Alhamisi, 24 Agosti 2017

WAACHE WAONGEE TU

WARUHUSU WASEME TU
Na Steven Mshiu
Baba mmoja alimaliza elimu yake ya juu miaka kadhaa iliyopita ni m-bobevu kwenye masuala ya uhasibu. Akiwa ametunukiwa cheti chake kutoka bodi ya wakaguzi wa hesabu za taifa inayojulikana kama CPA,
Mwanaume huyu alizunguka na vyeti vyake vyenye ufaulu mzuri akihangaika kutafuta kazi bila matokeo yoyote. Alizunguka kila wizara, aliingia kila shirika, lile la uma hata mashirika binafsi. Lakini hakufanikiwa kazi.
Mwanaume huyu alimtumainia Mungu kwa kiwango cha hali ya juu sana. Licha ya kutumia muda mwingi kutafuta kazi, hakukosa kutenga muda wake mwingi kumtumikia Mungu, mara nyingi alikuwa akikesha kanisani kumwomba Mungu, pamoja na kufanya huduma nyingine.
Ndugu zake na marafiki zake walipomuona akitumia muda mwingi kwa mambo ya kikanisa baada ya kukosa kazi, Walianza kuongea kama ilivyo desteuri ya wanadamu.
Wakadiriki kusema, "Ona sasa mnajiita walokole. Huyo Mungu wako yuko wapi mbona asikupe kazi sasa," "Tuliwaambia walokole wamechanganyikiwa, Sasa utakula huko kanisani"
Wengine wakasema, "Twende tukupeleke kwa mtaalam" akutengenezee dawa ya "kisimati" ili upate kazi" Wengi walikejeli sana na kumdharau sana.
Yule ndugu hakukubali maneno ya wale ndugu zake yauathiri moyo wake. Aliendelea kumtegemea Mungu tu. Siku zikaenda bila matokeo ya kupata kazi, miezi ikakata, miaka nayo ikazidi kusogea,
Siku moja akiwa kanisani alipigiwa simu na mtu asiyemfahamu akielekezwa kufika sehemu fulani kwa ajili ya usaili ili aweze kupata kazi. Anasema alimshukuru sana Mungu. Hatimaye akaenda kwenye usahili huo. Mungu si Athumani alifanikiwa kupata kazi na kuanza kupewa mshahara mzuri tu huku akipewa baadhi ya promosheni nyingi tu.
Ghafla yale maneno ya wale ndugu zake yakaanza kuyeyuka ghafla kama mshumaa. Wakakosa cha kuongea tena. Mbaya zaidi wakawa wakimkwepa. Hawakupata tena ujasiri wa kumwangalia usoni.
Wakati wa Bwana ukifika wale waliokucheka na kukubeza itakuwa ni zamu yao kuaibika. Akiwa kazini yule ndugu alipata nafasi ya kujiendeleza kimasomo kwa ngazi ya Masters, Baada ya kumaliza masomo yake moja kwa moja akapata kazi ofisi ya Waziri mkuu akiwa kama mkaguzi wa hesabu za mashirika yote yaliyo chini ya ofisi ya waziri mkuu.
Mungu akamuinua kwa mfumo huo. Yale maneno ya ndugu zake yakawa ni chanzo cha baraka zake. Akathibitisha uzuri wa wokovu wake. Akamthibitisha Mungu wa Walokole mbele ya wale ndugu zake. Kwa sasa wale ndugu zake wote wanamtegemea baba huyu kwa kila kitu.
Mpendwa rafiki,
Kuna watu watasema mbona umekaa miaka bila kuoa au kuolewa? Huoni kama umri unakwenda? Waruhusu waseme tu. Kuna mambo mazuri Mungu amekuandalia mbele.
Walisema mengi juu ya Hana. Hana aliwaruhusu waseme tu. Hatimaye leo tunasoma habari za Samwel.
Unamkumbuka Yusufu?
Walisema mengi sana juu yake. Ohh Mara yule Bwana ndoto anakuja kule. Wakamkejeli sana na kumdharau sana. Yusufu hakuwazuia kusema. Biblia yangu inaniambia wakati wa Yusufu kuinuliwa na Mungu, kisima hakikuweza kuzuia, mke wa Potifa hakuweza kuzuia, Hata gereza halikuweza kuzuia. Hatimaye akawa WAZIRI MKUU. Wale ndugu zake waliokuwa wakimsema wakashiba kwa mkono wa Yusufu.
Leo huna kazi. Waache waseme tu, Mungu amekuandalia ofisi yako. Utawaajiri hao hao wanaokusema.
Leo unatembea kwa miguu, wanasema mbona umeajiriwa miaka kumi huna hata Vitz? Waache waseme tu. Kuna siku watakuomba lifti au watakuona ukiwa kwenye BMW yako.
Leo si unaishi kwenye nyumba ya kupanga? Wanasema "tulijua hata kujenga hataweza kabisa" Waache waseme tu. Kuna siku hao hao watakuja kupanga katika nyumba zako. Ulifeli darasani wakasema tulijua tu. Wa kusoma uwe wewe?
waache waseme tu, kuna siku watakuona ukitukiwa cheti kutoka chuo kikuu.
Leo chakula kwako ni cha shida. Ukipata dagaa unamshukuru Mungu. Wanasema ona watoto wamevimba tumbo, tena wana kwashakoo. Ukiomba unga kwao watakutangaza mtaa mzima. Kuwa wewe ni omba omba. Nataka nikuambie kuwa wakati wa Mungu kukufanyia kicheko cha shibe u karibu. Utakula na kusaza. Hao hao wanaokuita omba omba watahitaji vyakula kutoka kwako. Utakula na kusaza mpendwa. Waruhusu waseme tuu.
Wale waliomsema Yesu kuwa si mwana wa Mungu eti anatoa pepo kwa Belzebuli, Leo ulimwengu mzima unamtambua Yesu kama MFALME. Mtu pekee aliyekufa na kuzikwa na akafufuka. Zaidi akapaa mbinguni.
Waache waseme tu. Maneno yao ni chanzo cha baraka zako. Maneno ni daraja la mafanikio yako. Muda si mraefu watashuhudia kinyume cha yale waliyokutabiria.
Mungu akupe uvumilivu wa kubakia kimya pindi wanaposema maneno yao juu yako.
Nakutia moyo mtu wa Mungu. Kamwe usiishie njiani.
Kumbuka wahenga walisema kuwa "KELELE ZA CHURA HAZIMZUII TEMBO KUNYWA MAJI" Maneno ya adui ni kelele za chura tu. Kamwe zisikutoe kwenye lengo.
Insipired by
Steven Mshiu
0655 882074

AMELIPA GHARAMA

AMENILIPIA GHARAMA.
Na Steven Mshiu.
Mara nyingi nimekuwa nikikutana na matukio mengi ambayo yananifanya niendelee kujifunza mambo mengi sana. Kumbuka kila unachokutana nacho una jambo la kujifunza.
Nakumbuka ilikuwa ni jumanne ya wiki iliyopita majira ya asubuhi sana na mapema. Kila mtu yuko busy tena kwa mwendo wa haraka kuhakikisha anawahi katika eneo lake la kujitafutia riziki.
Nikiwa ndani ya daladala, tulifika kituo fulani, tukakuta wanafunzi wengi ambao nao wanahitaji usafiri wa daladala ili waweze kufika shuleni.
Miongoni mwa wanafunzi alikuwepo mmoja ambaye nauli yake haikutosha. Akajaribu kumsihi kondakta amsaidie, lakini kondakta alikataa kata kata, Kondakta akagonga bodi ishara ya kumruhusu dereva aondoke.
Kwa kuwa nilikuwa nimekaa seat ya mbele kabisa, Nilimuona yule mwanafunzi akiwa katika hali ya majonzi makubwa sana, Akiwa kama amekosa msaada kwa wakati ule. Akiwaangalia wenzake waliokuwa na nauli ya kutosha wao wameruhusiwa kuingia ndani ya gari.
Wakati daladala ile imeanza safari nilijisikia kukosa amani kabisa. Nikasikia sauti ikiniambia unajisikiaje kumwona mwanafunzi yule ameachwa pale. Hivi akichelewa shule si ataenda kukumbana na adhabu?
Tukiwa mwendo wa kama mita kumi na tano hivi, nilimwambia dereva asimamishe gari halafu amwambie kondakta amruhusu yule mwanafunzi aingie ndani ya gari, MIMI NITAMLIPIA NAULI,
Ghafla dereva akasimamisha gari na kumwagiza kondakta tena kwa haraka amwite mwanafunzi yule. Ikabidi nitoe uso wangu kwa nje huku nikimuashiria yule mwanafunzi aje. Alikuja kwa furaha kubwa sana, hatimaye akaingia ndani ya gari. Yule kondakta ambaye alimzuia kuingia ndani ya gari ni kondakta huyo huyo aliyemwambia njoo, tena kaa hapa. Maana kuna mtu amekulipia nauli.
Yule mwnafunzi alifurahi sana, maana hata ile nauli yake hakuitoa, kwa sababu tayari nilishamlipia.
Alipofika sehemu anayotelemkia alinishukuru sana sana. "Kaka ahsante sana sana".
Mara nyingi nimekuwa nikikutana naye kwenye daladala au nje ya daladala na kila anaponiona hunisalimia kwa furaha sana, halafu anawageukia rafiki zake na kuwaambia "kuna siku sikuwa na nauli huyu kaka akanilipia aisee"
TUNAJIFUNZA NINI???
Wanadamu tulimkosea Mungu kwa kutenda dhambi. Dhambi ikatutenga na uso wa Mungu. Dhambi hii ikavunja mahusiano kati ya mwanadamu na Mungu. Hivyo lilihitajika daraja litakalomuunganisha Mungu na mwanadamu. Gharama ya daraja hili ni lazima lijengwe au liunganishwe kwa damu
Au kwa kifupi ili mwanadamu awe karibu na Mungu ilitakiwa amwage damu yake maana yake ajiokoe kwa damu yake. Hii ilikuwa ni adhabu kubwa sana kwa wanadamu. Wapo waliojaribu kuchinja kondoo, mbuzi, njiwa, lakini damu zao zilionekana hazina thamani mbele za Mungu.
Mungu akaitisha kikao kikubwa sana mbinguni akiuliza ni nani atakaekuwa tayari kuja kuwaokoa wanadamu? Hakuna malaika yeyote, wala Kerubi wala Serafi aliyeweza kuinua sauti yake kuwa atakwenda kuwaokoa wanadamu.
Inawezekana walijiuliza maswali mengi sana, Hivi wataachaje enzi ya mbinguni ili waje kuwaokoa wanadamu?
Viumbe hawa walifahamu fika sifa za kiumbe anayetakiwa kuwaokoa wanadamu. Sifa ya kwanza ya mtu huyo ni lazima awe mwenye haki, pia awe mwenye upendo na sifa ya tatu ni lazima akubali kufa. Utasoma kitabu cha Ufunuo 5 kuzipata sifa hizi. Lilipofikia suala hili la kufa pakatokea ukimya mkuu sana kama anavyosema katika Ufunuo 5
Ndipo iliposikika sauti ya mtu mmoja aitwae YESU. Yeye alijitokeza kwa ujasiri mkubwa akiiacha enzi na utukufu wake wote uliopo mbinguni akasema "mimi nitakenda nimkomboe mwanadamu"
Kwa lugha nyepesi alikuwa tayari kulipa gharama ya makosa ya mwanadamu.
Akaja duniani akaishi kama mwanadamu kwa asilimia mia na kama Mungu kwa asilimia mia, Wanadamu hawa hawa wadhambi wakamsulubisha ili tu litimie neno.
Kwa kusulubiwa kwake akawa ameyakomboa maisha yetu kwa damu yake. Nikamkumbuka mwanafunzi huyu aliyepungukiwa nauli alivyokuwa katika sintofhamu kubwa nikafikiria maisha ya mwanadamu yangekuwa kwenye hatari gani endapo Yesu asingelipa gharama. Nikawaza huyu mwanafunzi endapo angechelewa shule angekutana na adhabu kali sana.
Vipi kwa huyu mwanadamu kama Yesu asingejitolea kulipa gharama wanadamu tungekutana na adhabu gani.?
Sisi sote ni abiria. Safari yetu inaelekea mbinguni. Nauli ni damu ya Yesu. Wale ambao hawajalipiwa nauli hii hawana furaha kabisa. Wapo kwenye wakati mgumu sana. Wanawaza kuchelewa kufika. Wanawaza adhabu itakayotokana na kuchelewa. Wanawaza mbona wenzao wana nauli ya kutosha?
Lakini wale ambao tuna nauli yaani tumeshaokolewa kwa damu ya Yesu kwetu ni furaha ya ajabu. Hatuna hofu ya kupata adhabu. Tuna uhakika wa safari.
Nikimkumbuka yule mwanafunzi niliyemlipia nauli kila akiniona jinsi anavyonichangamkia na kunisemea kwa rafiki zake huwa najisikia vizuri sana. Lakini huwa naenda mbele zaidi na mimi namkumbuka yule aliyelipa Gharama ya dhambi zangu. Yeye amenipa agizo moja tu katika Mathayo 28:18-19, Ameniagiza kuzitangaza habari zake kwa ulimwengu wooote, na kuwaambia wanadamu kuwa yeye ndiye aliyelipa gharama ya dhambi zangu.
Mpendwa rafiki,
Naomba nikuache na maswali machache ya kutafakari,
Ukiwa unasafiri halafu umepungukiwa nauli mara nyingi hukosa furaha kabisa. Hivi umeshajiuliza juu ya safari ya mbinguni? Una nauli ya kutosha?
Je kama ungetakiwa ujilipie peke yako gharama ya dhambi zako ungeweza? Ikiwa malaika mbinguni walikaa kimya wewe ungeweza?
Unairtumia vizuri nafasi uliyopewa kwa ajili ya kumtangaza huyo aliyekulipia gharama? Anasema atakayenionea haya mbele za wanadamu(Yesu) naye atamuonea haya Mbele za baba yake(MUNGU).
Mpendwa, hakuna gharama nyingine tunayotakiwa zaidi ya kufuata Yesu tu.
Kuna wimbo mmoja katika Tenzi huwa naupenda sana
Anasema "Nimekombolewa na Yesu, Aliyenirehemia, Kwa bei ya mauti yake nimekuwa mtoto wake"
Huna haja ya kuwa na hofu. Umeshalipiwa gharama. Tatizo hujijui kama umeshalipiwa gharama.
Ni kazi yako kutafuta kujua kama umelipiwa gharama.
Na Steven Mshi

Jumatatu, 21 Agosti 2017

TUNZA UWEPO WA MUNGU MAISHANI MWAKO

SIKU UWEPO WA MUNGU UKIONDOKA.
Na Steven Mshiu.
Aliomba mvua isinyeshe kwa muda wa miaka mitatu na nusu, nayo haikunyesha, MAANA UWEPO WA MUNGU ULIKUWA JUU YAKE.
Alishusha moto kutoka mbinguni ukaiteketeza ile sadaka.
Yule mwanamke wa Sarepta alibarikiwa kupita maelezo kwa neno lake.
Maana Uwepo wa Mungu ulikuwa juu yake.
Hata yule mtoto wa yule mjane aliyekuwa amekufa aliweza kufufuka kupitia yeye.
Aliweza kumthibitisha Mungu wake mbele ya wale manabii 450 wa Baali.
Na kwakuwa wale manabii wa Baali walishindwa kumthibitisha mungu wao aliweza kuwaua woote. Mtu mmoja akawaua watu 450 kwa ajili ya Mungu wake.
Lakini mtu huyu huyu aliyefanya mambo makubwa tena ya kuushangaza ulimwengu, alitishwa na mwanamke tu aliyeitwa Yezebeli, Akakimbia na kuketi chini ya mti huku akijiombea afe. Kwanini, Vitisho vya Yezebeli vilimfanya apoteze ule uwepo wa Mungu maishani mwake.
Huyu ndiye ELIYA aliyenyakuliwa kwa gari la moto. 1 Falme 16-19.
Alizaliwa kama mnadhiri wa Mungu.
Siku moja akiwa anaenda Timna alikutana na simba akamkamata na kumuua.
Alipotakiwa kulipa kile alichowaahidi wale watu juu ya kile kitendawili, aliweza kuwakamata wanaume 30 akawanyang'anya yale mavazi.
Walipomuudhi kwa kumchukua yule mchumba wake alikamata mbweha 300 akawafunga mikia wawili wawilihalafu akachoma ngano ya wafilisti.
walipojua kuwa yupo mjini wakapanga njama za kumkamata. Aling'oa lango(geti) kuu la mji halafu akalipeleka juu ya mlima. Huyu ni mtu mmoja tuu.
Akafika tena mji mmoja wakamkamata na kumfunga Roho wa Bwana akaja kwa nguvu juu yake akawaua watu 1000 kwa taya la punda.
Uwepo wa Mungu ulikuwa juu yake.
Mtu huyu huyu ndiye aliyekubali kulazwa kwnye mapaja ya Delila na akanyolewa nywele. Uwepo wa Mungu ukamtoka.
Hatimaye anakamatwa anatobolewa macho na kutupwa gerezani kisha anapewa kazi ya kusaga ngano.
Jina lake ni Samson. Amuzi 13-16.
Alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wa Yesu.
Alitembea juu ya maji kwa Neno la Yesu. Akamkata sikio yule askari walipokuja kumkamata Yesu. Aliapa ataambatana na Yesu hadi kifo.
Lakini anakuja kutishiwa na kijakazi tu hatimaye akamkana Yesu
Huyu jina lake ni Petro.
Mpendwa,
Hakuna kitu cha maana kama kuutunza uwepo wa Mungu maishani mwako. Kamwe yeye hatakuacha. Ijapo tunaanguka ila tuna kila sababu ya kuuhitaji uwepo wa Mungu juu ya maisha yetu. Daudi alikuwa mkosaji mara nyingi sana, lakini aliutambua umuhimu wa uwepo wa Mungu juu ya maisha yake.
Nakukumbusha kuwa shetani hafurahii wewe kuwa chini ya uwepo wa Mungu. Anasubiri tu ufanye kosa dogo tu aanze kukunyanyasa. Anasubiri uanguke kwenye dhambi aanze kukutesa.
Anakusubiri akutoboe macho kama Samson.
Anasubiri uwepo wa Mungu ukuondokee aanze kukutia hofu ya kujiua.
Anatumia mbinu nyingi sana kuhakikisha anakunyanyasa.
Lakini nakutia moyo kuwa, bado una nafasi ya kuuhitaji uwepo wa Mungu juu ya maisha yako kwa nafasi nyingine.
Eliya alipokuwa chini ya mretemu Mungu alimtia moyo kuwa Safari bado ni mbichi.
Samson alikuja kuwaua watu wengi zaidi ya wale aliokwisha kuwaua hapo mwanzo,n.k
Nikutahadharishe jambo moja. Usifikiri kuutunza uwepo wa Mungu ni kazi rahisi. Kuna gharama za kulipa. Gharama za kuutunza uwepo wa Mungu ni kuishi maisha ya Utakatifu. Maisha ya kujikana. Maisha ya kujitenga dhambi. Vinginevyo utakugarimu uhai wako kama Samson.
Steven Mshiu.

NGUVU YA MACHO

NGUVU YA MACHO.
Na Steven Mshiu,
Shalom watu wema wa Mungu. Naamini tumeianza wiki yetu vyema kabisa. Wiki iliyojaa ushindi mkubwa. Wiki itakayokuwa ya baraka sana kwako.
Leo nataka nikuletee makala hii fupi tu kuhusu nguvu ya macho.
Asilimia kubwa ya viumbe hai hususani wanyama vina macho. Mungu alipomuumba mwanadamu alimpa macho. Wakati wanyama wanapita mbele ya macho ya Adam, Alipowaangalia tu, akaanza kuwapa majina. Wewe utaitwa tembo, wewe utaitwa sungura. Bila shaka wewe utakuwa chura.
Kazi kubwa ya macho ni kupeleka taarifa kwenye ubongo, ili ubongo uweze kuanza kazi ya kuzichakata hizo taarifa ili kuleta majibu.
Kwa mfano,
Nimeona gari zuri au nyumba nzuri kwa kutumia macho. Sasa nataka nichore picha niliyoiona. Tayari macho yanapeleka ile picha ya gari au ile nyumba kwenye ubongo, Ubongo nao unaanza kazi ya kuchakata muonekano wa kitu nilichokiona halafu unakileta katika mchoro wa picha. Kwa hiyo inafanyika kazi ya kuhamisha ile nyumba niliyoiona, kutoka kwenye muonekano wake halisi halafu naileta kwenye mfumo wa picha.
Naweza kusema kazi kubwa ya macho ni kutransform kitu kutoka kwenye ule muonekano wake na kukipeleka kwenye ubongo ili kupata matokeo chanya au hasi, kutokana na ubongo utakavyoitafsiri hiyo picha.
Macho ni taa ya mwili. Kazi nyingine kubwa ya macho ni kuhakikisha kuwa mwili unakuwa salama kabisa. Siku moja nilikuwa natembea maeneo fulani, ghafla mbele yangu kulikuwa kuna nyoka. mguu haukuweza kumwona yule nyoka. Lakini macho ndiyo yaliyomwona yule nyoka, yakapeleka taarifa kwenye ubongo, ubongo nao nao ukapeleka taarifa kwenye miguu, kuwa ni wakati wa kukimbia.
Jana baada ya ibaada, nikawa nimekaa peke yangu huku nikitafakari mambo mengi kuhusu macho. Tafakari yangu ikaanzia kwenye Zaburi 119:37, "Unigeuze macho yangu nisitazame visivyofaa, unihuishe katika njia yako.
Anaeandika au anaesema maneno haya alishakutana na madhara ya matumizi mabaya ya macho. Wakati wanaume wameenda vitani yeye akabaki amelala gorofani kwake akamwona mwanamke anaoga, macho yake yakapeleka taarifa hasi kwenye ubongo wake na kumletea majibu kuwa ni vizuri akalala na huyo mwanamke, naye akafanya hivyo, Zaidi ya hapo bado akaongeza dhambi nyingine ya kuua kwa kukusudia. Huyu ni DAUDI 2 Samwel 11:1-5,
Nikaendelea mbele zaidi, nikakutana na mtu mwingine aliyeishi maisha ya utakatifu, ambaye alijitenga na dhambi kwa kiasi kikubwa sana, Biblia inamsifu kuwa alikuwa ni mtu mkamilifu sana, Hakupenda kumkosea Mungu Kwa namna yeyote ile. Hata aliposhawishiwa na marafiki zake na watu wake wa karibu amkufuru Mungu ili afe, yeye alikataa, Nikatafuta sana siri ya ushindi wake. Nikagundua kuwa yeye aliidhibiti nguvu ya macho yake. Huyu ni AYUBU.
Katika Ayubu 31:1, Anasema, "Nilifanya AGANO na MACHO yangu, Basi nawezaje kumwangalia msichana?"
Nikaendelea kujiuliza maswali mengi juu ya huyu Ayubu. Kwani kuna mvutano gani kati ya macho na msichana? Kwani hao wasichana wana tatizo gani? Anyway. Nikamkumbuka tena mtu anaeitwa YUSUPH na Mke wa Potifa. Yule mke wa Potifa alikuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa Yusuph, Aliamini atakapovua nguo mbele ya Yusuph, basi hapo Yusuph hatakuwa na ujanja. Ni lazima angeingia kwenye kumi na nane zake kama wanavyosema vijana wa siku hizi. Lakini mtu huyu Yusufu naye alishafanya maagano na macho yake ili asimtende Mungu dhambi.
Nikasema labda hizo zilikuwa ni sheria za Agano la Kale.
Nilipokuja kwenye Agano Jipya Hapa ndipo niliishiwa nguvu kabisa. Maneno ya Yesu mwenyewe anahitimisha kwa kuonyesha nguvu ya macho. Kuwa macho yanaondoa kitu kutoka mfano wa picha na kukileta kwenye uhalisia.
Katika Mathayo 5:27-28, anasema, "Mmesikia imeandikwa usizini, Lakini mimi nawaambia kila mtu amtazamaye mwanamke kwa kumtamaniamekwisha kuzini naye moyoni mwake" Hapa nikafunga Biblia yangu nikasema Ee Mungu naomba nifanye Agano na macho yangu ili nisitazame visivyofaa, ili niweze kuwa hai na kubaki kwenye njia yako.
Haya macho yetu haya yatatusababisha tuikose mbingu hivi hivi, Siku moja nilishika simu ya kijana mmoja simu imejaa video zisizo na maadili ya mkristo, video za utupu, nikamuuliza ukishaangalia hizi video nini huwa kinafuata? Alikosa cha kunijibu nikamwambia unahitaji kuokoka upya.
Macho yetu huzalisha nguvu ya tamaa. Shetani alipojaribu kumpima Yesu kwa kutumia tamaa ya macho alimpandisha juu ya mlima mrefu na kumwonyesha milki zooote za dunia akidai kuwa atampa Yesu milki zote hizo endapo tu Yesu atamsujudia. Sio kwamba Yesu hakuziona hizo milki zote na uzuri wote. Yesu alikwisha fanya Agano na macho yake kuwa asitazame vitu vitakavyomtoa kwenye lile kusudi lake.
Watu wengi wamepoteza MAKUSUDI yao, kutokana na tamaa ya macho. Wengi wameshindwa kuizuia/control nguvu inayozalishwa na macho. Unaona mali nzuri ya mtu, badala ya kufanya kazi kwa bidii, na kuusumbua ubongo wako, unaruhusu taarifa kutoka kwa macho yako ambayo inaenda kuchakatwa kwenye ubongo wako ikuletee majibu ya kuiba hiyo mali. This is dangerous.
Ninapomalizia nitoe mtazamo wangu mimi kama mimi. Wahenga walisema kuwa macho hayana pazia. Viko vitu vingi tunaviona kwa macho yetu. Jambo la msingi ni kuyazuia au kuizuia taarifa ambayo macho yanaipeleka kwenye ubongo wako. Ukiona unatazama kitu halafu kikawa kinakuelekeza kuchukua maamuzi yasiyo mazuri chukua tahadhari kubwa. Yusufu alimkimbia mke wa Potifa. Akawa salama na akalitunza kusudi lake. Daudi yeye aliamua kuchukua hatua ya kulala na mke wa Uria.
Yesu yeye aliziona milki zote za dunia lakini akamjibu shetani hivi, "Nenda zako shetani. Imeandikwa msujudie Bwana Mungu wako umwabudu yeye peke yake"
Baada ya Yesu kumshinda shetani kwa kuizuia nguvu ya tamaa inayozalishwa na macho Biblia inaniambia kuwa shetani alimwacha na malaika wakaja kumtumikia Yesu.
Tunahitaji kuishi kwenye lengo. Ni lazima tupambane na hali zote zinazotutoa kwenye lengo. Sijui kwanini Biblia inapiga sana vita dhambi ya uzinzi. 2 petro 2:12.
Mungu anisaidie niidhibiti nguvu inayozalishwa na macho yangu
Steven Mshiu.
0655 882074
0768 882074
smshiu42@gmail.com

Jumatatu, 14 Agosti 2017

SIMAMA PEKE YAKO.

SIMAMA PEKE YAKO HATA KAMA HAKUNA ANAYEKUUNGA MKONO.
Na Steven Mshiu
Mwaka jana nikiwa na rafiki yangu Elias Kisingi, tulipata muda mzuri wa kujifunza juu ya kitabu cha Ayubu sura hadi sura.
Tulitumia zaidi ya miezi mitatu tukijifunza juu ya kitabu hiki kuanzia maisha ya Ayubu. huduma yake, njia zake pamoja na mambo mengi sana.

Maisha ya Ayubu yalikuwa ni mfano tosha na kielelezo kwa wanadamu wote waliopo juu ya uso wa dunia. Biblia inamsifu kuwa alikuwa ni mtu mkamilifu wala hila haikuonekana ndani yake.
Maisha yake ya kiroho sichelei kusema kuwa yalikuwa ni ya viwango vya hali ya juu. Alitambua maana ya kumtolea mungu, Mara nyingi alitoa sadaka za kuomba rehema kwa Mungu juu ya familia yake.
Wakati fulani Mungu aliruhusu shetani amjaribu Ayubu. Ayubu huyu ambaye hakuwa mtenda dhambi akaanza kupitia katika vipindi vigumu sana katika maisha yake. Mali zake zikaisha, watoto wakafariki. Hali yake ya kiuchumi ikawa mbaya sana. Kumbuka Biblia inaposema kuwa alikuwa ni tajiri, ni tajiri kweli kweli. Licha ya kuwa tajiri Ayubu alimcha Mungu.
Kama unavyofahamu kuwa mtu anapokuwa tajiri huwa na marafiki wengi sana. Jambo la muhimu la kufahamu je siku ukiishiwa hao marafiki watakuwa na wewe.
Hali ilipozidi kuwa mbaya kwa Ayubu, walewale marafiki zake waliokuwa wakila pamoja, wakinywa pamoja na kufanya mambo mengi kwa pamoja walimkimbia, Wakadiriki kusema kuwa Ayubu ametenda dhambi. Lakini haikuwa hivyo.
Hata mtu wa karibu sana wa Ayubu ambaye walilala kitanda kimoja alidiriki kufika hatua ya kumwambia Ayubu amkufuru Mungu ili afe.
Kitu ambacho nilitaka kukukumbusha ni kwamba ni vyema ukasimama wewe kama wewe mwenyewe pale unapopatwa au kukumbwa na chochote. Mara nyingi wale watu wa karibu wanaweza wakakuacha, mke wako anaweza akakuacha, familia yako ikakuacha, hata mpenzi wako akakuacha. Watu hawa wanaweza wakawa na dhamira nzuri za kukusaidia lakini dhamira zao zikawa ni anguko kwako, Kama Ayubu angefuata ushauri wa mke wake nahisi angekuwa ni mtu wa ajabu sana.
Kila mtu anapokuwa kinyume na wewe, jitahidi kusimamia kile unachokiamini. Ayubu hakufuata ushauri wa akina Elifasi, Elihu, Bilidadi wala mke wake. Biblia inaniambia kuwa mwisho wa Ayubu ulikuwa mkubwa kuliko ule mwanzo wake. Alibarikiwa zaidi kuliko ilivyokuwa mwanzo.
Kwanini?
Ayubu alisimama peke yake ingawa kila mtu alikuwa kinyume na yeye.
Mungu amekusudia kuufanya mwisho wako kuwa bora zaidi ya mwanzo wako. Lile wazo la biashara ulilo nalo kuna watu umewaambia, lakini mawazo yao ni kama yale ya mke wa Ayubu, Wengine wanakuambia huwezi kufanikiwa kupitia wazo hilo. Ni wakati wako wa kusimama peke yako.
Mwisho mzuri unaandaliwa na mwanzo mzuri. Mwanzo mzuri ni yale mawazo ya kwanza kabisa yanayotokea kwenye akili yako. Unatamani kuwa mtumishi mkubwa wa Mungu lakini kuna watu wana roho ya Herode au ya Farao ya kutaka kumuua mtoto, Ni wakati wako kusimama peke yako.
Steven Mshiu

WEWE NI WA TOFAUTI. KUWA WA TOFAUTI.

TAFUTA KUWA NA UTOFAUTI
Habarini za asubuhi wapendwa. Ni matumaini yangu kuwa mmeamka mkiwa na nguvu na afya tele ambayo tumepewa bure na Muumba wetu.
Nikupongeze wewe ambaye tayari umeshayaanza majukumu yako ya kila siku ya kujitafutia riziki ili mkono uweze kwenda kinywani. Biblia inatuagiza kufanya kazi. Hivyo ni vyema ukazidi kuweka juhudi kubwa juu ya kile unachokifanya.
Kila siku tunapitia mambo au changamoto ambazo tunajifunza kutokana nazo.
Moja ya changamoto ambayo tunakutana nayo ni ile hali ya kushindwa kujitofautisha.
Kuna mtu unaweza kumkuta mahali fulani na ameridhika na sehemu ile alipo lakini kwa hadhi na heshima yake asingestahili kuwepo sehemu hiyo. Kwa mfano, huku kwetu uchagani kuna vilabu vya pombe ya kienyeji huwa wanaiita mbege, Itashangaza sana kumkuta mchungaji au mtumishi wa Mungu ameketi kilabuni pamoja na wanywaji wa pombe hiyo bila sababu maalum. Mtu huyo atakuwa ameshindwa kujitofautisha.
Au umkute kiongozi mkubwa wa serikali amekaa kijiweni na watu wasiokuwa na kazi wakipiga hadithi tu bila mantiki yoyote. Kiongozi huyo atakuwa na walakini mkubwa sana.
Kipindi cha huduma ya Yesu, mara nyingi alijitofautisha sana na Wayahudi kuanzia usemi, namna ya kuishi n.k. Sababu za kujitofautisha ni ili ile kazi yake au huduma yake aliyokuwa akiifanya iweze kukubalika.
Utofauti unakufanya uwe mtu wa tofauti. Mtu wa tofauti ni lazima afanye mambo tofauti kabisa na yale wanayoyafanya watu walioshindwa kujitofautisha. Unapofanya kitu cha tofauti mara nyingi kitu hicho hudumu kwa muda kwa muda mrefu lakini endapo utafanya kitu au jambo lolote kwa mazoea jambo hilo haliwezi kudumu kwa muda mrefu.
Ngoja nikupe ushuhuda huu mfupi, Siku tatu zilizopita nikiwa nimetoka kazini kwangu, Mara nyingi huwa natumia usafiri wa daladala. Nikapanda daladala moja hivi kutokana ile hali ya uchovu wa siku nzima nikawa nimetulia tu kwenye moja seat ya katikati ya daladala hiyo, mbele yangu walikaa watu wanne na nyuma yangu walikaa watu wanne pia.
Tukaanza safari, Nilipoangalia wale waliokuwa wamekaa mbele yangu walikuwa busy sana na smartphone zao, kuna mbao walikuwa wakiangalia nyimbo kwenye Youtube, wengine walikuwa wakichat faceook na whatsapp, vivyohivyo hata wale wa nyuma yangu nao walikuwa very busy kuchat, na kuangalia video/nyimbo kwenye youtube.
Nikawaangalia tena wale abiria waliokaa pembeni yangu nao pia walikuwa busy kuangalia mitindo ya nguo na nywele kwenye simu zao. Nikawaza sana. Hivi na mimi nitoe simu yangu nianze kuperuzi facebook na Whatsapp?
Nikasikia sauti ikiniambia tafuta kuwa tofauti na hawa wote, nikawaza sana nitawezaje kuwa tofauti nao? Kwa bahati nzuri nilikuwa nimebeba Biblia yangu kwenye bahasha ya A4, nikaitoa bila woga wala wasiwasi na nikaanza kujisomea zangu Biblia.
Nami nikawa very busy nikiperuzi baadhi ya mistari kwenye Biblia yangu. Jambo la kushangaza na la ajabu wale waliokuwa very busy wakichati walibadilisha topic na kuanza kusema huyu kaka atakuwa ameokoka. Nami bila kusita nikawajibu Bila shaka. Hatimaye safari yetu ikazidi kusonga mbele.
Wakaanza kuniuliza maswali kuhusu Biblia, nami nikawajibu. Hivyo nikafanikiwa kuwabadilisha kile walichokuwa wakikifanya wakajiunga nami.
Nikajifunza jambo lingine kuwa watu wako tayari kukufuata kwenye kile unachokifanya endapo utaonyesha utofauti. Kijana niliyeokoka niwe tofauti na wale ambao hawajaokoka. Wao wakivalia suruali chini ya makalio basi mimi nivalie kiunoni vizuri tena nimechomekea ikibidi na tai nifunge. Kwanini? Natafuta utofauti.
Binti uliyeokoka wakati wenzako wamevalia nusu uchi, basi wewe waonyeshe utofauti kwa kuvalia mavazi yanayousitiri mwili wako. Wakati wao wanatafuta kuufanania ulimwengu wewe tafuta utofauti kwa kutaka kumfanania Kristo, kuanzia usemi wako, mwenendo wako, na hata maisha yako ya ujumla.
Heshima hufuata utofauti. Unaweza kujikuta unaitwa majina fulani fulani kwa sababu tu umeonyesha utofauti au umeshindwa kuonyesha utofauti, Kulikuwa na wana wa Sikewa wao walipokutana na mtu mwenye pepo wakaanza kumkemea kwa Jina la Yesu anaehubiriwa na Paulo, Pepo wakamjibu Paulo tunamfahamu, Na hata Yesu tunamfahamu. Je ninyi ni akina nani? Watu hawa walishindwa kutambua tofauti iliyopo kati yao na Paulo. Wakajikuta wakiaibika mbele ya pepo. Mdo 19:13-16
Epuka kufanya vitu kwa mazoea au namna wenzako wanavyofanya. Wewe umeumbwa kwa utofauti. Wewe ni tofauti na mimi, Na hata mimi ni tofauti kabisa na wewe. Mungu anampenda mtu anayefanya vitu vya tofauti. Lakini tofauti ninayizungumzia hapa ni ile inayojenga tu. Ukitafuta kufanya vitu vya utofauti wenye tofauti hasi imekula kwako.
Yuda Iskariote yeye alitafuta utofauti wake kwa kumsaliti Yesu, Kilichomkuta ni siri yake mwenyewe.
Nikutie moyo.
Yawezekana umekuwa ukifanya mambo kwa hali ya ukawaida tu, Leo una nafasi ya kuanza kufanya kwa hali ya tofauti kabisa. Usijali dunia itakuonaje. Au watu watakusemaje. Wewe fanya jambo la tofauti.
Jifunze kwa Elisha na Eliya. Kipindi Eliya anakaribia kunyakuliwa kwa magari ya moto, Elisha alidhamiria kumfuata hadi mwisho.
Licha ya kukatishwa na tamaa na miongoni mwa watu wa karibu naye tena manabii, yeye aliwajibu jibu moja tu, Ndio. Nafahamu atanyakuliwa ila niacheni. Elisha alitafuta kuwa tofauti na mawazo ya wale manabii. Mwishowe wale manabii walikuja kuwa chini ya Elisha.
Mungu amekusudia kukuweka sehemu fulani. Amekusudia kukubariki. Amekusudia kukufanyia muujiza mkubwa kwenye kazi yako, kwenye biashara yako, kwenye masomo yako, kwenye familia yako au popote pale utakapopita endapo utaamua kuonyesha utofauti tu.
Mungu akubariki sana kwa kuwa utatafuta kuwa wa tofauti.
Na Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074

Alhamisi, 10 Agosti 2017

KUTOAMINI NI DHAMBI INAYOUA

KUTOAMINI-DHAMBI INAYOUA
Na Steven Mshiu.
Habari za wakati huu mpendwa rafiki. Naamini umekuwa na siku njema ya leo. Hakika Mungu ni mwema kwetu maana anatuwezesha hata pale ambapo akili zetu zinafikia ukomo.

Ahsante kwa wewe ambaye unafuatilia makala zangu, naamini kuna kitu au vitu huwa unajifunza, kutiwa moyo na kuinuliwa tena. Sisi sote tu viungo katika mwili wa Kristo hivyo ni lazima tujengane kila iitwapo leo.
Tangu jumatatu sikuweza kuandika makala yoyote, lakini nilikuwa nikitafakari kila siku kuwa ni kitu gani Mungu anataka kuwakumbusha watu wake kwa wakati huu.

Juzi niliweka headline hii inayosema "KUTOAMINI NI DHAMBI INAYOUA. Hivyo tangu jumatatu nimekuwa nikijiuliza maswali mengi sana kuhusu IMANI,

Kipindi Yesu akiwa hapa duniani, akifanya huduma huku na kule akihubiri na kuponya wagonjwa alikuwa anakutana na changamoto nyingi sana.

Moja ya changamoto alizokuwa akikutana nazo ni juu ya suala la imani. Wako ambao imani zao za kupokea muujiza zilikuwa ni ndogo sana, Si kwamba Yesu alishindwa kuwaponya. La hasha. Kabla Yesu hajawaponya alianza kuziponya imani zao kwanza. Kama wewe ni msomi wa Biblia utaona mara nyingi Yesu alikuwa akiwaambia wale wagonjwa. Inuka. Jitwike godoro lako uende. Imani yako imekuponya,

Mara njingi sana Yesu alikuwa akiwaambia "Imani yako imekuponya". Namkumbuka yule mtumwa wa yule akida. Akida alipokwenda kwa Yesu akihitaji uponyaji wa mtumwa wake, Alipojenga imani yake kwa Yesu na kumwambia kuwa hakuna haja ya Yesu kwenda hadi nyumbani kwake akisema neno tu yule mtumwa atakuwa mzima. Yesu aliishangaa sana imani ya akida huyu. Kulingana na imani yake yule mtumwa akawa mzima.

Namkumbuka yule mwanamke aliyekuwa akitokwa na damu kwa zaidi ya miaka 12. Akaamini kuwa atakapolishika pindo la vazi la Yesu tu, hakika atakuwa mzima. Ikatokea kama alivyoamini. Akawa mzima kulingana na imani yake.

Wako watu wanne waliokuwa na mgonjwa wao. Walizunguka kila mahali kutafuta uzima wa mgonjwa wao lakini juhudi zao zikagonga mwamba. Waliposikia habari za Yesu na matendo yake ya uponyaji, imani yao ikajengeka na kuwa kubwa sana. Wakiamini kuwa Yesu atamponya mgonjwa wao. Lakini wakakutana na tatizo la kusongwa na watu. Wakakosa nafasi ya kumfikia Yesu.

Nikukumbushe jambo moja la muhimu sana, imani huwa haiangalii gharama.
Wakaamua kukwea juu ya nyumba na kuanza kubomoa nyumba, yaani paa la nyumba ili tu wamfikishe mgonjwa wao kwa Yesu, Walipomaliza Biblia inaniambia Yesu alipoangalia imani ya wale watu akamponya yule mgonjwa.

Kiasi kile unachoamini ndicho kiasi sahihi cha mafanikio au matokeo uliyo nayo, Yule mwanamke wa Sarepta aliyeambiwa na Nabii atafute vyombo vya kuweka mafuta. Aliamini vile vyombo alivyotafuta vingemtosha, Na kweli alipokea mafuta kulingana na idadi ya vyombo aliyokuwa navyo, Najaribu kuwaza kama angetafuta vingi zaidi ndivyo ambavyo angepokea mafuta mengi zaidi.

Hadi hapa nikawa nimeziona faida nyingi sana za kuamini. Nikarudi kwa Naamani aliyekuwa mwanajeshi mwenye ukoma, Alipoambiwa akaoge mto Yordan mara saba, akataka kukataa, lakini aliposhauriwa imani yake ikakua alipoenda kuoga tu, ile imefika mara ya saba akawa mzima kabisa.

Mpendwa rafiki imani yako haiwezi kukua kama hakuna au huna kitu chochote kitakachoifanya imani yako kukua. Imani huanzia kwenye mambo madogo tu, au yale ambayo hayaonekani.
Katika Ebrania 11:1, Inatueleza kuwa imani ni kuamini au kuwa na uhakika kwenye vitu vinavyoonekana au visivyoonekana, Wengine wanasema ni kuwa na hakika. Naam nami naafiki.

Lakini sikuishia hapo kwa kupata tu faida za kuwa na IMANI. Nikajaribu kuwaza kuwa ikiwa mtu hataamini ninini kitatokea? Nikapata majibu kuwa ni lazima mauti imkute mtu huyo. Yohana 3:16-18, Biblia inasema kwenye mstari huu wa 18 kuwa "Aaminiye hahukumiwi, asiyeamini amekwisha kuhukumiwa kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.

Kuhukumiwa inayozunguzwa hapa ni kule kuangukia jehanum moja kwa moja. Hukumu hii haina rufaa. Ukiangukia jehanam, Huo ndio umauti wa milele. Hivyo nikaamini kuwa kutokuamini ni dhambi inayoua.
Nilipoendelea kuyatafuta maandiko zaidi ndipo nikakutana kisa hiki cha ajabu sana cha akida mmoja katika kipindi cha Elisha.

Ilitokea kipindi fulani Elisha aliomba mvua isinyeshe kwa muda wa miaka mitatu na nusu katika taifa la Israel. Ikafikia hatua watu wanakula mavi ya njiwa na vichwa vya punda, Bidhaa hizi zilikuwa zikiuzwa ghali sana. Ilikuwa ni hali mbaya sana ya njaa kwa taifa la Israel,

Baada ya miaka mitatu na nusu kuisha Elisha anatoa unabii kuwa baada ya muda hali itakuwa shwari, Watu watakula na kustarehe, Lakini anatokea mlinzi mmoja wa mfalme, anatofautiana na Elisha, 2 Wafame 7:2, Akasema hivi Tazanma kama Bwana angefanya madirisha ya mbinguni je jambo hili lingewezekana????
Elisha anamjibu kuwa yeye ataangalia tu kwa macho wengine wakipata chakula, wale walioamini.

Mungu akaamua kuwatumia wakoma kuleta ushindi mkubwa juu ya taifa la Israel kwa kuwatisha washami wakakimbia wakaacha kila kitu kambini. Israel wakapata chakula kama neno la Elisha lilivyosema,
Cha kusikitisha yule akida ambaye hakuamini yeye aliwekwa getini kusimamia watu wakipata chakula. Msongamano ukawa mkubwa sana. Watu wakamkanyaga yule akida hadi akafa.
Kutoamini kwake kukamsababisha yule akida aone kwa macho tu lakini hakupata chochote zaidi ya kukumbwa na kifo. 2 Wafalme 7:17-19

Mpendwa rafiki,
Nataka nikukumbushe mambo machache.
Mungu hampendi mtu asiyeamini. Mtu asiyeamini hana muda wa kusoma Neno la Mungu. Imani huja kwa kusikia. Na kusikia Hutokana na Neno la Mungu. Kupitia Neno la Mungu huwa tunamsikia Mungu akisema na maisha yetu,

Imani husababisha mambo yatokee. Vitu vyote vinavyoonekana juu ya uso ni matokeo ya imani. Kumbuka imani ni matokeo ya Neno. Mungu aliumba kwa Neno(Imani) Tunaokolewa kwa kujenga imani yetu kwa Yesu. (Amwaminiye Mwana Yu na uzima tele).

Kutoamini kutakufanya ushuhudie wengine wakitendewa miujiza tu mwisho wake wewe utakufa bila kutendewa. Jifunze kwa huyu akida kwenye 2 Wafalme 7:18.

Kutokuamini kutakufanya wewe uwe daraja la wale wanaoamini katika kuelekea kupata kile wanachokiamini. Epuka dhambi ya kutokuamini sasa,

Nimalizie kwa kukutia moyo kuwa Yesu akamwambia Martha kuwa ukiamini utauona ukuu wa Mungu. Martha alipoamini na kuliondoa jiwe hakika Lazaro alifufuka.

Kuna mambo umeyaua mwenyewe kwa kutokuamini kwako. Lakini leo nakukumbusha kuwa ukiamini tu, yataenda kufufuka tena, jambo la kuzingatia ni kuliondoa jiwe la kutoamini tu ndani ya moyo wako.

Ahsante sana, Mungu akubariki na kukuinua tena wewe ambaye nimezungumza nawe.
Unaweza ku-share ujumbe na rafiki yako ukimkumbusha kuwa kutoamini ni dhambi inayoua, ili imani yetu ikue hatimaye kuiathiri dunia.

Rafiki yako,
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

Jumatatu, 7 Agosti 2017

KUNA HAJA YA KUOMBA KWA AJILI YA VIJANA

KUNA HAJA YA KANISA KUOMBA KWA AJILI YA VIJANA
Na Steven Mshiu.
Siku mbili zilizopita nikiwa katika tafakari yangu binafsi juu ya mustakabali wa maisha yangu kama kijana, nilijihoji maswali mengi sana.

Katika maswali niliyojihoji ni kuwa mimi ni nani? Ni kitu gani natakiwa kufanya nikiwa kama Kijana? Je jamii inautambua mchango wangu? Ni Kwa kusudi lipi nipo hai hadi leo? Kanisa linatambua nafasi yangu kama kijana? Je naitendea haki nafasi yangu?

Biblia inamzungumziaje kijana? Kwa nini nyakati hizi vijana wengi hawana muda na Muumba wao?
Kwanini vijana wengi tunajikuta tumeshaangukia katika kutenda dhambi? Tatizo liko wapi? Je ni hatua gani za kuchukua ili kuweza kutatua tatizo hili?

Baada ya kujiuliza maswali haya na mengine mengi tu, nikajumlisha na utafiti wangu mdogo nilioufanya kwa muda mchache sana ambao nilibaini mambo kadha wa kadha kuhusiana vijana.

Mambo niliyoyabaini ni kwamba, Kwa nyakati hizi vijana wengi hasa waliopo kwenye makanisa ya kiroho wapo kwenye mahusiano yasiyo rasmi kabisa. Mvulana na msichana wanaishi kama tayari walikwisha oana siku nyingi tu, Binti yupo tayari kwenda kwa kijana tena mwenyewe na wanaweza kukaa hata kwa muda mrefu wakiwa wenyewe tu. Hata the way, wanavyotembea, maongezi, na michezo yao inaakisi mahusiano yasiyo rasmi kabisa.

Pia nilibaini asilimia kubwa ya vijana hawaendi kanisani. Hawana muda wa ibada. Nilitembelea kanisa moja ili kuzungumza na vijana ila nilikuta vijana 12 tu, wa kiume wanne(4) na mabinti 8, Nilipowauliza kuna vijana wangapi kanisani hapo niliambiwa wapo 37, maana yake ambao hawajaenda kanisani siku hiyo ni mara mbili ya walioenda kanisani siku hiyo.

Kati ya hao vijana 12., niliowakuta, vijana 7 hawakuwa na Biblia, vijana watatu walikuwa na Biblia kubwa, wawili walikuwa na zile za Agano jipya tu.

Kati ya hao vijana 7 ambao hawakuwa na Biblia, vijana wanne walikuwa na simu za Smartphone zenye memory card, na nyimbo nyingi sana za Bongo Fleva. Vijana watatu wao walikuwa na simu nyingine nzuri tu, zenye thamani ya zaidi ya elfu 40.

Hivyo nikagundua kuwa vijana wengi hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu.
Kingine Nilichogundua ni kuwa vijana wengi hawajui kuomba. Nilimsimamisha kijana mmoja ili aombe, aliomba kwa sekunde 57, tena kwa kunong'ona. Binafsi sikumsikia kabisa.

Yapo mambo mengi niliyoyagundua ikiwa ni pamoja na vijana wengi kutokupenda maonyo au kukemewa pale wanapokosea. Kutokuhusika na huduma yoyote wawapo kanisani. Utakuta binti amejipara akapendeza kuliko hata nyanya, lakini hawezi hata kuimba pambio la sifa, haimbi kwaya, hafundishi hata watoto. anakuja kanisani kwa kuchelewa. Anakuta kiti kimefutwa. Anakaa tuu. HAlafu mchungaji akimaliza mahubiri anaita vijana mbele "Haya wale ambao Wanahitaji Mungu awatendee muujiza wa kupata mume au mke watoke mbele niwaombee" Bila aibu unainuka unaenda kuombewa. My friend. Unasubiri U-download huyo mchumba kutoka google au?

Kingine nilichobaini ni kuwa vijana wengi tunachelewa kuingia kanisani. Kijana hana mtoto, hana kuku, hana mbuzi yani hana shughuli yoyote ile lakini anachelewa kanisani.
Sasa basi nikawaza nini kifanyike ili kuweza kumrudisha kijana katika mstari.
Katika Zaburi 119:9 Biblia inasema, "Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Ni kwa kutii na kulifuata Neno lako(MUNGU)

Kumbe njia za vijana zimechafuka. Zimechafuliwa kwa uzinzi, Zimechafuliwa na anasa za dunia hii. Sasa dawa ni kutii na kulifuata Neno la Mungu.
Zaburi 119:11, "Moyoni mwako nimeliweka Neno lako ili nisije nikakutenda dhambi. Dawa ya kuepuka dhambi ni kuliweka Neno la Mungu moyoni. Huwezi kuliweka Neno moyoni kama husomi Biblia. Huwezi kusoma Biblia kama huna. Nunua Biblia na anza kuisoma.

Katika Mhubiri 12:1-14, Sulemani aliyekuwa mfalme mwenye hekima hata Biblia inathibitisha hivyo, ameandika mambo mengi sana kuhusu maisha ya ujana. Anasema kipindi cha ujana ndicho kipindi cha kumkumbuka Muumba maana kuna siku zinakuja ambazo utatamani kufanya mambo lakini itashindikana
Hutaweza kuonda raha tena. Maana meno yatakuwa yameshaanza kung'ooka mdomoni. Hizo nywele ambazo unatumia zaidi ya masaa sita sijui kusuka na saloon, kichwa chote kitajawa mvi, Leo unaona kufunga kilemba ni ushamba nyakati hizo wala hutaambiwa ufunge kilemba. Actually ni nyakati mbaya sana. MKUMBUKE MUUMBA WAKO.

Tambua kuwa wewe ni wakili wa Kristo. Katika 2 Korinto 5:20, Biblia inasema kuwa, " BAsi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo. Kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu, twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu. Vijana tumepewa jukumu la kuupatanisha ulimwengu na Mungu. Na kazi kubwa hapa ni kuwepo kwenye huduma.

Katika makala zangu za nyuma niliwahi kuandika "MAMBO SITA ANAYOTAKIWA KUWA NAYO KIJANA ILI AWEZE KUKUBALIKA KATIKA JAMII" Ukisoma katika 2 Timotheo 4:11-12, Hapa ziko sifa kadhaa anazotakiwa kuwa nazo kijana yeyote yule. Unapokuwa na sifa hizi hakika jamii itakutambua, kanisa litakutambua, pia utaheshimika.

Katika 1Yohana 2:13b, anasema "Nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule mwovu"
14b anasema tena "Nimewaandikia ninyi vijana kwa sababu mna nguvu, na Neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu"

Neno kumshinda mwovu limerudiwa mara mbili katika sura hii moja. Nguvu ya kumshinda mwovu inapatikana kwa kusoma Neno la Mungu na maombi. Tambua kuwa Mungu amekupa nguvu ili umtumikie yeye,

Mafanikio ya huduma ya Timotheo ni kwa sababu alikuwa ni mtu wa kumtumikia Mungu. Muda mwingi alikuwa akitumika na Paulo. Alikubali maonyo, licha ya kuwa alikuwa ni kijana. Pia Timotheo huyu aliyaishi malezi ya wazazi wake kama Paulo anavyosema katika 2Timotheo 1:1-6,

Nafasi ya watumishi wa Mungu kwa vijana.
Wachungaji na watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya kuweza kuwarejeza vijana kwenye mstari. Ni kwa njia ya maombi tu.

Hezekia baada ya kuota kiburi na kumsahau Mungu, Mungu alimtuma Isaya amwambie kuwa atakufa. Hivyo atengeneze Mambo ya nyumbani kwake. Hezekia akatubu na kuomba rehema. Mungu alimponya lakini kupitia utendaji wa mtu mwingine ambaye ni Daudi. Soma Isaya 38:5. Ikiwa na maana kuwa tayari kuna maombi ambayo Daudi aliyaomba akiwa kama Mtumishi wa Mungu, hivyo yakafanyika kama chanzo cha uponyaji wa Hezekia.
Isaya 37:35, Mungu anasema ataulinda mji huu na kuuokoa kwa ajili yake mwenyewe na kwa ajili ya DAUDI MTUMISHI WAKE.

Ina maana katika mji huo kuna juhudi za maombi ya Daudi
Hivyo watumishi wa Mungu watakapoweka juhudi kubwa za maombi ya kuwakomboa vijana juu ya baa hili la kuangukia mikononi mwa shetani, Hakika Kwa maombi yao Mungu atawaponya vijana.
Jambo la mwisho kwetu sisi vijana wenyewe. Tukumbuke kuwa tunahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu katika Maisha yetu, Hatuwezi kumshinda mwovu kama hatuna roho mtakatifu, hatuwezi kuushinda ulimwengu kama hatuna Roho Mtakatifu. Licha ya kumhitaji Roho Mtakatifu katika maisha yetu, Huyo Roho Mtakatifu ndiye atakaehusika katika unyakuo.

Nina mengi ya kuandika ila naamini kwa haya machache umejifunza mengi. Mimi pia kama kijana nimejifunza na kuyatendekea kazi.

Natamani umshirikishe mwenzako unaemfahamu kuwa ni kijana, iwe ni kwenye groups au popote ili kila kijana apate ujumbe huu, ili abadilike.
Ahsante na Ubarikiwe sana.

Makala hii imendikwa na;
Steven Mshiu,
Mwandishi, na mwalimu wa Neno la Mungu,
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

Jumatano, 2 Agosti 2017

NGUVU YA USHUHUDA

NGUVU YA USHUHUDA.
Na Steven Mshiu.
Habari za leo mpendwa rafiki. Naamini una uzima wa kutosha kabisa. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana kwa uzima huu tulio nao.
Leo tumeuanza mwezi wa nane ni matumaini yangu kuwa utakuwa ni mwezi wa ushindi mkubwa sana kwangu na hata kwako pia. Nakutia moyo endelea kuweka juhudi juu ya kile unachokifanya ili uweze kufanikiwa sana.
Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza kwanini huwa tunakwama au kushindwa jambo fulani? Ni wapi ambapo huwa tunakosea ili tujirekebishe? Lakini sikupata majibu. Baada ya kufikiri na kuwaza kwa muda mrefu ndipo nikagundua kuwa kuna kitu kinaitwa USHUHUDA.
Wakati nilipoamua kumkiri Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yangu, na kujiunga na kanisa linalomwabudu Mungu katika Roho na Kweli, Kipindi hicho nilikuwa darasa la saba. Nilikuwa bado ni mtoto sana. Umri kama miaka 12 hivi.
Nilipofika kanisani hapo, na ratiba za ibaada zikiwa zinaendelea kama kawaida ilifika kipindi cha watu kushuhudia matendo makuu ambayo Mungu amewatendea kwa wiki nzima, au mambo Mungu aliyotenda kwenye maisha ya waumini.
Niliona watu kama sita hivi wamesimama na kuanza kushuhudia. Kila mmoja alishuhudia jambo ambalo Mungu amemtendea. Kwakuwa nilikuwa bado ni mgeni sana sikuweza kuelewa ni kwanini watu wanashuhudia na kusema mambo waliyokutana nayo?
Baada ya kutoka ibadani, niliamua kumuuliza swali hilo mama yangu mzazi ambaye ndiye aliyenionyesha njia ya wokovu, na kwa bahati mbaya ni marehemu kwa sasa. Akaniambia, Mtu anaposhuhudia jambo ambalo Mungu amemtendea husababisha kuleta ushindi mkubwa sana. Kwa hiyo kushuhudia ni chanzo cha ushindi.
Niliridhika na majibu yale kuwa kushuhudia ni chanzo cha ushindi. Nakumbuka jambo lingine alilonisisitiza sana kuwa nisiache kusoma Biblia. Sasa siku moja wakati nasoma Biblia nikakutana na andiko kutoka Ufunuo wa Yohana 12:11, "Nao wakamshinda kwa damu ya mwana kondoo na kwa neno la ushuhuda wao ambao hawakupenda maisha yao hata kufa"
Nilipoendelea kusoma maneno haya nilifarijika sana. Ukisoma mistari ya nyuma kwenye sura hii tunaona kuna vita inatokea huko mbinguni kati ya malaika Mikael na shetani, Ilikuwa sio vita ya kawaida. Lakini ushindi mkubwa unatokea baada ya yule joka kutupwa chini kabisa. Lakini chanzo cha ushindi huu ni lile Neno la Ushuhuda kama inavyojieleza kwenye mstari huo tuliouona hapo juu.
Tangu wakati huo nilikipenda sana kile kipindi cha watu kushuhudia katika ibaada.
Unajua unaposhuhudia huenda yuko mtu ambaye amekutana na changamoto kama yako, na amekata tamaa kabisa, akiamini kuwa Mungu hawezi kusaidia, Lakini anaposikia mtu akishuhudia kwamba Mungu amemtendea jambo, Imani ya mtu yule huinuka tena. Imani yake hujengeka tena.
Ngoja nikupe mfano mmoja,
Kipindi fulani alitokea mtu mmoja aliyeitwa Goliath, Mtu huyu alikuwa ni mbobevu wa vita kwa nyakati zile. Alikuwa ni mfilisti. Kwa muda mrefu taifa la Israel lilipigwa sana na mtu huyu Goliath, Katika makala zangu zilizopita nilishawahi kuzitaja sifa za huyu Goliath. Alikuwa ni mtu mkubwa sana kwa umbo(giant) au unaweza kusema alikuwa ni jitu.
Mtu huyu alisababisha adha kubwa sana kwa taifa la Israel. Majeshi yote ya Israel yalijificha mbele ya mtu huyu. Wanaume wote wa Israel waliingia mapangoni. Mfalme Sauli naye hakuweza kupambana na Goliath, japo naye alikuwa ni mtu wa vita.
Kulikuwa na mtu mmoja aliyeitwa Yese. Baba huyu alikuwa na watoto kadhaa na miongoni mwa watoto hawa walikuwa kwenye jeshi la Israel linalopambana na Goliath, Lakini nao walishindwa.
Yese alikuwa na kijana wake mdogo jina lake akiitwa DAUDI. Kwa kuwa Daudi alikuwa ni mdogo yeye hakuruhusiwa kwenda vitani badala yake alikuwa akichunga kondoo wa baba yake.
Wakati akichunga kondoo hao walijitokeza wanyama wakali kama simba na dubu wanaotaka kuwakamata kondoo wa baba yake hivyo Daudi alikuwa akipambana nao hadi kuwaua na kuwaokoa kondoo wale.
Siku moja Daudi alienda kuwaangalia ndugu kule vitani. Akakuta wamejificha. Goliath naye analitukana jina la Mungu, wala hakuna aliyejitokeza kupigana na Goliath..
Daudi akaamua kujitoa kupambana na Goliath. Kumbuka Daudi hana uzoefu wowote ule wa kivita kwa hiyo ilikuwa ni ngumu sana kuaminika. Kwanza ni kijana mdodo sana. Kaka zake wameshindwa. Yeye ataweza? Lakini Daudi alifahamu NGUVU YA USHUHUDA.
Alipopelekwa kwa mfalme Sauli, yawezekana Sauli aliona kama kijana anafanya utani. Hakumwmini kabisa. Daudi akaanza kushuhudia mambo aliyoyafanya. Akasema alipambana na simba hadi akamuua. Alipambana na dubu hadi akamuua, Hivyo Goliath ni kiumbe mdogo sana. Soma zaidi 1 Samweli 17:32-37
Sauli alimfahamu simba na dubu. Hawa ni wanyama hatari sana. Hivyo akamruhusu Daudi. Watu wote walihisi labda huo ndio mwisho wa kijana Daudi. Wakasahau kuwa tayari Daudi alishajitengenezea ushindi wake tangu zamani kwa njia ya ushuhuda. Sipendi niendelee sana ila sote tunafahamu kilichokuta Goliath. Alianguka kifudifudi mbele ya Daudi.
Mpendwa rafiki.
Nataka nikukumbushe mambo machache.
Mungu anapokutendea jambo usiache kushuhudia. Yaseme matendo makuu ya Mungu. Ushuhuda ni chanzo cha ushindi
Ushuhuda hujenga ujasiri. Na ujasiri unaojengeka kupitia ushuhuda humdhoofisha adui.
Mungu amekubariki chochote usiache kushuhudia. Kushuhudia ni njia moja mojawapo ya kuonyesha kushukuru. Mungu anampenda mtu anaeshukuru.
Pia kushuhudia ni njia mojawapo ya kumtangaza Mungu na kuutangaza ukuu wake. Unapomtangaza Mungu kwa njia ya ushuhuda humfanya Mungu kupata sifa. Mungu anaposifiwa yeye hushuka na uwepo wake.
Nikuhakikishie kuwa Mungu atakaposhuka na uwepo wake hutabaki vile ulivyo. Mungu aliposhuka kwa Daudi, Daudi hakuendelea kuchunga kondoo. Aliinuliwa hadi kuwa Mfalme. Kina Shadraki na wenzake walipoamua kumshuhudia Mungu hawakubaki kuwa watumwa. Yusufu alipoamua kushuhudia Mungu, hakubaki kuwa mtumwa. Aliinuliwa hadi kuwa waziri mkuu.
Ushuhuda wako ndio utakaokuweka pale ambapo wewe unataka. Utabarikiwa kulingana na ushuhuda wako. Utakula mema ya nchi kutokana na ushuhuda wako.
Changamoto tuliyo nayo ni kwamba je tunatengenezaje mambo ambayo yatakuwa na nguvu ambayo itakuwa ni ushuhuda mbele za watu na kwa Mungu wetu. Daudi yeye aliua simba na dubu. Haya yalikuwa ni majaribu makubwa sana kwake.
Ili utengeneze ushuhuda mzuri na wenye nguvu ni lazima kuyashinda majaribu makubwa unayokutana nayo. Kama utakuwa ni mtu wa kuanguaka anguka kwenye majaribu madogo madogo sahau kupata ushindi unaotokana na NGUVU YA USHUHUDA.
MUngu akubariki sana. Anza leo kufanya mambo yatakayotengeneza Ushuhuda wako.
Ushuhuda wako ni ushindi wako
Ni mimi rafiki yako,
Steven Mshiu
+255 655 882074
+255 768 882074
smshiu42@gmail.com

MAKUNDI MAWILI YA WATU WANAOKUZUNGUKA.

FAHAMU MAKUNDI MAWILI YA WATU KATIKA MAISHA YAKO. Na Steven Mshiu . Maisha ya kila mwanadamu yamezungukwa na watu. Watu hawa waweza kat...