
Na Steven Mshiu
Mara nyingi sisi kama wanadamu tumekuwa tukifikia hatua ya kuona tumesahaulika kabisa. Hali hii hasa hutokea pale tunapokuwa tumeingia katika shida au matatizo, aidha ugonjwa, mkwamo wa maisha na mambo mengine mengi tu,
Nilimsikia mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa akilalamika sana kuwa ndugu zake hawajaenda kumwona pale hospitali, akafikia hatua hata ya kulaani kabisa. Kwake kutotembelewa na ndugu zake kwa siku chache tu alijiona kama wamemshau na hawampendi kabisa.
Lakini pia ni kawaida ya wanadamu kumkimbia au kumtenga mtu aliyeingia kwenye shida fulani. Mtu huyo anaweza kuwa katika hali ya upweke mkubwa, kukata tamaa, kukosa tumaini maana hana mtu wa kumfariji.
Kipindi Yesu akiwa pale msalabani alikutana na hali hii, alihisi upweke mkubwa sana. Aliangalia wale aliowapa mikate na kuwaponya ndio hao hao wanamsulubisha.
Yusufu aliyekuwa na ndoto kubwa lakini akaangukia gerezani akiwa pamoja na wafungwa wenzake, hawakutengwa na yale matatizo yao. Lakini pale tu kulipotokea mpenyo baadhi ya wafungwa wakatoka mle gerezani. Yusufu alijihisi upweke na kuona wale wafungwa wenzake waliokuwa pamoja mle gerezani wamemsahau.
Japo wafungwa hawa waliweza kumsahau Yusufu sio kwamba Mungu alikuwa amemsahau Yusufu. La hasha. Bado kile Mungu alichokisema kwa Yusufu Ni lazima kitimie tu, Ni kiasi cha muda na wakati tuu uwadie.
Nataka nikukumbushe kitu kimoja kuwa. Mungu ni mwaminifu na ni Mungu wa maagano. Kile alichokisema juu ya maisha yako unaweza kuona kama anachelewa au amekusahau, lakini atakitimiza kwa wakati wake tuu.
Mwanadamu anaweza akakuahidi kitu lakini akasahau. Kipindi fulani tulikuwa tukijiandaa na sherehe ya kumuaga dada yetu(send Off) mtu mmoja aliniahidi mchango, lakini akasahau hivyo hakunipatia mchango ule. Lakini Mungu wetu akiahidi kukubariki ni lazima atakubariki tu.
Wakati wa Mungu kukumbuka ukifika kila mtu atashangaa, Hata wewe mwenyewe utajishangaa. Kibinadamu ni ngumu sana kutoka gerezani na kuwa waziri mkuu kwa wakati huo. Lakini hilo liliwezekana kwa Yusufu maana Mungu alimkumbuka.
Waweza kudhani Mungu amekusahau kila ukipata mchumba baada ya muda mfupi mchumba anayeyuka kama mshumaa, Mungu aliyemkumbuka Hana na Sara atakukumbuka na wewe.
Waweza kudhani kuwa Mungu amekusahau kwenye ajira vyeti vizuri unavyo, elimu nzuri unayo, Mungu aliyemkumbuka Daniel na wenzake atakukumbuka na wewe.
Umeolewa lakini unashuhudia wenzako wakiwapeleka watoto wao kliniki lakini kwako huu ni mwaka wa sita sasa, unahisi Mungu amekusahau. Mapema sana Mungu atakukumbuka kwa kukuletea Isaka.
Jambo moja la kuzingatia:
Usikubali kuchukua maamuzi yoyote yanayokujia kwenye akili yako pindi unapokuwa katika msongo wa mawazo ya kuhisi kuwa Mungu amekusahau. Sara aliamua kuchukua uamuzi wa kumshauri Ibrahimu azae na kijakazi wake Hajiri. Haya hayakuwa maamuzi sahihi kwa Sara.
Jifunze kumngoja Mungu,
Jifunze kuziamini ahadi zake.
Ongeza kiwango chako cha Subira.
Maamuzi ya Sara ni tofauti kabisa na maamuzi ya Hana.
Kumbuka wote hawa walipitia kwenye shida zinazofanana.
Usikubali shida au jaribu lako likutoe kwenye viwango vyako vya kumwamini Mungu.
Pia usisahau kumshukuru Mungu kwa chochote kile anachokutendea.
Steven Mshiu
0655 882074
0768 882074
Fr. Oct 27, 2017
