Jumanne, 26 Septemba 2017

HATUA TANO ZAIDI MBELE.

UKIRUDI NYUMA HATUA MOJA SONGA MBELE HATUA TANO.
Image may contain: 3 people, people smiling, people standing Na Steven Mshiu.
Habarini za muda huu watu wa Mungu.
Naamini umeamka u bukheri wa afya.
Tumshukuru Mungu kwa pumzi aliyotujalia kila leo,

Mara nyingi tumekuwa tukikutana na mambo au changamoto ambazo huturudisha nyuma na kutufanya kujenga dhana ya kushindwa.

Leo nataka nikutie moyo kuwa endapo utarudi nyuma hatua moja bado una nafasi ya kusonga mbele hatua tano.

Jana nilikuwa nasafiri kutoka eneo fulani hadi eneo jingine. safari iliyochukua muda wa kama masaa mawili hivi. Kwa bahati nzuri nilikaa karibu kabisa na dereva. Muda mwingi niliutumia kumuangalia yule dereva jinsi anavyoendesha gari.

Ili gari iweze kwenda alikuwa akitumia "gia"
Ikabidi nitumie nguvu kubwa zaidi kuangalia kile "kirungu" au gia ni namna gani kinavyotumika.
Nilipoangalia kwa umakini sana pale juu ya kile kirungu niliona namba 1,2,3,4,5 na R.
Mwanzo wa safari yetu wakati tunaondoka pale stendi, Kile kirungu alikielekeza kwenye herufi R, nikaona gari ikirudi nyuma maana kuna gari nyingine iliyokuwa mbele yetu. Baada ya kurudi nyuma kidogo na palipopatikana upenyo wa ile gari yetu kupita, dereva alielekeza kile kirungu kwenye namba 1 hatimaye nikaona gari ikienda mbele.

Kadri tulivyoendelea mbele dereva alikuwa akihamisha kile kirungu kutoka namba hadi namba. Yaani alitoka 1 hadi 2 akaendelea 3,4 hadi 5. Sikumwona akitumia tena au akilekeza kile kirungu kwenye herufi R.

Hata wakati alipotaka kupakia barabarani sikumwona akirudisha kile kirungu kwenye herufi R, mara nyingi alikuwa akikiacha kikiwa katikati, na alipomaliza kupakia abiria alikielekeza kwenye namba 1 gari ikasonga mbele kwa mbele.

Baada ya kutumia muda mrefu saaana kumuangalia yule dereva, huku nikizalisha maswali mengi kichwani, nilishindwa kuvumilia ikabidi nimuulize yule dereva. Mbona huelekezi hicho kirungu kwenye hiyo herufi R? Mbona umekitumia mara moja tuu.

Ndipo akaniambia kuwa Hiyo herufi R ni gia ya kurudi nyuma, mara nyingi tunapoendesha gari gia hii huwa tunaitumia mara chache sana, haswa kwa biashara zetu hizi za kubeba abiria. Abiria wao wanaenda mbele, sasa tukiweka hii gia ya kurudi nyuma hawatafika na sisi hatutapata pesa, maana tutakuwa tunarudi nyuma tu, Wakati ananiambia maneno haya alikuwa akihama kutoka namba 3 hadi 4, huku gari ikizidi kuongeza mwendo tofauti na ule wa wakati ameweka namba1.

Nikamwambia ahsante kwa majibu yako. Lakini mbona ukihama kutoka namba 1 au 2 unapohamia 3 au 4 mwendo unaongezeka? Akaniambia siku zote unapoanza safari huwa ngumu sana au nzito lakini kadri unavyosonga mbele safari huwa nyepesi, hivyo ninavyobadili gia kutoka 1,2 kwenda 3 au 4 gari huwa nyepesi sana hivyo mwendo nao unaongezeka.

Kila alipozidi kubadili gia ndivyo ambavyo mwendo uliongezeka.
Nikamsikia "konda" akigonga bodi akiashiria kuwa ameona abiria anaetaka kuingia kwenye gari. Wakati huo dereva alikuwa kwenye gia namba 5, wakati anasimamisha gari alianza kurudi gia za nyuma yaani 4, 3, 2 hadi 1. Nilichoshangaa tena wakati anabadili gia hizi kurudi nyuma gari nayo ilikuwa ikipunguza mwendo.

Nilijifunza mambo mengi sana kuhusu mfumo huu unaotumiwa na gari hili.

Katika maisha yetu ni vyema tukajitengenezea mfumo kama wa gari. Unapoianza safari mara nyingi hurudi nyuma kuangalia mwanzo wako, Ni namna gani mbele yako kulikuwa na vikwazo vingi vinavyokuzuia wewe usisonge mbele, rudi nyuma mara moja tu, utengeneze mwanya wa wewe kusonga mbele. Yule dereva alirudi nyuma mara moja tu ili kukwepa ile gari iliyokuwa mbele yake.

Ni lazima ukubali kurudi nyuma mara moja tu, yule dereva angeng'ang'ania kuweka gia za mbele angeweza kusababisha ajali na safari yake ingekwama.

Unapoanza kusonga mbele, mara nyingi mwanzo huwa mzito. lakini kadri unavyozidi kubadili gia za kusonga mbele safari huwa nyepesi yale mazito uliyokuwa ukiyaona yanakuwa mepesi. Kadri unavyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo unazidi kutengeneza fursa nyingi zinazokuletea faida.
UKIRUDI NYUMA MARA MOJA SONGA MBELE MARA TANO ZAIDI

Usikubali kurudi nyuma mara nyingi. Ukiwa jeshini yule anayeonekana kurudi nyuma huwa anapigwa risasi. Kwenye daladala dereva akianza kuweka gia ya kurudi nyuma tu, hakuna abiria atakaepanda gari hiyo. Matokeo yake watakosa pesa.

Ukikubali au ukiruhusu kuwa mtu wa kurudi nyuma tu, jiandae kupigwa risasi, jiandae kukosa abiria, jiandae kukosa fursa.

Ukianza jambo jitahidi lisonge mbele na wala sio kurudi nyuma.
Insipired by Steven Mshiu.
+255 655 882074



UJUMBE MAHUSUSI KWA VIJANA WA LEO.

KWA VIJANA WENZANGU AMBAO BADO HATUJAFANIKIWA KUWA NA WATOTO.
Image may contain: one or more peopleNa Steven Mshiu.
Moshi,
Nataka nikushirikishe umuhimu na faida za kuwaombea watoto wako ingawa hujafahamu hata watatokea wapi.

Kwanza kabisa fahamu watoto ni urithi kutoka kwa Mungu. Zaburi 127:3, "Tazama, wana ndio urithi wa BWANA. Uzao wa tumbo ni thawabu.

Hakuna kitu cha thamani kama urithi. Urithi huwa unatunzwa kwa gharama yoyote ile. Huku kwetu uchagani tunaambiwa shamba la urithi huwa haliuzwi kabisa.
Mwana mpotevu alijikuta akila chakula walichokuwa wakila nguruwe kwa sababu alichezea urithi wake.

Maombi kwa watoto wetu ni kinga imara kwao.
Pili, Kila mtoto huzaliwa kwa kusudi kamili, Kusudi la Musa lilikuwa ni kuwatoa wana wa Israel kutoka utumwani Misri

Kusudi la Daudi lilikuwa kuja kuwa mfalme wa taifa la Israel, na kupitia kwake angezaliwa Yesu Kristo.

Kusudi la Yesu lilikuwa ni kuuokoa ulimwengu.
Siku zote shetani hupambana sana kuhakikisha analiua lile kusudi lililopo ndani ya watoto wetu.

Wakati Musa alipozaliwa ilitoka amri kuwa watoto wote wa kiume umri wa mwezi mmoja hadi miaka mitano wauwawe, vivyo hivyo kwa Yesu pia ilitoka amri hiyo.

Lengo lilikuwa ni moja tu, kuua lile kusudi lililopo ndani ya watoto wale.
Huwezi kufahamu mwanao atakuja kuwa nani. Huenda ni rais wa Tanzania miaka 50 ijayo. Shetani ataanza kumharibu kwa roho ya ulevi ili tu lile kusudi lisitimie. Una nafasi ya kuwaombea.

Tatu, Tunapowaombea tunawakabidhi kwa Bwana. Wewe kama wewe huwezi kuwalea watoto wako. Ni Mungu peke yake ndiye anayeweza kuwalea watoto wetu. Katika Isaya 54:13, Biblia inasema "Na watoto wako wote watafundishwa na BWANA. Amani ya watoto wako itakuwa nyingi"

Siku za leo kwa wazazi wengi imekuwa ni kilio kikubwa sana. Ukifuatilia utakuta tatizo ni watoto tu. Utamkuta mama ana kilio juu ya watoto wake, vivyo hivyo na wanaume pia. Na mara nyingi mtoto anapoharibika lawama nyingi huwa zinamuendea mama, Wanaume ni mara chache sana kujali juu ya hilo.

Kwenye Kitabu cha Mithali kuna sehemu anasema kuwa mwana mpumbavu huwa mzigo kwa mama yake, Lakini yule mwana mwerevu humfurahisha baba yake.
Mwana mpumbavu atatengenezwa na wazazi vivyo hivyo na mwana mwenye hekima atatengenezwa na wazazi. Wewe binti au kijana huna muda wa kuwaombea watoto wako halafu unataka kupata watoto werevu usifikiri ni kirahisi hivyo. Wahenga walisema kuwa ukiona vyaelea vimeundwa.

Wewe huna muda wa kuunda watoto wako, Unategemea mchungaji aje kukuombea siku ile unafunga ndoa pale kanisani, Kuwa Mungu abariki uzao wako, aisee utakuwa umechelewa sana.
Elewa kwamba hatima ya watoto wako ipo mikononi mwako. Wakati Mungu anatafuta ni nani atakaeweza kumzaa mtu mnadhiri wa Mungu Samsoni usifikiri aliwachagua Manoa na mke wake bila sababu. Watu hawa walikuwa wakimcha Mungu. Waliishi maisha ya maombi na imani kwa Mungu. Kuna mambo ambayo hutakiwi kufanya ili kutunza kusudi la wanao. Soma Waamuzi 13:4,

Mke wa Manoa anapewa maelekezo namna ya kutunza mimba ya mtoto atakaezaliwa, Kwanza anaambiwa asinywe kileo wala mvinyo wala divai, pia asile vitu visivyo najisi. Kwanini? Mtoto atakaezaliwa ni mnadhiri wa Mungu.

Kumbuka maelekezo yote haya anayopewa hajapata hata ujauzito, Lakini maandalizi yameanza mapema sana. Hakupata ujauzito halafu ndio apewe maelekezo. Ndipo sasa Manoa na mkewe wanaungana kuyashika na kuyatunza yale maelekezo ya Mungu juu ya mtoto atakaezaliwa ili kuitunza hatma ya maisha yake.

Malaika anamtokea Mariam na kumpa maelekezo kuwa atazaa mtoto kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, anapewa maelekezo kuwa huyo mtoto atakuwaje, lengo la kupewa maelekezo kabla ni ili ahakikishe analilinda lile kusudi lililopo ndani ya mtoto huyo.

Kwa hiyo basi mimi naamini kabla Mungu hajaruhusu mtoto kuzaliwa huanza kutoa maelekezo kuwa mtoto atakaezaliwa atakuwaje na kusudi lake ni lipi. maelekezo haya huyatoa kwa wazazi husika wa mtoto huyo. Maelekezo haya huyatoa kupitia maombi, Kama huna muda wa kumuomba Mungu na kumsikiliza itakuwa ngumu kupata maelekezo na utajikuta ukienda kwa akili zako na kujikuta uko nje ya mpango wa Mungu.

Kijana muombee mke wako. Yusuph alidhamiria kumuacha Mariam kwa siri kwa sababu alihisi ameshamsaliti. Lakini hakufahamu nini kusudi la Mungu. Watu hawa walikuwa ni wataua kama Biblia inavyotuambia. Kwa sababu bwana huyu alimfahamu Mungu, alipomuomba ndipo Mungu anamwambia kuwa asimwache maana kilicho ndani yake ni kitakatifu.

Elikana hakuacha kumuombea Hana, alimuombea na alimpenda sana. Ingawa Hana hakufanikiwa kuwa na mtoto, lakini alimuombea. Hatimaye Mungu akawapatia Samweli. Utaona baada ya Samweli kuzaliwa Elikana anafanya karamu kubwa sana. Tunakuja kkuona kazi kubwa sana aliyoifanya Samweli kwenye kitabu cha 1 samweli sura za mwanzo mwanzo.

Watabirie mema wanao. Sema wanao hawatavuta bangi, wanao hawakuwa machangudoa, wanao hawatakuwa watu wa kawaida. Wasemee watoto wako vile unavyotaka wawe. Unataka wawe wabunge watabirie kuwa wabunge, unataka wawe watumishi wa Mungu watabirie hivyo. Endapo hautawatabiria mema shetani atakuongoza kuwatabiria mabaya. Niliwahi sikia mama mmoja akimwita bintiye "njoo hapa mbwa wewe"

Halafu sidhani kama anafahamu tabia za mbwa. Huyo binti akikua kidogo akianza umalaya unaanza kusema mwanangu ameharibika. Unasahau kama ulimtabiria hivyo wewe mwenyewe.

Mimi huwa nawatabiria na kuwaombea wanangu mambo mema sana katika ulimwengu wa roho. Huwa nawatabiria kuwa watu wakuu wa Mungu. Watu wenye mamlaka. Watu wabarikiwa. huku nikijitahidi kuishi maisha ya utakatifu. Maisha ya kutokujichanganya. Yani nikifika kuomba juu ya jambo hili hapo sinaga utani kabisa.

Sulemani anaambiwa "Mjue sana Mungu wa baba yako(DAUDI) ndipo mambo mengi mema yatakapokujia. Kumbe wazazi kumjua Mungu ni chanzo cha baraka za watoto wetu.

Unaweza kujilaumu mbona wanao hawana mafanikio, kumbe mzazi huna muda na Mungu.
Jifunze kuomba toba na rehema kwa wanao. Ukisoma kitabu cha Ayubu sura ya kwanza, Mara nyingi Ayubu alitoa sadaka na kuwaombea rehema watoto wake, huenda labda wamefanya dhambi au la. Hili ni jambo lingine la Muhimu sana.

Natamani ningeendelea kuandika mengi lakini kwa haya machache naamini yanaweza kukusaidia sana
Jifunze kuwaombea watoto wako.
Inspired by Steven Mshiu
+255 655 882074

Jumatatu, 18 Septemba 2017

TUNZA UTAKATIFU WAKO

MARA YA KWANZA KWENDA DAR.
Na Steven Mshiu
Kwa wale ambao ni mara ya kwanza kufika mahali ambapo hukuwahi kufika hapo awali unaweza ukakubaliana na mimi.
Nakumbuka siku moja nikiwa nasafiri kutoka Moshi kwenda Mbeya, ilinibidi nipite Dar, nipumzike japo kwa siku moja ili niendelee na safari yangu.
Nikiwa Moshi watu waliwahi kuniambia historia ya Dar. Dar sio mahali pa mchezo. Pale watu huwa hawalali. Wizi, Utapeli, Ujambazi vimekithiri ndani ya jiji la DAR, Ni mji ambao umegubikwa na matukio mengi ya kutisha.
Wengine wakaniambia ukienda kama wewe ni mgeni unahitajika kuwa makini sana, Unaweza tapeliwa kila kitu.
Basi bhana, baada ya kufika zangu Ubungo na kwakuwa ilikuwa ni jioni sana, nikayakumbuka maneno ya wale watu, NIkakumbuka kuna rafiki yangu mmoja naye alishaibiwa simu na pesa hapo hapo Ubungo.
Kiukweli niliingiwa na hofu kubwa sana. Muda mwingi niliutumia kulinda mizigo yangu yaani begi langu, fedha nilizokuwa nazo pamoja na simu inayonisadia kupata mawasiliano. Kila niliyekutana naye pale DAR sikuweza kumwamini hata kidogo.
Chumba chenyewe nilichokitumia kama sehemu ya kupumzika sikupata hata lepe la usingizi. Muda wote nilikuwa macho nikiamini kuwa sehemu ile sio sahihi kwangu, maana mimi ni mpitaji pale tu. Hivyo endapo nitafanya ujinga na kutokuwa makini ninaweza kuibiwa jambo ambalo litasababisha safari yangu kuwa ngumu.
Kulipopambazuka tu nilifanya haraka haraka na kuelekea moja kwa moja kwenye basi nililokuwa nimekata tiketi kwa ajili ya safari yangu kuelekea Mbeya. Baada tu ya kuingia ndani ya lile basi la New Force, Aisee nilijihisi comfortable sana, Nikaamini kuwa sasa naweza kufika kule ninakoelekea.
NIlifika salama, na baada ya kufika pale nilipopataka, yaani sikuwa na wasiwasi wala ile hofu tena, Niliamini hakuna tena kitu ambacho kitaweza kuizuia safari yangu. Kwanza nimeshafika. Watu wa mahali pale ninawafahamu. hivyo sikuwa na hofu kabisa.
Hii ilikuwa ni safari yangu ya hapa duniani tu.
SASA NATAKA TUJIFUNZE NINI???
Sisi kama wakristo, hapa duniani ni wageni na wapitaji tu. Kuna mahali ambapo tunaelekea. Yesu mwenyewe alituthibitishia hilo na akatuambia kuwa anaenda kutuandalia makao huko mbinguni, na atarudi tena kutuchukua ili tukaishi kwenye hayo makao.
Jana nilikutana na andiko hili lililonifanya niikumbuke hii safari yangu, ni jinsi gani nilivyokuwa na hofu maana nilikuwa sijafika kule ninakoelekea.
1 Petro 1; 17, kwamba hapa duniani sio petu hivyo tuishi kwa hofu tukifahamu kuwa kuna siku tutaiacha.
Kuishi kwa hofu ni kutunza kile kitu kinachokusaidia kufika pale unapotaka kufika.
Ili mtu afike mbinguni jambo la kwanza ni lazima autunze UTAKATIFU wake. Ukisoma sura hii utaona Mungu anaagiza tuwe WATAKATIFU, maana yeye ni MTAKATIFU.
Hakuishia hapo, Katika Ebrania 12;14, anasema tafuteni kuwa na amani na watu wote, akaongezea jambo lingine pamoja na huo UTAKATIFU ambao pasipo huo hakuna atakaemuona MUNGU.
Kuna watu wanacheza na wokovu, wanona hii neema ya wokovu ni kitu cha mzaha tu, wamejisahau kuwa kama shetani halali anafanya kila njia kukunyang'anya wokovu wako. Ili aupate wokovu wako, anaanza kukutoa kwenye UTAKATIFU. Hapo amemaliza kazi yake.
Watu tuko busy kulinda mali zetu kama mimi nilivyokuwa ninalinda begi langu, simu na pesa ambazo zingenisaidia katika safari yangu ya kuelekea Mbeya, lakini tumejisahau kuulinda Utakatifu wetu utakaotusaidia kwenda mbinguni.
Watu tuko busy kupambana na wezi wanaotuibia mali zetu, wengine hatupati usingizi kama mimi, lakini tumemsahau shetani ambaye yeye halali usiku na mchana akituwinda.
Mimi nilifuata maelekezo ya wale walioniambia historia ya dar ilivyo, nikayaelewa vizuri sana. Kwetu sisi tunaolekea mbinguni maelekezo yetu yanapatikana ndani ya neno la Mungu.
Nilikuwa makini sana kuitunza simu yangu ili mradi tu nipate mawasiliano ya kule ninakoelekea. Ingetokea nikapoteza simu tu. safari yangu ingekuwa ngumu sana.
Mawasiliano yetu ya wale tunaoelekea mbinguni ni maombi. Usikubali shetani akuibie mawasiliano haya.
Biblia inaniambia kuwa vile vyenye maana hatuvipi maana, bali vile visivyo na maana ndivyo tunavyovipa maana.
Kuna mtu anaishi hapa duniani bila hofu ya Mungu. Anaishi kwa kufanya yasiyompendeza Mungu. Yesu anatutahadharisha. Atakuja kama mwivi. Wale ambao watakuwa wameutunza utakatifu wao watamlaki mawinguni,
Wale ambao watakuwa wameishi hapa duniani kama wamefika, wakalala usingizi, wakaruhusu shetani awaibie utakatifu wao, kwao itakuwa ni kilio na kusaga meno.
Ningeweza kukueleza mambo mengi ila jambo moja ninalokukumbusha ni kuwa usiku umeendelea sana, asubuhi inakaribia, Amka lkatika usingizi wako, kaa tayari, Ishi ukijua kuwa uko safarini. Ukilala kidogo tu, jiandae kuibiwa tiketi, na kila kitu.
Mungu akubariki sana
Steven Mshiu

Jumatano, 6 Septemba 2017

MAFANIKIO YASIKUTEKE MOYO

MAFANIKIO YA KIMWILI AU YA KIROHO YASIUTEKE MOYO WAKO.
Na Steven Mshiu.
Habarini za muda huu watu wa Mungu. Naamini sote tumeanza juma hili tukiwa na nguvu na afya tele. Kwa muda wa wiki moja hivi nimekuwa kimya ni kutokana na mambo yaliyokuwa nje ya uwezo wangu.
Bado tuko pamoja.
Karibu tuendelee kubadilishana mawazo pamoja na kujifunza mambo kadha wa kadha ambayo yanaweza kuwa msaada wa maisha yetu na viroho vyetu.
Kwa nyakati za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa sana la watu wanaohubiri sana habari za mafanikio. Asilimia kubwa wamejikita kwenye mafanikio ya kimwili. Ukipita kwenye mitandao ya kijamii watu wako busy kuchangamkia fursa zinazojitokeza, huko whatapps ndio usiseme. Yapo magroup mengi sana yanayofundisha kwa wingi juu ya habari ya mafanikio ya kimwili.
Hata mimi napenda kuwa na mafanikio. Tena mafanikio makubwa sana. Na ninajitahidi kuyatafuta. Maana Biblia imeagiza baraka zinifuate. Mara nyingi nimekuwa nikisema kuwa mafanikio ya kimwili ni matokeo ya mafanikio ya kiroho. Yaani mtu anapoanza kuziogelea baraka za kimwili, ni kwamba baraka hizo zimeanzia rohoni.
Yohana anapomwandikia waraka mzee Gayo, anaanza kwa kumwambia Naomba ufanikiwe kama vile roho yako ifanikiwavyo. Ikiwa na maana kuwa baraka za Gayo zianzie rohoni kwanza.3 Yohana 1:1-2.
Kama utakuwa busy kukimbizana na kazi au na fursa ambazo unahisi huenda ukafanikiwa ukasahau kukimbizana kutafuta ustawi wa kiroho chako, utakuwa unapotea.
Kama uko busy kwenye kazi hadi unasahau muda wa kumtumikia Mungu imekula kwako. Kama moyo wako umetekwa na habari za pesa tu imekula kwako.
Mahali fulani Biblia ikasema kuwa palipo na hazina ya mtu ndipo ambapo na moyo wake ulipo. Yaani moyo unafuata pale ulipoweka juhudi kubwa. Kama umeweka juhudi kubwa kwenye kilimo, moyo wako utakuwa kwenye kilimo, kama umeweka juhudi kubwa katika kumtumikia Mungu, moyo wako wote utakuwa umejawa mambo ya kiMungu, maana hap ndipo hazina yako ilipo. Lakini anaendelea kusema kuwa jiwekeeni hazina yenu mbinguni, mahali ambapo hakuna kutu wala wezi wala chenye kuweza kuiharibu hazina yako.
Pale unapong'anga'ania kujiwekea hazina yako hapa duniani, Yaani 24/7 unatafuta pesa tu, huku ukitoa sababu kuwa hali ya maisha ni ngumu nikupongeze tu maana umechagua njia ya kupoteza. Usifikiri kuwa hutafanikiwa. La hasha. Utafanikiwa sana. Lakini jiandae kisaikolojia. Unaweza kujikuta kila unapopata pesa nondo wanakula. kutu inaharibu. wezi wanakuibia. Kwanini? Umeuruhusu moyo wako uelekee mafanikio ya kimwili.
Nikupe mfano huu ambao Yesu aliutoa.
Anasema kulikuwa na mtu mmoja alipambana na kilimo sana, Mungu akamsaidia akapata mavuno meeeengi sana, baada ya kuvuna akayaangalia yale mavuno, halafu akaziangalia ghala zake, akaanza kuwaza ndani ya moyo wake,
Kuwa atazivunja ghala za mwanzo, halafu atajenga nyingine kubwa zaidi zitakazotosha kuyahifadhi mazao yale.
Akaendelea kusemea moyoni mwake kuwa baada ya kujenga ghala hizo na kuyahifadhi mazao yake ataiambia nafsi yake kuwa sasa huu ni wakati wako wa kukaa ule, unywe na ufurahi maana nimepata mazao mengi. Wakati natafuta tafakari ya mfano huu nikajifunza kuwa pale mtu anapopata mafanikio kidogo tu wengi humsahau Mungu. Hufikiri wameyapata kwa nguvu zao tu. Hata huduma wengine huacha kabisa. HUbadili hata mfumo wa maisha. Mungu amekuinua kidogo tu hata kwenye huduma kiburi cha uzima huota. Huchukua hata ile nafasi ya utukufu wa Mungu.
Huyu mkulima alisahau mambo kadhaa, alisahau kuwa Mungu ndiye aliyenyesha mvua mimea ikaota, Akasahau kama Mungu ndiye aliyeyalinda mazao hayo na wadudu waharibifu. Inawezekana hata hakukumbuka kumtolea Mungu malimbuko. Yeye aliona ni wakati wake wa kukaa na kuanza kula. Ndivyo ilivyo kwa watu wengi siku za leo, mtu anapopata kidogo tu anajisahau kabisa.
Majibu ya Mungu kwa mtu huyu yalikuwa ni magumu sana. Mungu anamwita mtu huyo kuwa ni mpumbavu. Anamwambia Usiku huu wa leo wanaitaka roho yako. Je hayo yote uliyokuwa ukiyawaza yatakuwa ni ya nani? Unafahamu watakaokula hayo mazao yako? Jifunze kitu kimoja hapa. Mungu anamwambia kuwa WANAITAKA roho yako. Hapa sio Mungu anaitaka. Bali ni wengine wanaitaka. Soma Luka 12:16-20.
Haya ni madhara makubwa sana ya kukubali mafanikio yawe ya kimwili au ya kiroho yachukue nafasi ya ndani ya moyo wa mtu. Lusifa alitolewa kule mbinguni kwa sababu aliruhusu moyo wake uchukue utukufu wa Mungu. Kiburi cha uzima kikaota ndani ya nafsi yake, naye pia alijisemea nafsini mwake kuwa atakiinua kiti chake hadi mbinguni ili afanane na aliye juu. Kumbuka anjisemea moyoni mwake. Mungu akamshusha hadi chini kabisa. lile lengo lake halikuweza kutimia. Soma Isaya 14: 13-20.
Mpendwa rafiki, wakati Mungu anapokufanikisha hebu mtukuze na umkumbuke yeye. Kumbuka kuwa ni yeye amekupa tu kwa kupenda. Pia usisahau kumtumika Mungu. Moyo wako usitekwe na mambo ya ulimwengu huu, Tengeneza mafanikio mazuri ya moyo wako kwanza, Kumbuka maji hufuata mkondo. Baraka za kimwili nazo hufuata mkondo wa baraka za kiroho.

NEVER LOOSE HOPE

USIPOTEZE TUMAINI KWA HARAKA.
Na Steven Mshiu.
Luka 7:18-23
Nimekutana na watu wengi wakiwa wamekata tamaa kabisa. Wamechoka kuishi hapa duniani. Wengine hudiriki kusema ni afadhali kuf kuliko kuendelea kuishi,
Hali ngumu ya maisha, majaribu, magonjwa, kukataliwa, na kila aina ya mateso vimekuwa ni vyanzo vikubwa vya wanadamu kupoteza tumaini kwa haraka.
Haijalishi kuwa utakuwa kwenye mazingira gani au wewe ni nani na umefanya nini, lakini tu pale unaporuhusu nafsi kupoteza tumaini hapo ndipo unapomruhusu shetani akutese sawasawa.
Alitokea mtu mmoja aliyezaliwa kwa ishara ya kimbingu, baba yake alikuwa ni kipofu(alikuwa na tatizo la kutoona). Katika harakati za kupewa jina kukaleta utata. Ndipo baba wa mtoto alipotaka aletewe kalamu na karatasi kisha akaandika jina la mwanae.
Mama wa mtoto huyu aliitwa Elizabeti na baba yake aliitwa Zakaria. Mtoto huyu alizaliwa siku zake zikiwa bado hazijatimia. Jina lake aliitwa YOHANA. Huyu ndiye Yohana aliyembatiza Yesu.
Ni nabii aliyetabiri kipindi cha Agano la kake na Agano jipya. Ni nabii aliyetabiri habari za Yesu na akamshuhudia Yesu. Ndiye aliyekuwa mtangulizi wa Yesu. Alitabiri kazi kubwa ambazo Yesu angekuja kuzifanya hapa duniani.
Injili yake ilikuwa ni ya upako sana. Alihubiri nyakati zote, Muda mwingi aliutumia kukaa nyikani akihubiri na kubatiza watu. Watu walitoka mjini na mijini na kumfuata kule nyikani ili kusikia habari za masihi atakaekuja.
Ikafika kipindi nabii huyu akaingia katika shida. Akapoteza tumaini juu ya Yesu aliyekuwa akizisema habari zake, Kwamba hata kamba za viatu vyake hataweza kuzilegeza. Akaamua kutuma wanafunzi wake waende kwa Yesu wamuulize je Ni yeye kweli au watazamie mwingine???
Yesu akawajibu wale wanafunzi, "nendeni mkamwambie mambo mliyoyaona, kuwa watu wanapona magonjwa yao, na misiba yao, pepo wabaya wanawatoka watu, vipofu wanaona, na mambo makubwa yanatokea"
Nina imani wanafunzi hawa wa Yohana walipofikisha habari hizi kwa Yohana, Tumaini lake lilirudi. Kipindi hiki Yohana alikuwa gerezani akisubiri kuuawa. Akahisi endapo atakufa je yale aliyoyatabiri ni kweli yatatukia?
TUNAJIFUNZA NINI LEO???
*Kuna wakati unafika tunatabiri mambo makubwa kutokea lakini ghafla tumaini la kuyaona yale mambo makubwa yakitokea linapotea ghafla. Hii inaweza kuchangiwa na hali ya kimaisha tunayopitia, au magonjwa au chochote kile.
*Ulikuwa n alengo la kusona uje kuwa mtu fulani, lakini kinainuka kikwazo cha kukosa ada. Kule kukosa ada kunakufanya upoteze tumaini la kutimiza ndoto yako ya kielimu. Leo nakuletea habari hizi kuwa mambo makubwa yanatendeka, Usipoteze tumaini kwa haraka. Nafasi yako bado ipo. Hakuna aliyeijaza bado inakusubiria wewe.
*Ulikuwa na mipango mingi baada ya kumaliza chuo lakini huu ni mwaka wa saba bado hujapata kazi. Umepoteza tumaini kabisa. Umejiona kuwa wewe ni wa kushindwa tu. Waliokuwa nyuma yako wana mafanikio makubwa. Lakini wewe bado upo katika hali ngumu. Leo nina ujumbe wa matumaini kuwa USIPOTEZE TUMAINI KWA HARAKA.
Kama ilivyo kwamba usiku hauwezi kuizuia asubuhi isifike, ndivyo ambavyo shida, magonjwa na hali unayopitia haitaweza kukuzuia kuifikia ndoto yako. Usipoteze Tumaini kwa Haraka.
Nataka nimtie moyo kijana na binti mmoja kuwa, umekuwa ukishuhudia kila jumamosi wenzako wakioa na kuolewa, lakini wewe hadi leo hakuna hata aliyekusemesha. Usipoteze tumaini kwa haraka. Hata wewe siku yako itafika. Jifunze kwa sara. Alimsubiri Isaka akampata akiwa na miaka tisini, ingawa alipoteza tumaini lakini bado alilirejesha tena.
*Tambua hila na mbinu za shetani. Kazi kubwa ya shetani ni kukufanya upoteze tumaini, maana anafahamu fika kuwa mtu mwenye tumaini hana hofu juu ya chochote. Mlango mkubwa shetani anaoutumia kumpata mtu ni kumwingizia hofu. Ukipatwa na hofu tu tumaini linayeyuka.
Niliwahi kukutana na mtu mmoja akinyunyiza sijui ni dawa gani katika eneo la nyumba yake, Nilipomuuliza kulikoni, Akaniambia kuwa amepewa dawa hiyo na "mtaalamu"
ili iwe kinga ya mji na nyumba yake dhidi ya wachawi. Nikatambua kuwa mtu huyu amepoteza tumaini.
Nikamshirikisha mtu mwingine juu ya biashara fulani niliyokuwa nimekusudia kuifanya. Akaniambia kabla kabla hujaanza twende nikupeleke mahali ukapatiwe kinga na dawa. Nikamjibu kuwa nina kinga moja tu ya Yesu nawe nikupe kinga hiyo. Hakuwahi kuwasiliana na mimi tangu siku hiyo.
Mpendwa huna haja ya kwenda kwa waganga, Huna haja ya kutafuta mazindiko kutoka kwa wachawi, Huna haja ya kuogopa majaribu, Huna haja ya kuogopa vikwazo unavyokutana navyo. Bado liko tumaini la kuinuka na kusonga mbele. Biblia yangu inaniambia mahali fulani kuwa kama liko tumaini kwa mti uliokatwa kuwa utachipua tena hata kwako yale mambo yanayoonekana kama yamekufa bado yatachipuka tena.
Bado hujachelewa
Usipoteze tumainikwa haraka.
Naamini nimezungumza na moyo wa mtu mmoja.
Kama ni wewe hebu sema neno moja kuwa
"NAREJESHA TENA TUMAINI LANGU"
Inspired by Steven Mshiu
0655 882074

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...