiwa tumboni mwa mama yake kwa ajili ya kuharibu, kubomoa na kung'oa ili kupanda na kujenga.
Kwa hiyo hata wewe kuna kazi ambayo Mungu anataka uifanye. Mungu anampenda yule anayefanya kazi yake kwa kumtii yeye, kuyafuata maagizo yake ikiwa ni pamoja na kumtii yeye.
Unapofanya kazi ya Mungu kwa moyo na kwa kumtii yeye, yeye hufurahishwa na wewe.
Sauli mfal,e wa Israel, licha ya kuchaguliwa na Mungu kuwa mwamuzi wa Taifa la Israel baada ya Samwel, alijiona kuwa yeye hana muda wa kuyasikiliza maagizo ya Mungu kwani anaweza kufanya lolote kwa kuwa yeye ni Mfalme. Hata alipopewa maagizo ya kuwaua Amaleki wote yeye alimwacha Agagi Mfalme wa Amaleki angali hai.
Mungu akajuta kwanini alimchagua Sauli kuwa mfalme. Ni kwa sababu hakutaka kufuata maagizo ya Mungu katika kuitimiza kazi aliyoagizwa
Mwishowe Mungu alimkataa kabisa na kuuhamisha ule ufalme kutoka kwa Sauli na Kwenda kwa Daudi. Soma 1 Samweli 15
Yapo madhara yanayoweza kukupata endapo hutasimama katika nafasi Mungu aliyokuweka. Au pale ambapo utaacha kulifuata agizo la Mungu
Kwanza Mungu atajuta kwa ajili yako
Utaondolewa kwenye ile nafasi yako, na nafasi yako itapewa mtu mwingine
Mungu atakukataa kabisa
Sasa basi fanya mambo haya ili uendelee kubaki katika nafasi ambayo Mungu amekuweka
Mtii na kutekeleza kile Mungu anachokuagiza
Kuwa mnyenyekevu na mtu wa kujishusha
Usijikweze
Kuwa mtu wa kukubali kushauriwa(flexible)
Kuwa mvumilivu na mwenye subira
Kaa kwenye kusudi lako. Tekeleza kile unachotakiwa kukifanya
Tambua kuwa kuna watu wanaokutegemea ikiwa ni kujifunza kutoka kwako na mengine mengi.
Epuka kuwa m-binafsi. Kufanya mambo kwa kutegemea matakwa yako, kwa tamaa zako.
Kuwa mtu wa kujihukumu mwenyewe. yani mtu wa toba pale unapokuwa umekosea.
Ukifanya yote haya Mungu atajisifia kwa ajili yako kama alivyojisifia kwa Daudi kwamba Daudi ni mtu anaeupendeza moyo wa Mungu na anafuata kile anachomuagiza
Ahsante
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...